Ni miaka saba sasa tangu Dk. Ali Mohammed Shein, Rais wa Awamu ya Saba Zanzibar kushika hatamu za uongozi wa Visiwa vya Zanzibar baada ya ushindi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mengi yalisemwa na kuandikwa kuhusu utawala wake utakavyokuwa kabla na baada ya kuchaguliwa mwaka 2010 na mwaka 2016 katika Uchaguzi wa marudio. Wapo waliotabiri kuwa hatakuwa na jipya lolote, lakini wengine walibashiri umakini, weledi na uwajibikaji wake.
Katika nadharia ya uongozi, usomi wa ngazi mbalimbali si sifa ya mtu kufaa kuwa kiongozi bora. Zanzibar na nchi nyengine katika historia yake imesheheni majina baadhi ya viongozi ambao walikuwa wasomi, lakini hatima ya uongozi wao haikutofautiana na wajinga.
Wapo vigogo katika utumishi wa umma, wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, wakuu wa mikoa na wilaya, madiwani, makatibu wakuu, makamishna, wakurugenzi -nawataja kwa uchache- ukiona shahada zao za usomi utaingia woga, lakini utendaji wao baadhi yao ni kichefuchefu.
Dk. Shein si katika aina ya wasomi hao. Yeye ni msomi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika fani ya afya ambaye usomi wake haukuwa kikwazo kwake katika kutenda yaliyotarajiwa na umma.
Ingawa wapo watakaosema haya na yale, lakini ukweli utabaki kuwa hivyo maana kila aliye na macho anaona umakini wake, utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama chake na ahadi alizotoa akiwa mgombea mwaka 2010 na mwaka 2015. Anaendelea kuzitimiza.
Zanzibar hivi sasa imetulia kisiasa kwani kama si busara na kuwa muumini wa utawala bora pamoja na sera madhubuti za CCM, pengine leo tungekuwa tunazungumza mengine.
Licha ya kupitishwa kwa marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar yaliyobadili mfumo wa utawala kama angetaka kuipuuza Katiba kwa kutotekeleza angeweza kufanya hivyo, lakini kwake yeye hilo si muhimu. Jambo la lazima na muhimu ni kusimamia misingi ya utawala bora Zanzibar.
Rais Shein, si mtu mwenye visasi, chuki, si mtu wa kujilimbikizia mali. Katika kipindi cha miaka mitano kama hichi angekuwa kiongozi tama, basi leo ungesikia miguno kutoka kwa wananchi kuwa ahaa jumba lile la Shein, kiwanda kile cha mwanawe- licha ya kuwa pengine mwanawe anastahiki kuwa hivyo, lakini watu wasingefahamu hivyo.
Kwanini iwe sifa zote hizi kwa Rais Dk. Shein? Jibu ni kwamba yeye ndiye ameweza kutekeleza ahadi zake bila kuchelewa au kubadili msimamo. Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu aliahidi kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa Serikali.
Tayari  sasa watumishi wa umma Zanzibar wanalipwa kima cha chini cha mshahara Sh 300,000 kwa mwezi. Hii ni hatua nzuri ambayo haiwezi kubezwa na mtu mwenye akili timamu.
Hakuishia kuongeza mshahara tu, bali Serikali anayoiongoza imefanya mageuzi makubwa ya mfumo wa utumishi wa umma ambako zile kada ambazo zinahitaji uangalizi maalum zimepewa kipaumbele kama walimu na madaktari.
Naamini, dhamira zake za kuboresha maslahi ya watumishi wa Serikali inatokana na kazi nzuri aliyofanya katika kipindi chake cha uongozi wa miaka saba. Katika kipindi hicho tumeshuhudia kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar.
Gugu la ujinga lililokuwa limetamalaki katika siasa za Zanzibar wakati huo lilianza kukatwa mwishoni mwa mwaka 2010 baada ya wananchi walio wengi kumchagua kwa mara ya kwanza Dk. Ali Mohammed Shein kuwa Rais na akaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Pamoja na changamoto zake, lakini Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar chini ya Rais Dk. Shein iliweza kubadili historia ya kisiasa Visiwani Zanzibar ambako siasa za kushupaliana zimezikwa katika kaburi la sahau.
Kila mmoja anafahamu kuwa mkataji wa gugu hilo ambalo liliwapa shida walimaji wengi katika shamba la siasa, si mwengine, ni Rais wa Awamu ya Saba Zanzibar, Dk. Shein.
Nyota yake kisiasa ilianza kung’aa mapema zaidi katika viunga vya Zanzibar. Kila mmoja ni shahidi wa uwajibikaji wake alipokuwa Naibu Waziri wa Afya Zanzibar chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar, wa Awamu ya Tano ‘Komando’, Dk. Salmin Amour; alipokuwa Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar wakati wa Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Amani Abeid Karume na alipokuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Umri wake umeingia katika utu uzima na kuanza kugusa uzuri wa nywele zake, lakini katika mwili wake bado nguvu na maarifa yanafanyakazi tena kwa kiwango kikubwa.
Dk. Shein anajali mambo na kushiriki katika shida za watu kama ilivyojitokeza alipoingia madarakani aliapoanza kuwatetea wananchi wanyonge kuwa na maisha bora.
Wale waliokuwa wakichelewa kulipwa viinua mgongo vyao sasa hawachelewi tena, lakini pia chini ya uongozi wake, Serikali inawalipa wazee wote waliofikia umri wa kustaafu hata kama hawakuwahi kufanyakazi serikalini wanalipwa pesa kila mwisho wa mwezi Sh 20,000.
Mara nyingi watu wanapozungumzia maendeleo kama dhana ya kifalsafa huwa tunafikiria uwezo wa mtu binafsi wa maisha yake kuwa bora, kuondokana na hali ya dhiki na kujiendesha mwenyewe.
Mambo hayo ndiyo anayoyasimamia Dk. Shein katika uongozi wake na hata ukisoma ilani ya uchaguzi anayoinadi masuala hayo yamefafanuliwa kwa kina.
Dunia ya leo ni yenye kuheshimu matakwa ya watu. Wananchi wanavyotaka ndivyo viongozi wanavyopaswa kuwa na kufanya. Kinyume chake ni kukaribisha mivutano na mitafaruku isiyokuwa na manufaa kwa jamii.
Rais Dk. Shein katika pindi cha miaka miaka saba cha uongozi wake amekuwa msikivu, anaejali matakwa na maoni ya wananchi na kwa sababu hizo Zanzibar imetulia kisiasa – amani na utulivu vimetamalaki.
Vyombo  vya habari vya ndani na nje ya nchi, wanasiasa wamekuwa wakimkosoa wengine kwa chuki tu, wengine kwa nia njema, lakini kama ilivyo sifa ya kiongozi bora, Rais Dk. Shein hawachukii wala kuwa na nongwa zaidi ya kuendelea kuchapa kazi na kuyasimamia yale anayoyaamini.
Dk. Shein si katika aina ya viongozi wanaofuata hisia zao, au vionjo vyake; hofu, wivu, woga, wasiwasi, hasira, chuki, kinyongo havina nafasi katika uongozi wake.
Rais Dk. Shein si mbabe, ni muungwana, mpenda watu na hana chembe hata nduchu ya ufisadi, ni mwadilifu hasa na kwa maana hiyo ndipo wanafalsafa wa “existentialism” ndio waliokuwa wa mwanzo kubuni misingi mipya ya falsafa iliyopita.
Wanafalsafa hao waliamini kwamba mambo hayo yote yanaambatana na uhuru pamoja na mtazamo rahisi kuhusu maisha aliyokuwa nayo mtu. Rais Dk. Shein, Serikali anayoiongoza inajali watu na kwa kupima matokeo ya utendaji unaweza kukubaliana nami kuwa Zanzibar inaelekea pazuri katika kufikia maendeleo endelevu.
Wazanzibari wa leo wanahitaji maisha bora na kuongozwa katika misingi ya amani, utulivu na haki. Hayo yote tumeyashuhudia yamesimamiwa kwa umakini mkubwa na Rais Shein, hivyo wananchi wa Zanzibar hawakukosea kumchagua kuwaongoza.
Kimsingi uamuzi (choice) wanao watu wapigakura ambao kwa desturi ya binadamu hawawezi kuacha kumuunga mkono kiongozi makini na mwadilifu wakachagua viongozi wengine ambao hawajawaona utendaji wao.
Kizazi cha leo hakitaki porojo. Kinahitaji kuona hali zao za maisha zinakuwa bora, sera za CCM na ilani yake imejiegemeza katika kuendeleza maisha bora kwa Wazanzibari wote na hilo lilianza tangu mwaka 1964 muda mfupi baada ya kuangushwa kwa utawala mkongwe wa kisultan.