Na Ruja Masewa, JamhuriMedia, Mbeya
Kufuatia mkwaruzano baina ya Dk. Wilbroad Slaa na CHADEMA, mara baada ya kuachiwa huru na Mahakama amesema, kuanzia leo Machi 23, 2025 anaanza kutangaza ‘No reforms, No Election’ (bila mabadiliko hakuna uchaguzi).
Slaa alisema hayo kwenye mkutano wa CHADEMA wa uzinduzi wa ziara ya No reforms, No election, mkoani hapa iliyohudhuriwa na viongozi wake wakuu, akiwemo Mwenyekiti wa Chama Tundu Lissu na viongozi wa dini.
Akishangiliwa na wananchi kwenye mkutano huo uliofanyika kwenye viwanja vya Ruanda Nzovwe, Slaa amekichana Chama cha Mapinduzi (CCM) akidai, amerudi CHADEMA kudai haki na kauli ya Mwasisi Marehemu Julius Nyerere aliyowaambia, wasipowasikiliza wananchi, “Watachukua nchi yao”.
Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa Joseph Mbilinyi (Sugu) akiwakaribisha viongozi wa kitaifa na wananchi Mbeya alisema, hatuwezi kuingia katika uchaguzi kwa mazingira yaliyopo, watu wauwawe, waumizwe, wapate vilema ndipo tutangazwe.
“Tupo hapa kudai Tume Huru ya Uchaguzi, tunaomba wananchi,walimu,Polisi mtuunge mkono ili kuhakikisha kuna uwepo wa chaguzi huru”.alisema.
Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa Deogratius Mahinyira alisema, kauli ya hatutashiriki na hatutasusia uchaguzi sio ya CHADEMA. Kauli CHADEMA ni yasipokuwepo mabadiliko ya mfumo na sheria za uchaguzi hakutakuwa na uchaguzi.
“Kauli ya Waziri mkuu ya vijana waliohitimu Shahada waende VETA, wanakimbia majukumu yao. Mlinzi pekee wa rasilimali za nchi ni kura zenu” alisema Mjumbe wa Kamati Kuu ya Rose Mayemba.
Aidha Mwenyekiti Tundu Lissu alisema, tuunganishe nguvu, umwambie jirani, ndugu, rafiki, mwanao, mzazii, viongozi wa dini, Polisi, na vyama vingine, dunia na kila anayependa nchi hii tukwamishe uchaguzi ujao, tutengeneze utaratibu bora wa kufanya chaguzi .
“Hili jambo linatuhusu sisi sote, tukiunganisha nguvu zetu itawezekana,hatuombi kitu ambacho hakijawahi kusemwa nchi hii tunadai haki tu, haki huinua taifa, wenye haki wakipata amri watu hufurahi, Waovu wakitawala watu huugua” alisema.
