Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akizunguma na Mtukufu Dk. Sheikh Sultan Bin Mohammed Al Qasimi alipofika katika makaazi yake kwa mazungumzo akiwa katika ziara yake katika Nchi za Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu.

ZANZIBAR na Sharjah zimekubaliana kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wao uliopo katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo elimu na biashara,

Katika mazungumzo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Makaazi ya Mtukufu Dk. Sheikh Sultan Mohammed Al Qasimi mjini Sharja, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na kiongozi huyo wote kwa pamoja walisisitiza haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kwa lengo la kuimarisha sekta hizo muhimu za maendeleo.

Rais Dk. Shein kwa upande wake alimpongeza Dk. Sultan kwa hatua zake za kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo ukiwemo mradi wa maji.

Pamoja na hayo, viongozi hao walizungumza jinsi ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano katika kuimarisha sekta ya elimu hasa ikizingatiwa kuwa Sharjah imeweza  kupata mafanikio katika sekta hiyo kutokana na kuwa na miundombinu mizuri ya elimu vikiwemo vyo vikuu.

Aidha, Dk. Shein alieleza haja kwa Sharjah kutoa ushirikiano wake kwa Zanzibar katika sekta ya elimu kupitia Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), jambo ambalo Dk. Sheikh Sultan Mohammed Al Qasimi ameliunga mkono.

Pia, viongozi hao kwa pamoja, wameeleza namna ya pande mbili hizo kushirikiana katika sekta ya biashara hasa ikizingatiwa kuwa kuna bidhaa ambazo ziko Zanzibar na zinatumika sana nchini Sharjah vikiwemo viungo ambapo nchi hiyo wamekuwa wakinunua kutoka nchi za mbali ikilinganishwa na masafa kati ya Zanzibar na Sharjah.

Dk. Shein, pia alitumia fursa hiyo kumueleza Dk. Sultan hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii zikiwemo uhifadhi wa Mji Mkongwe wa Zanzibar ambapo tayari serikali imejenga ukuta wa kuzuia athari za maji ya bahari katika eneo la Mizingani kuelekea katika bustani ya Forodhani.

Kwa upande wake Dk. Sheikh Sultan nae alimueleza namna Sharjah ilivyokuwa na uhusiano na ushirikiano na Zanzibar kwa muda mrefu jambo ambalo amehakikisha ataliendeleza na kuliimarisha kwa lengo na manufaa ya pande zote mbili.

Pia, Dk. Sheikh Sultan alimuleza Rais Dk. Shein namna Sharjah ilivyopiga hatua katika sekta ya elimu sambamba na inavyotoa fursa za ufadhili wa masomo na kusisitiza kuwa kuna kila  sababu na Zanzibar nayo ikafaidika na fursa hizo.

Aidha, Dk. Sultan alimueleza Dk. Shein fursa mbali mbali za kibiashara zilizopo Sharjah na kusisitiza haja ya kuwepo mashirikiano kati ya pande mbili hizo ili sekta hiyo ilete manufaa kwa pande zote mbili hizo.

Katika kuendeleza na kukuza sekta ya biashara na utalii kati nchi mbili hizo, Dk. Sultan alimueleza Rais Dk. Shein umuhimu wa kuwepo usafiri wa ndege wa moja kwa moja kati ya Zanzibar na Sharja na kusisitiza kupitia Shirika la ndege la Sharjah hilo atahakikisha analiweka katika vipaumbele vyake katika kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo.

Katika ziara yake mjini Sharja Dk. Shein alipata fursa ya kutembelea eneo la shughuli za uvuvi la ‘East Fishing Processing LLC”, lililoko Al Jurf  katika eneo la Ajman  na kupata maelezo juu ya namna ya eneo hilo lenye kiwanda kikubwa cha kisasa cha samaki jinsi kinavyosarifu  na kuhifadhi samaki pamoja na kuwaweka katika mfumo maalum wa kwa ajili ya kuuzwa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo inayolishirikisha kundi la Kampuni ya THOMSUN, K.V. Thomas alimueleza Rais Dk. Shein namna na kiwanda hicho kinavyosarifu samaki wa aina mbali mnali wakiwemo kamba kutoka nchi mbali mbali ikiwemo Tanzania.

Dk. Shein kwa upande wake alipendezewa na namna kiwandaa hicho kinavyofanya kazi na kutokana na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sekta ya uvuvi na viwanda vya samaki pamoja na azma ya kuanzisha Kampuni ya Uvuvi,

Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja ili Zanzibar ipate kupanua wigo katika sekta hiyo.

Kutokana na kiwanda hicho kutumia teknolojia ya kisasa katika kusarifu samaki wa aina mbali mbali pia, soko la ajira limeonekana kuchukua fursa yake kutokana na kuajiri vijana wengine hatua ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika kupambana na changamoto iliyopo katika suala zima la ajira.

Wakati huo huo, Dk. Shein na ujumbe wake akiwemo Mama Mwanamwema Shein walitembelea katika  shamba la ngombe wa maziwa la Al Rawabi, ambapo pia eneo hilo lina viwanda vya vinywaji vya matunda pamoja na bidhaa nyengine zinazotokana na maziwa.

Akiwa katika eneo hilo la Al Rawabi, Dk. Shein alipata maelezo kutoka kwa uongozi wake ambapo Mkuu wa Kampuni inayosimamia Shamba hilo Abdalla Eleweis alimkaribisha Dk. Shein na ujumbe wake na kumueleza namna eneo hilo linavyofanya shughuli zake za ufugaji wa ngombe pamoja na uendelezaji wa viwanda vya matunda.

Nae Meneja Mkuu wa Shamba hilo Dk. Ahmed Eltigani Al Mansour alimueleza Rais Dk. Shein na ujumbe wake jinsi ya shamba hilo linavyofuga ngombe kwa kutumia teknolojia ya kisasa ikiwemo kuwawekea viyoyozi na mafeni maalum kutokana na mazingira ya hali ya hewa ya ukanda huo.

Kwa mujibu wa maelezo ya Dk. Ahmed shamba hilo lina ngombe 12,500 ambapo kwa kila ngombe mmoja kwa siku hutoa lita 60 za maziwa na kutoa lita 250,000 kwa siku huku akitumia fursa hiyo kueleza siri ya mafanikio hayo ikiwa ni pamoja na utafiti mkubwa walioufanya kabla ya kuazisha ufugaji huo.

Dk. Ahmeda alieleza kuwa ufugaji wanaoufanya ni ufugaji bora duniani na pia ni eneo lililopata mafanikio makubwa ikifananishwa na ufugaji unaofanyika katika maeneo mbali mbali zikiwemo nchi za Afrika na hata nchi zilizoendelea ikiwa ni pamoja na kutoa ajira kwa wingi.

Akimaliza ziara yake katika eneo hilo, Rais Dk. Shein aliuhakikishia uongozi wa Al Rawabi kuwa Zanzibar itakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mashirikiano yanakuwepo katika sekta hiyo ya ufugaji ikiwa ni pamoja na kupanua wigo na kujifunza jinsi ya mafanikio hayo yalivyopatikana.