Siku hazigandi. Nathubutu kusema hivyo kwani Desemba 13, 2013 ndiyo siku ambayo nguli Ramadhan Mtoro Ongala ‘Dk, Remmy’ alitimiza miaka mitatu tangu aiage dunia. Dk. Remmy alifariki usiku wa kuamkia Jumatatu, Desemba 13, 2010 nyumbani kwake Sinza jijini Dar es Salaam, baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi ya kisukari. Akawaacha wapenzi wake wa muziki wa dansi na Injili pia wananchi kwa ujumla katika dimbwi la majonzi yasiyosahaulika kutokana na tungo za nyimbo zake, ambazo hadi leo zinarindima katika vituo vingi vya redio hapa nchini na hata nje ya mipaka yetu.
Dk. Remmy alikuwa wa kwanza kupata ujasiri wa kukemea ngono zembe, akatunga wimbo wa Mambo kwa soksi, lakini jamii ikambeza kwamba wimbo huo haukuwa na maadili mema. Baadaye viongozi wa Serikali na dini na watu kwa jumla walielewa nini alichokuwa akisema Dk. Remmy. Wakaanza kuhubiri majukwaani hadhari hiyo.
Wakati wa uhai wake, Dk. Remmy alijipatia umaarufu katika jiji la Dar es Salaam, hususani maeneo ya Sinza. Alikuwa na gari lake dogo soloon lililokuwa la aina yake ambako kokote lilikopita watu walilishangaa. Nyuma ya gari hilo kulikuwa na maneno, ‘Baba yako analo’?
Historia ya maisha ya Dk. Remmy inaeleza kwamba mara Dk. Remmy Ongala alipozaliwa, wazazi wake walimuita Ramazani Mtoro Ongala. Alizaliwa mwaka 1947 katika Mkoa wa Kivu, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Familia yake iliishi katika eneo lililoitwa Kindu, si mbali kutoka mpakani na Tanzania. Baba yake alikuwa mwanamuziki mashuhuri na mpiga ngoma kwa kutumia mikono na mbira. Baada ya kuzaliwa haikuchukua muda mrefu familia yake ilihamia katika mji wa Kisangani huko huko DRC.
Ipo habari kwamba kabla ya kuzaliwa, mama yake alipata ujauzito mara mbili, lakini kwa bahati mbaya kila alipojifungua, watoto walifariki. Alipopata ujauzito mara ya tatu alienda kwa mganga wa kienyeji kumuomba ushauri afanye nini ili mtoto atakayezaliwa asiage dunia.
Bila kusita, mganga wa kienyeji akampa ushauri. Akamwambia kwanza safari hii asiende kujifungulia hospitali, bali akajifungulie porini. Pia alipewa ushauri kwamba mtoto akishazaliwa asije akamkata nywele zake. Yote hayo yalitendeka na ndiyo kisa cha Dk. Remmy kutokata nywele hadi alipozidiwa na maradhi yaliyomfanya aokoke, na ndipo aliponyoa nywele zake akiwa nchini Tanzania.
Mwenyewe aliwahi kusema kwamba mwanzoni alikuwa anajisikia aibu sana kuwa na nywele ndefu namna ile, hadi baadaye jina na taswira ya mfalme wa reggae ulimwenguni, Bob Marley ilipopata umaarufu nchini DRC, ndipo alipoipenda staili ile ya nywele kwani hata watu wengine pia walianza kuikubali na kuionea fahari.
Pia inasemekana Remmy alizaliwa akiwa tayari na meno mawili ya mbele, kitu ambacho kwa imani ya kabila lao, kilichukuliwa kama ishara ya baadaye kuja kuwa mganga wa kienyeji. Ingawa utabiri huo haukutimia, inasemekana huo ndiyo ukawa mwanzo wa yeye kujulikana hapo baadaye kama Dokta Remmy Ongala.
Baba yake ndiye aliyeanza kumfunza masuala ya muziki tangu akiwa mdogo kabisa. Jambo hilo lilimfanya aamini kabisa kwamba kama jinsi ambavyo watu wengine wamezaliwa kuwa madaktari, wanasheria, waalimu, wakulima n.k, yeye alizaliwa ili awe mwanamuziki.
Kwa bahati mbaya baba yake huyo alifariki dunia na kumuacha Dk. Remmy akiwa na umri wa miaka sita, akiwa tayari ameshaanza shule. Lakini kutokana na ukosefu wa fedha na kwa sababu mama yake hakuweza kuendelea kumlipia karo, ilibidi aache shule.
Kwenye miaka ya1960, Remmy alikuwa ameshajifunza mwenyewe kupiga gitaa. Mwaka 1964 ulikuwa si mwaka mzuri kwake kwani mama yake mzazi alifariki dunia; jambo ambalo lilimuacha Dk. Remmy na mzigo wa kuwalea wadogo zake.
Bila elimu na ujuzi mwingine wowote, alilazimika kuanza kujitafutia riziki kupitia muziki. Ujuzi wake wa kupiga gitaa uliongezeka kwa kasi ya ajabu, kitu ambacho kilimwezesha kutumbuiza kwa kupiga ngoma na gitaa katika hoteli nyingi na sehemu mbalimbali nchini DRC akiwa na bendi yake iliyokuwa imesheheni vijana wenzake iliyoitwa Bantu Success.
Kwa miongo kadhaa iliyofuata, Dk. Remmy alizunguka sehemu mbalimbali za Congo akiambatana na bendi kadhaa maarufu za wakati huo nchini humo, zikiwamo Success Muachana na ile ya Grand Mickey Jazz nchini Uganda.
Japokuwa Dk. Remmy alijifunza mwenyewe kupiga gitaa, lakini aliwahi kukiri kwamba muziki wa kutoka Cuba ambao wakati huo ulikuwa unaanza kujipatia umaarufu barani Afrika, ulimsaidia kupata staili za pekee katika upigaji gitaa. Kwa upande wa uimbaji anasema uimbaji wa Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ na ule wa Franco ulimsaidia kupata staili yake ya uimbaji kama tulivyoizoea kusikia enzi za uhai wake.
Maisha yake nchini Tanzania
Mwaka 1978 Dk. Remmy aliingia jijini Dar es Salaam baada ya kuitwa na mjomba wake, Kitenzogu Makassy, ili ajiunge katika bendi maarufu ya wakati huo ya Orchestra Makassy iliyokuwa chini ya uongozi wa mjomba wake huyo.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa maisha ya Dk. Remmy nchini Tanzania. Akiwa na bendi ya Orchestra Makassy, alitunga wimbo wake wa kwanza uliojulikana kama Siku ya Kufa, wimbo ambao aliuandika kumkumbuka rafiki yake aliyefariki dunia.
Wimbo huo ulianza kumpatia umaarufu mkubwa na kujulikana kwa haraka ndani na nje ya nchi. Mzee Makassy aliamua kuihamishia bendi yake nchini Kenya, kitendo kilichomfanya Dk. Remmy ajiunge na bendi ya Matimila baada ya kudumu katika bendi ya Orchestra Makassy kwa takriban miaka mitatu hivi.
Jina la bendi hiyo ya Matimila lilitokana na jina la kijiji kimoja kilichoko kusini mwa Tanzania. Kujiunga kwa Dk. Remmy katika bendi ya Matimila, kulimwongeazea umaarufu katika anga za muziki nchini Tanzania wakati huo. Chini ya uongozi wake, Dk. Remmy aliisuka upya bendi hiyo na kuibadilisha jina ikaitwa Orchestra Super Matimila.
Miaka iliyofuata Watanzania walishuhudia umaarufu wa Dk. Remmy ukiongezeka kutokana na mashairi ya nyimbo zake, ambayo yaliegemea katika kuzungumzia mambo halisi ya kijamii kama vile umasikini, afya, siasa, majanga ya Ukimwi nk.
Mafanikio ya Dk. Remmy na kundi lake zima la Super Matimila hayakuishia nchini Tanzania, kwani katika miaka ya mwishoni mwa 1980 walianza kujipatia umaarufu nje ya Tanzania na Afrika.
Dk. Remmy aliwahi kusema kwamba kupata mialiko ya nje lilikuja kama mchezo tu. Alimpa kaseti yenye nyimbo zao rafiki yake mmoja Mzungu aliyekuwa akiondoka nchini Tanzania kurejea kwao Uingereza.
Rafiki yake huyo alipofika huko aliwapatia jamaa wa World of Music, Arts and Dance (WOMAD) ambalo ni shirika linalopandisha chati wanamuziki na wasanii mbalimbali kutoka katika nchi za Dunia ya Tatu. Walivutiwa na nyimbo zao na hivyo kuwapa Super Matimila mwaliko kushiriki katika maonesho yao barani Ulaya mwaka 1988.
Baada ya kureja nchini, bendi ya Super Matimila ilitoa albamu yenye jina la Nalilia Mwana ikiwa na mkusanyiko wa nyimbo zao zilikuwemo nyimbo zilizopendwa sana kama vile Ndumila Kuwili na Mnyonge Hana Haki.
Mwaka 1989 Dk. Remmy na Super Matimila walirudi Ulaya kutokana na mwaliko mwingine wa WOMAD. Ni wakati huo huo walipopata fursa ya kurekodi kwenye studio ya kisasa zaidi ambayo ilikuwa inamilikiwa na mwanamuziki maarufu aitwaye Peter Gabriel. Studio hiyo ilikuwa inaitwa Real World Studios.
Dk. Remmy aliwahi kufafanua kuwa wimbo maarufu ya Kipenda Roho, aliuimba mahsusi kwa ajili ya mkewe, ambaye ni Mzungu Mwingereza, ambaye wakati huo tayari walikuwa wameshazaa watoto watatu.
Mwaka 1990, Remmy na bendi yake ya Super Matimila walirejea tena katika studio za Real World ambako walirekodi albamu nyingine yenye nembo ya ‘Mambo’ ambayo ilikuwa na wimbo kama huo wa Mambo ambao aliuimba kwa lugha ya Kiingereza na kuweza kukidhi kiu ya wapenzi wake wasiojua Kiswahili. Nyingine ni pamoja na No Money, No Life na One World.
Umaarufu wake ulizidi kung’ara mwaka 1990 alipotoa wimbo wa Mambo kwa Soksi ingawa baadhi ya watu waliupinga kwa kusema kwamba haukuwa na maadili ingawa kimsingi alikuwa anawaasa watu, hususani vijana kutumia kondomu ili kuepukana na maambukizi ya Ukimwi.
Akiwa Super Matimila, Dk. Remmy alitoka na nyimbo nyingi zikiwamo za Bibi wa Mwenzio, Kipenda Roho, Asili ya Muziki na Ngalula. Nyingine ni Mwanza, Mama Nalia, Harusi, Hamisa, Mnyonge Hana Haki, Ndumila Kuwili na Mtaka Yote, ambazo zilimuongezea sifa kubwa kutokana na maudhui yaliyokuwa yakiigusa jamii.
Baadaye Dk. Remmy alianza kusumbuliwa na maradhi ya kisukari yaliyomfanya aachane na muziki wa dansi kwa madai ya kwamba umejaa mambo mengi ya kishetani. Baada ya kuokoka, akatubu dhambi zake na akaanza kumuimbia Bwana.
Kabla ya kifo, Dk. Remmy alitoa albamu yake ya injili aliyoiita Kwa Yesu Kuna Furaha. Dk. Remmy alikuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha albamu yake ya pili, lakini Mungu akampenda zaidi usiku wa kuamkia Jumatatu, Desemba 13, 2010 nyumbani Sinza.
Eneo hilo alilokuwa akiishi lilipewa jina la Sinza kwa Remmy kutokana na umaarufu wake.
Mungu aiweke roho yake Mahali Pema Peponi, Amina.
Mwandishi wa makala haya anapatika kwa simu:
0784331200, 0713331200 na 0767331200.
Barua pepe: [email protected]