Mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha  Mrisho Gambo  akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa uzinduzi rasmi wa Kamati ya kitaifa ya kuandaa Mwezi maalumu wa maadhimisho ya Urithi wa Taifa la Tanzania katikati ni Mjumbe wa Kamati hiyo  na ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya EAG.
 Waziri wa Maliasili na Utalii  Dkt.Hamisi Kigwangala akizungumza katika mkutano na  Kamati ya kitaifa ya kuandaa Mwezi maalumu wa maadhimisho ya Urithi wa Taifa la Tanzania uliofanyika leo kwenye chuo cha Utalii cha Taifa Posta jijini Dar es salaam leo kushoto ni Dkt. Aloyce Nzuki Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasoli na Utalii.
 Mjumbe wa Kamati hiyo  na ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya EAG akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa uzinduzi rasmi wa Kamati ya kitaifa ya kuandaa Mwezi maalumu wa maadhimisho ya Urithi wa Taifa la Tanzania kushoto ni Mjumbe wa Kamati hiyo Jokate Mwegelo.
 Mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa  Simiyu Anthony Mtaka akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa uzinduzi rasmi wa Kamati ya kitaifa ya kuandaa Mwezi maalumu wa maadhimisho ya Urithi wa Taifa la Tanzania wanaofuatia katika picha ni wajumbe wa kamati hiyo Mkuu wa Mkoa wa Iringa mama Amina Masenza, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, Jokate Mwegelo na Imani Kajula
 Wajumbe wa kamati hiyo kutoka kulia ni Wema Sepetu na Dkt. Sebastian Ndege pamoja na wajumbe wengine

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangala amekutana na Kamati ya Kitaifa ya kuratibu shughuli za maandalizi ya Mwezi Maalum wa Maadhimisho ya urithi wa Taifa la Tanzania ili kukwepo na mwezi maalum wa kusherehekea Urithi wa Taifa la Tanzania

Pamoja na mambo mengine, Kamati hiyo ya kitaifa inategemewa kuandaa utaratibu maalam kwa Watanzania wote ndani na nje ya nchi kushiriki kikamilifu  kupitia midahalo na programu mbalimbali za kielimu; matamasha mbalimbali yakiwemo michezo ya jadi; vyakula vya asili na vazi la Kitaifa.

Dk.Kingwangala amkutana na kamati hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati akizundua rasmi kamati hiyo ya maandalizi ambapo pia wameamua kwa pamoja jina la maadhimisho hayo ambapo tayari wamekubaliana yatakuwa yanafanyika kila ifikapo Septemba ya kila mwaka.

Ametumia nafasi hiyo kuelezea kuwa lengo la mwezi wa urithi huo wa taifa la Tanzania ni kutoa nafasi ya kuiweziwezesha jamii kuutumia urithi ambao taifa limejaliwa nao kama zao la utalii na hivyo kuchangia kiuchumi katika jamii na taifa kiujumla.

“Pia maadhmisho hayo yatatumika kuelimisha jamii kuhusu kumbukumbu tulizonazo na namna ya kuzitumia kikamilifu katika kuendeleza Taifa na kuboresha maisha yao. Kuzikumbusha jamii chimbuko la tabia, mila na desturi za watanzania

“Na kuzitambua na kuzienzi mila na desturi za makabila mbalimbali ya nchi hii pamoja na kuhakikisha kuwa matamasha yote ya utamaduni yanafanyika katika mwezi husika (mwezi wa urithi) ambao tumekubaliana iwe Septemba ya kila mwaka,”amesema Dk.Kigwangala.

Amefafanua kuwa lengo la wizara yake ni kuhakikisha wanaunganisha wadau katika kuthamini, kuendeleza na kuhifadhi uritihi wa taifa.Hivyo amehimiza taasisi zote za umma na binafsi zinazojihusisha na masuala ya urithi kujiandaa kikamilifu na kuunga mkono dhamira hiyo ili kufanikisha lengo hilo kwa manufaa ya Taifa letu.

“Nichukue fursa hii kuwaomba wajumbe wateule kushirikiana ili kutekeleza lengo hili ili kuendeleza juhudi za kukuza sekta ya utalii kwa manufaa ya Taifa letu. “Ingawa najua kuwa sote tuna majukumu mengine ya kitaifa, ushirikiano wa wanakamati wote pamoja na watendaji wa Wizara yangu ndio utarahisisha ufanisi wa kazi hii. Niwahakikishie mimi na watendaji wa Wizara yangu tutakuwa nanyi bega kwa bega ili kufanikisha kazi hii,”amesisitiza.

Amefafanua urithi huu wa Taifa ni miongoni mwa vivutio vya utalii kwa kuwa ni vielelezo vya historia, utamaduni na ustaarabu wa jamii katika hatua mbalimbali za maisha. “Urithi huu huonesha na kuikumbusha jamii husika chimbuko la tabia, mila na desturi ambazo inazitumia katika nyanja za uchumi, siasa, teknolojia na elimu.

“Jamii yoyote ile inatambuliwa, kuthaminiwa na kuheshimiwa kutokana na urithi wake. Kwa sababu hiyo, tuna kila sababu ya kuendeleza urithi huu tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu,amesema.

Hivyo kwa kutambua umuhimu huo wa kuuenzi, kuutangaza na kuutumia uritihi wa Taifa la Tanzania kama kivutio cha utalii na kumbukumbu za Taifa, Wizara yake imeona ni vema kukwepo na mwezi maalum wa kusherehekea Urithi wa Taifa la Tanzania .