Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Mafia

Wanawake nchini wameaswa kujiamini kwa kupaza sauti zao ili kukabiliana na wimbi la vitendo vya ukatili vinavyowakabili.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima alikutana na wananchi wa Kata ya Kirongwe ,wilayani Mafia alipotembelea eneo hilo hivi karibuni kukagua uundwaji wa Kamati za kupambana na ukatili wa wanawake na watoto wilayani humo. 
 
Akionesha kutoridhishwa kwake na uhai Mabaraza ya Watoto na Kamati za MTAKUWWA hasa kwenye ngazi za Vijiji na Kata, Waziri Gwajima aliahidi kurudi wilayani Mafia na kupiga kambi ili aweze kuwafikia hadi wananchi walio katika visiwa vingine vidogo vidogo vinavyounda wilaya hiyo.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (mwenye kilemba chekundu) akijumuika kucheza na akina mama wakati wa Kongamano la Wanawake Mafia.

Vilevile Dkt. Dorothy Gwajima amewapongeza akina mama wilayani Mafia kwa kuandaa Kongamano la kuhitimisha wiki ya maadhimisho ya mapambano dhidi ya ukatili kwa wanawake na watoto. 

“Nimefurahishwa sana kwa jinsi mlivyojitokeza kuungana kupaza sauti zetu kupinga kwa dhati matukio ya kikatili wanayofanyiwa wanawake na watoto”

Awali, Mhe. Dkt. Gwajima alipokea taarifa kuwa matukio yanayoongoza kwa wilaya ya Mafia ni; ubakaji, ulawiti, mimba za utotoni na mashambulio ya aibu.

Kwa Mwaka 2021/2022 jumla ya matukio 493 yalitolewa taarifa katika Ofisi za Ustawi wa Jamii na kituo cha Polisi ambapo matukio 56 yalikuwa ya ubakaji na ulawiti, kutelekezwa 64, shambulio la mwili 134 na shambulio la aibu matukio 239. 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (kushoto) akipokea kutoka kwa mmoja wa washiriki wa Kongamano la Wanawake Mafia, zawadi ya mfano wa samaki aitwaye Papa Potwe,Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhandisi Martin Ntemo.

Kati ya kesi hizo zilizotolewa taarifa, kesi 53 zipo Mahakamani na kesi 4 wahusika wamefungwa ambapo mmoja amefungwa maisha, kesi 5 wapo katika kifungo cha nje, kesi 11 zimekosa ushahidi na kesi 9 zinaendelea.

Pamoja na hayo ,”Watu wengi hawajapata fursa ya kujionea maeneo ya kuvutia kiasi hiki! mimi nimeamua kuwa Balozi wa hiari wa kukitangaza kisiwa cha Mafia, ni kisiwa chenye vivutio vingi sana” alifafanua Dkt. Dorothy Gwajima.