Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango amesema serikali itahakikisha inaondoa changamoto za wakulima katika msimu mpya wa kilimo ikiwemo kusogeza huduma za mbolea ya ruzuku katika maeneo ya jirani zaidi na wakulima.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mbinga akiwa ziarani mkoani Ruvuma. Amesema mkoa huo ni mkoa tegemeo kwa uzalishaji wa chakula nchini hivyo ameitaka Wizara ya Kilimo kutekeleza kikamilifu suala la upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa kiasi cha kutosha na kwa wakati.
Amewasihi wananchi wa mkoa huo kuacha tabia ya kuuza mazao yote pasipo kuweka akiba kwani usalama wa chakula ni vema kuanzia katika ngazi ya kaya ili Taifa liweze kupiga hatua za kimaendeleo.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka watanzania kufanya siasa za hoja ili kuweza kuharakisha maendeleo. Amesema utumiaji wa lugha zisizo na staha bila kuonesha changamoto kwa hoja hupelekea uvunjifu wa amani.
Makamu wa Rais amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo na kuwaasa kutunza miundmbinu mbalimbali katika sekta za afya, elimu na maji.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amesema katika kuimarisha kilimo cha kahawa wilayani humo , serikali inatarajia kufanya uhakiki wa madeni ya vyama vya msingi na vyama vya ushirika ili kuwaondoa wananchi katika adha inayowapelekea kushindwa kununua pembejeo kwa wakati.
Mavunde ameongeza kwamba wakulima watapata mbolea ya ruzuku katika maeneo ya jirani zaidi na kuwataka kutunza namba ya siri ili kuepusha changamoto zilizojitokeza msimu uliopita.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amehitimisha ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Ruvuma.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais24 Julai 2023.Ruvuma.