Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, akihutubia kwenye Mkutano wa 53 wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika, amewataka washiriki wa mkutano huo kutumia jukwaa hilo kikamilifu kwa kuimarisha ushirikiano, kubadilishana mawazo bunifu na kuendeleza mikakati inayotekelezeka ambayo italeta manufaa makubwa kwa bara la Afrika na watu wake.

Dkt. Tulia ametoa kauli hiyo leo tarehe 3 Oktoba, 2024 wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika katika Ukumbi wa Grand Melia, Jijini Arusha uliofunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, akimuwakilisha Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika mkutano huo ambao umehudhuriwa na Maspika na Wabunge kutoka zaidi ya nchi 19 za Barani Afrika, Dkt. Tulia alitumia fursa hiyo kuwashukuru wajumbe wa Umoja huo kwa kumchagua kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Aidha, aliwasihi washiriki hao kutumia uwepo wao mkoani Arusha kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika Mkoa huo ili kufurahia uzuri na urithi wa nchi ya Tanzania.