Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema wananchi bado wana malalamiko mengi juu ya vitendo vya rushwa na kunyimwa haki kufuatia ripoti za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na ya Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA) za kila mwaka.

Amesema taarifa ya PPRA inasema taasisi 44 za umma zilizokaguliwa mwaka 2022/23 inaonesha zabuni 15 zenye thamani ya Tshs 67.27 bilioni zilitolewa kwa kutumia maelezo ya zabuni yenye kubagua baadhi ya wazabuni.

Dkt Mpango amesema hayo leo jijini Arusha wakati akifungua Mkutano Mkuu wa viongozi wa TAKUKURU wa mwaka 2024 na kuongeza kuwa ripoti hiyo imesema wazabuni walichaguliwa na kupewa mikataba 25 yenye thamani ya billioni 56.70 pasipo kuidhinishwa na Bodi ya Zabuni.

“Licha ya jitihada mnazofanya za kupambana na rushwa lakini vitendo vya rushwa bado vinaonekana katika sekta mbalimbali hadi sasa kwa mfano taarifa za TAKUKURU na PPRA zinasema majadiliano ya mikataba 23 ya taasisi 7 yenye thamani ya billioni 64.51 yalifanyika bila kuwepo kwa mpango wa majadiliano”

“Aidha mikataba 60 yenye thamani ya billioni 54.07 ilisainiwa pasipo kuidhinishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali na mikataba 10 ya manunuzi kwenye taasisi 5 yenye thamani ya billioni 7.48 iliongezwa muda bila kufuata utaratibu, ni wazi kuwa dosari hizi katika taratibu za manunuzi zinaashiria uwepo wa rushwa, hivyo ni vema TAKUKURU ifanyie kazi taarifa hizi na kuchukua hatua stahiki” amesema Dkt. Mpango.

Amesema taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zinaonesha kujirudia kwa maeneo ambayo yanahitaji juhudi za makusudi ikiwemo kuzingatiwa kwa taratibu za ununuzi na uwajibikaji kwa fedha zilizotolewa kwa matumizi ya maendeleo na ya kawaida.

Amesema miradi mingi ya maendeleo inayogharimu fedha nyingi za walipa kodi imeonekana kugubikwa na viashiria vya rushwa hivyo utekelezaji wa miradi hiyo kukosa ubora unaotakiwa na unaolingana na thamani ya fedha.

“Kutokana na hayo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge 2024 katika taarifa yake alieleza kuhusu miradi iliyokaguliwa na ambayo ilibainika kukosa ubora na kuiomba TAKUKURU kufanya uchunguzi wa miradi hiyo na kuchukua hatua stahiki kwa watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo, nami kupitia jukwaa hili nawakumbusha TAKUKURU kutekeleza agizo la Mhe. Rais la kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya wasimamizi wa miradi hiyo watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa au ubadhirifu katika miradi hiyo iliyobainishwa” amesisitiza

Akizungumzia mafanikio ya miezi 12 ya TAKUKURU, Mkurugenzi Mkuu Crispin Chalamila amesema Taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa fedha zaidi ya bilioni 18 kupitia kazi za uchunguzi na uokoaji.

Kwa upande wa uendeshaji wa kesi amesema Jamhuri imeshinda kesi kwa asilimia 75.9 tofauti na mwaka jana ambapo Jamhuri ilishinda kesi kwa asilimia 67.7 katika kesi zilizotolewa maamuzi.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu amesema kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanya na serikali kwa Taasisi hiyo ni wazi kuwa changamoto zote zitapungua.

“Serikali imefanya uwekezaji mkubwa TAKUKURU kwa kuboresha mazingira ya kazi kwa kuongeza rasilimali watu, vitendea kazi, samani, majengo mapya pamoja na kuimarisha matumizi ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA) hivyo ni wazi kuwa wananchi watapata huduma bora na kwa wakati” amesema Sangu.