Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdory Mpango ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuzindua Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond inayolenga kukusanya Shilingi bilioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara za vijijini na mijini zilizochini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Hatifungani hiyo ni mwendelezo wa mauzo ya Mpango wa Muda wa Kati wa Miaka Mitano unaolenga kukusanya shilingi sawa na dola za Marekani milioni 300.
Mpango huo wa miaka mitano uliidhinishwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Fedha na Mitaji (CMSA) na katika awamu ya kwanza, Benki ya CRDB iliuza Hatifungani ya Kijani ambayo ilikuwa ya kwanza kwa ukubwa kusini mwa Jangwa la Sahara.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyowakutanisha viongozi wa taasisi za umma na binafsi, wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi Dkt. Mpango amesema inafurahisisha kuona taasisi ya fedha za kizalendo ikiongoza mchakato wa kuwaleta pamoja Watanzania na wawkezaji kutoka nje ya nchi kuchangia ujenzi wa miundombinu ya babarabara kuchochea maendeleo ya taifa.
“Nafarijika sana ninapoona taasisi zetu zipo mstari wa mbele kuchochea maendeleo kama ambavyo Benki yetu ya CRDB, kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI na TARURA walivyokuja na hatifungani inayowawezesha Watanzania kuwekeza fedha zao kufanikisha ujenzi wa barabara nchini,” amesema Makamu wa Rais.
Amesema ni mkakati wa Benki ya CRDB kuwashirikisha Watanzania wote kuendeleza miundombinu ya barabara hali itakayoipa serikali shinikizo la kuhakikisha inajenga barabara nzuri na imara kadri inavyowezekana.
Amefafanua kuwa, serikali inafanya kila inaloweza kuhakikisha Watanzania wanainuka kiuchumi na kati ya njia za kufanikisha hilo ni kuboresha miundombinu muhimu zinazochangia maendeleo ya sekta tofauti.
“Pamoja na juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu, tumekuwa na changamoto za malipo kwa wakati. Sasa nategemea kuona makandarasi wakichangamkia fursa hii kikamilifu. Mbali na manufaa kwa nchi na makandarasi, hatifungani hii pia ina faida ya riba ya asilimia 12 kwa wawekezaji kwa kila mwaka kwa miaka mitano ya uhai wake.
“Riba hii italipwa katika kila robo ya mwaka hivyo inafanya mwekezaji kuwa na uhakika wa kipato kila baada ya miezi mitatu. Hakika ni uwekezaji mzuri kwa wote wenye nia na uwezo wa kuwekeza,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema wanafahamu serikali hutenga mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kujenga na kurekebisha barabara zilizoharibika ili kurahisisha ufikishaji wa huduma kwa wananchi, usafirishaji wa bidhaa na mazao pamoja na usafiri wa wananchi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
“Tunajivunia kuja na hatifungani hii maalum inayolenga kukusanya fedha kwa ajili ya miradi ya miundombinu ya barabara za mjini na vijijini. Kupitia hatifungani hii, tunatarajia kukusanya shilingi bilioni 150 zitakazotumika kuwalipa makandarasi wanaoendelea na watakaokuwa wanajenga barabara,” amesema Nsekela.
Kupitia hatifungani hii itakayouzwa kwa siku 30, kuanzia Novemba 29 ilipozinduliwa hadi Januari 17, 2024, Nsekela amesema Benki ya CRDB inatoa fursa kwa kila Mtanzania zikiwamo taasisi na kampuni kuwekeza kiasi chochote kuanzia shilingi 500,000 huku akitarajia kupokea faida ya asilimia 12 kwa mwaka.
Kwa mtu au taasisi inayotaka kuwekeza, Nsekela amesema anaweza kuipata hatifungani hiyo katika tawi lolote la benki katika zaidi ya matawi 260 yaliyopo nchini au akafanya hivyo katika simu yake ya mkononi kupitia SimBanking ikiwa ni Benki ya kwanza barani Afrika kuwezesha wateja na wawekezaji kuwekeza katika hatifungani kidijitali.
“Uwekezaji kwenye hatifungani hii ni salama na wenye faida nzuri. Ukiinunua unakuwa umewekeza kati benki kubwa zaidi nchini yenye uhakika wa kukulipa faida unayoitarajia. Namkaribisha kila Mtanzania mwenye uwezo kuja kushirikiana nasi kujenga barabara zetu,” amesema Nsekela.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA. Nicodemus Mkama kutokana na mafanikio yaliyopatikana kwenye awamu ya kwanza, ana imani mauzo ya Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond nayo yatavuka malengo yaliyokusudiwa.
“Hatifungani ya Kijani ilikusudia kukusanya shilingi bilioni 40 lakini zikapatikana shilingi bilioni 171.82 sawa na asilimia 429.6. Naamini rekodi hiyo itafikiwa tena kama si kuvunjwa kwani Watanzania wapo tayari kuijenga nchi yao. Nitumie fursa hii kuwahamasisha Watanzania kuwekeza kwenye fursa zilizopokatika masoko ya mitaji na dhamana kwani zina uhakika wa kipato,” amesema Mkama.
Waziri wa Ofisi ya Nchi – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
Mohamed Mchengerwa mwenye dhamana na TARURA amesema Benki ya CRDB ndio taasisi pekee iliyoendana na matakwa ya wizara katika mkakati wake wa kutafuta uhakika wa fedha za kufanikisha ujenzi wa barabara nchini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff amesema ushirikiano huu uliotolewa na Benki ya CRDB utasaidia kupatikana kwa fedha kwa wakati kuharakisha ukamilishaji wa miundombinu ya barabara na kutatua changamoto zilizopo katika maeneo tofauti nchini.