Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Pwani
Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani ambae pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Isdor Mpango ,amemuagiza Mwenyekiti wa UWT Mkoani Pwani Zainabu Vullu kuhakikisha anavunja makundi yanayoendelea ndani ya Jumuiya hiyo, hali inayosababisha uwepo wa chuki na hata kutofanikisha shughuli za Jumuiya ipasavyo.
Amekemea vitendo hivyo na kusisitiza umoja na mshikamano ili kuimarisha mahusiano ndani ya Jumuiya hiyo na chama.
Akizungumza katika sherehe za kutimiza miaka 46 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere,Dkt Mpango alieleza, UWT bado kuna changamoto nyingi za uwepo wa makundi kitu ambacho ni hatari sana katika Chama.
“Vullu maliza migogoro hiyo,Chama kinatambua kuwa Wanawake ni jeshi kubwa, lakini pasipo na uwepo wa makundi na kuondokana na siasa ya kusema mimi ni wa huyu na mwingine ni yule.”ameeleza .
Aidha amesema WanaCCM watembee kifua mbele kutokana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kutekeleza ilani kwa kiasi kikubwa nchini na katika Mkoa huo.
” Mkisemee Chama kwa mazuri yaliyofanywa ,tukazungumze na wananchi juu ya makubwa yanayofanywa na Serikali”Tukahamasishe watu hasa vijana kujiunga na Chama ili Kuwa na mtaji mkubwa wa wanachama”
Vilevile Dkt Mpango alihamasika na ufaulu wa kidato Cha nne shule ya Sekondari Tumbi ,Kibaha ,ufaulu wa miaka Saba mfululizo ambapo ametoa milioni 50 ikiwa ni motisha kwa walimu 50 wa shule hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge alisema Chama na Serikali Mkoani Pwani kipo katika mahusiano mazuri.
Ameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali Mkoani humo,na kusema bado wanakazi kubwa ya kuendeleza kuwatumikia wananchi na kutatua kero mbalimbali.