Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. John Jingu ametoa rai kwa wakulima kuongeza msukumo katika kilimo chenye tija kwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo ambazo zinahusisha teknolojia ili kuleta matokeo mazuri zaidi.

Wito huo ameutoa katika kikao cha Kamati ya Tathmini ya Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili kilichohusisha Makatibu Wakuu na Wadau wa Kilimo kilichofanyika jijini Dar es Saalam.

Katibu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. John Jingu akizungumza katika kikao alichokiongoza cha Tathimini ya Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili.

Dkt. Jingu amesema dhamira ya Serikali ni kuona wakulima wanatumia rasilimali kidogo na kupata faida zaidi.

Ameongezea kuwa Serikali itaendelea kubuni mbinu mbalimbali za kufanya katika kuimarisha sekta ya Kilimo na Mifugo ili kuongeza ufanisi kwa manufaa ya Taifa.

“Mwelekeo ni kwamba shughuli wanazofanya ziwe na mwelekeo wa kibishara kwa maana kilimo ni biashara na uvuvi ni biashara,” amesema Dkt.Jingu.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla amesema Uvuvi wetu bado tunatumia mbinu za zamani lakini sasa tunaenda kutoa boti mpya za kisasa zitakazofanya wavuvi waongeze tija.

Ameongeza kusema kuwa, jitihada hizo zinaenda sambamba na kutoa mikopo kwa wafugaji wa samaki kwenye vizimba katika ziwa Viktoria kwa kuwapatia vizimba vya samaki na vifaranga vya samaki na chakula cha samaki.

“Lengo ni kuongeza uzalishaji wa samaki na kutimiza malengo tuliyopewa na Mhe. Rais wa kuongeza tani za uzalishaji wa samaki ifikapo Mwaka 2026,” amesema Dkt.Madalla

Aidha Serikali itaenda kutoa mikopo kwa wakulima wa zao la Mwani katika ukanda wa Pwani ili waweze kununua vifaa na waweze kuongeza uzalishaji wa zao la Mwani.

Makatibu Wakuu na Wadau wa Kilimo wakiwa katika Kikao cha Tathimini ya Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili kilichofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dar es Salaam.

“Tunaimani zao hili litakuwa na mchango mkubwa sana katika kuinua kipato na kuboresha maisha hasa kwa wakina mama ambao ndiyo wakulima wakubwa wa zao la Mwani na vyote hivi ni katika utekelezaji wa Usimamizi na Ushauri wa Programu ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili,”amesisitiza Dkt. Madalla.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Maduhu Kazi amesema Mpango wa Usimamizi na Ushauri wa Program ya Kuendeleza Kilimo Awamu ya Pili ni mpango jumuishi unaohusisha wizara kupitia Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi ambayo yanajihusisha na shughuli mbalimbali za kilimo na uwekezaji.

Please follow and like us:
Pin Share