Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amefuatilia maendeleo ya ulipaji fidia kwa wananchi wa maeneo ya Mwasonga, Sharifu na Madege yaliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam ili kupisha eneo linalotarajiwa kujengwa mradi wa uchimbaji madini ya mchanga mzito (heavy mineral sands) utakaotekelezwa na Kampuni ya Nyati Mineral Sands Limited.

Waziri Biteko amesema madini hayo yanapatikana sehemu mbalimbali zenye mwambao wa bahari ambapo Serikali inatamani kujengwa kwa kiwanda kikubwa cha madini hayo ili kusaidia kuongeza ajira kwa Watanzania; kuimarisha huduma za afya; kuboresha elimu kwa Watanzania na kukusanya kodi zitokanazo na madini hayo.

Aidha, Dkt. Biteko amesema kujengwa kwa kiwanda cha madini hayo kutapelekea kutokea mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii ambapo amewataka wananchi wa Kigamboni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuvutia na kukaribisha wawekezaji nchini.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Biteko amesema, Nyati Mineral Sands Limited ni Kampuni inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 16 na Kampuni ya Strandline Resources Limited kwa asilimia 84 ambapo eneo la leseni hiyo lina jumla ya hifadhi ya mashapo ya tani milioni 12.3 za madini hayo na yanaweza kuchimbwa kwa miaka 6 hadi 8.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kigamboni Dkt. Faustine Ndungulile amempongeza Dkt. Biteko kwa kufanya ziara katika jimbo hilo ambapo wananchi wanalalamika kulipwa fidia ndogo ukilinganisha na bei ya soko ya ardhi katika maeneo mengine ya jijini Dar Es Salaam.

“Naomba nichukue nafasi hii kukupongeza Mheshimiwa Waziri kwa kusikia kilio cha wananchi na kufunga safari kuja kuwasikiliza, naamini leo utazimaliza kero zote zilizopo katika Wilaya ya Kigamboni,” amesema Ndungulile.

Naye, Afisa Malalamiko wa Kampuni ya Nyati Mineral Sands Limited Bi. Annagrace Rwehumbia amesema mpaka sasa kampuni hiyo amekamilisha fidia kwa asilimia 82 pamoja na kuwa na changamoto ya baadhi ya wananchi kutoridhika na kiwango cha fidia kinachotolewa.

Rwehumbia amesema kuwa kampuni hiyo inatarajia kusafirisha madini hayo nje ya nchi mara baada ya ujenzi wa mgodi kukamilika. Madini hayo ni kwa ajili ya matumizi ya viwandani hasa katika uimarishaji na uongezaji ubora wa vigae na kutengenezea rangi za magari.