Tea/sept2
lead
*Amwanika alivyohaha kujiunga Chadema
*Aeleza alivyotumia Uspika kuasi CCM
*Afichua hotuba aliyoandaa kujitoa
Siri za mkakati wa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, wa kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), zimeanza kuvuja.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, ametoboa siri nzito ikiwamo ya nakala ya tamko aliloliandaa Sitta, kwa ajili ya kulisoma kwa waandishi wa habari baada ya kujiunga Chadema.
Dk. Slaa ameiambia JAMHURI kwamba Sitta ni mbinafsi, mroho wa madaraka na ni kwa sababu hiyo, Chadema walisita kumkubali hasa kutokana na shinikizo la kutaka Mabere Marando aenguliwe kuwania kiti cha Spika, badala yake apewe nafasi hiyo yeye Sitta.
“Sitta si mwadilifu, ninayasema haya ili kama atathubutu kujibu, basi niweke hadharani hadi tamko lake aliloliandaa la kujitoa CCM na kujiunga Chadema yeye na viongozi wenzake waasisi wa Chama cha Jamii (CCJ). Tunalo lile tamko, alituletea ili turekebishe ili yeye na wenzake wa CCJ waje Chadema.
“Tulilikataa kwa sababu halikuwa la kisheria, alimtumia mtu anaitwa Makonda kama kiunganishi kati yake na sisi Chadema. Ninazo silaha (vielelezo), namvutia pumzi nitazitoa akijitokeza kukanusha haya ninayosema. Akitaka tutaweka hadharani kila kitu,” amesema Dk. Slaa.
Dk. Slaa amesema vikao vingi vya kujiunga Chadema viliendeshwa ndani ya ofisi ya Spika mjini Dodoma na jijini Dar es Salaam.
“Huyu ni mhaini. Vikao vya yeye kuihama CCM vilifanyika ndani ya ofisi ya Spika. Ni muasi huyu, akiendelea kutuchokoza tutatoa vielelezo… kwa kitendo hicho ndiyo tukaanza kuona huyu mtu mzima ni hovyo, akiendelea kutusakama tutampa haki yake (kumuumbua). Ajibu hoja, asilete propaganda.
“Inavyoonekana sasa ni kwamba amepoteza kumbukumbu, ana matatizo ya kuhifadhi kumbukumbu zake kichwani. Tena, viongozi halisi wa CCJ ni Sitta na wenzake. Mpendazoe alishatoa orodha yote,” amesema.
Dk. Slaa amesema Sitta alitaka kujiunga Chadema kwa masharti ya kugombea Uspika, lakini baadaye akapunguza kasi baada ya kuwa ameahidiwa kuteuliwa kuwa naibu waziri.
“Akaja akatueleza kuwa ameahidiwa unaibu waziri na yeye hautaki, kama ni uwaziri basi awe waziri kamili. Akasema kama mpango ungekuwa kupewa unaibu waziri, basi Chadema wamwondoe Marando ili yeye agombee Uspika,” amesema.
Anasema wakati alipoambiwa hivyo na kwamba kuwa hakubaliani na nafasi ya unaibu waziri, akaanza kupata shaka kama anaweza kuwatumikia Watanzania kiuadilifu kwa kuwa alionesha dalili kuwa anachowaza ni nafasi ya juu zaidi badala ya kuwatumikia watu.
“Huyu mtu si mzalendo kama anavyotaka watu wamwamini, ana uroho wa madaraka, ubinafsi na mroho wa vyeo. Anachotaka ni kuhakikisha anajinufaisha yeye na tumbo lake.
“Baada ya CCM kupata fununu kuwa anataka kujiunga Chadema kwa sababu hataki unaibu waziri, wakaahidi kumpa uwaziri kamili. Alipoupata hakurejea tena Chadema. Kumbuka ni huyu huyu aliyekuwa anapiga simu saa 9 usiku tunakesha hadi saa mbili. Akasema saa nane mchana anaenda Tabora (jimboni kwake Urambo) kuaga.
“Akasema baada ya kurudi tamko angelitoa Jumatatu, matokeo yake hakwenda Urambo, akabaki Dar es Salaam akaapishwa uwaziri,” amesema Dk. Slaa.
Dk. Slaa amekanusha madai kwamba Chadema inamsaidia Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kwa kuwashambulia maadui zake ili kumsafishia njia mwanasiasa huyo aweze kuwania urais mwaka 2015.
“Huu ni uongo wa hali ya juu, mimi sina kambi na wala Chadema hatuna filosofia hiyo. Sijifurahishi na mtu yeyote isipokuwa ukweli tu,” anasema.
Akiwa Iringa, Dk. Slaa alisema, “Huyu mtu haaminiki hata katika dhamira yake, kwa kuwa tulikutana zaidi ya mara 100 na hata tukawa tunaandikiana vimemo, yeye akiwa katika kiti cha Spika. Kama anabisha leo akanushe juu ya uhaini wake dhidi ya CCM,” amesema.
Dk. Slaa alikuwa akijibu kauli iliyotolewa na Sitta aliyedai kwamba Chadema haistahili kupewa madaraka kwa kuwa haina watu wenye uzoefu wa uongozi.
Sitta alidai mwenye uzoefu wa uongozi ndani ya Chadema ni Dk. Slaa pekee, na kwamba Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe uzoefu pekee alionao ni kuongoza kumbi za disko. Alitoa kauli hiyo mjini Karagwe, Kagera.
Akijibu hoja hiyo, Dk. Slaa alidai kuwa mara kadhaa walipokutana, Sitta akiwa Spika alimweleza kuwa ana kundi la wabunge 55 waliokuwa tayari kuondoka CCM, na kwamba wangefanya hivyo siku tatu kabla ya Bunge la mwaka 2010 kumalizika.
Alisema kuwa ukigeugeu wa Sitta haukuishia baada ya uchaguzi, bali hata wakati wa mchakato wa kumpata Spika wakati baada ya kutoswa na CCM, alihangaika kuwapigia simu viongozi wa Chadema akiwaomba wampe nafasi ya kugombea nafasi hiyo.
Dk. Slaa amesema mwaka 2010 Sitta akiwa na Dk. Harrison Mwakyembe na Fred Mpendazoe wakiwa ni waanzilishi wa CCJ, walikutana na viongozi wa Chadema katika ofisi za Spika mjini Dodoma na akawaeleza kuwa wanaanzisha chama hicho na ikishindikana watahamia Chadema.
Anasema baada ya kukubaliana na kuiangalia Katiba ya CCJ na kubaini kuwa ilikuwa inalingana na ya kwao, wakakubaliana Sitta awe mgombea urais kupitia Chadema. Hata hivyo, Sitta aliwageuka wenzake na akaendelea kubakia CCM.
Kwa upande wake, Sitta amekuwa akisema kwamba hasira za Chadema dhidi yake zinatokana na uamuzi wa yeye kukataa kujiunga na chama hicho. Anasema Chadema ndiyo waliokuwa mstari wa mbele kumtafuta ajiunge katika chama hicho, lakini mara zote amekuwa akikataa.