Na Lookman Miraji
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt: Damas Ndumbaro amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza Maalumu la Mawaziri wa Sheria la umoja wa Afrika katika kikao kilichowakutanisha mawaziri, mabalozi na wataalamu katika sekta ya sheria ya umoja wa Afrika.
Akizungumza wakati akihitimisha kikao kilichodumu kwa muda wa siku tisa, Waziri Ndumbaro amewashukuru wajumbe wa baraza hilo kwa kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa baraza la uongozi la mawaziri wa sekta ya sheria kwa nchi za umoja wa Afrika.
“Tumeikubali heshima mliyotupatia nchi ya Tanzania kuwa Mwenyekiti wa baraza la uongozi.Tutafanya kazi kwa pamoja katika kuhakikisha Umoja wa Afrika unakuwa ni sehemu nzuri katika sekta ya Sheria na mfano bora katika utoaji Haki kwa miaka inayokuja.” Alisema Ndumbaro.
Aidha waziri Ndumbaro ameongeza kwa kusema kuwa, Kamati za ufundi za Wataalamu katika masuala ya Haki na Sheria ni Kamati muhimu katika Umoja wa Afrika ikiwemo kupitia nyaraka ambazo zinatokea katika Kamati za Wataalamu nyingine ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu kwa wakati na usimamizi wa Haki na kuwa makini katika kufanya maamuzi kwa kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia maamuzi yenye tija.
Waziri Ndumbaro pia amewataka Viongozi waliochaguliwa wakiwemo Makamu Wenyeviti watatu waliochaguliwa na Katibu wa Kamati hiyo kuhakikisha kuwa wanaanza utekelezaji wa maazimio waliyokubaliana kwa kuunda timu itakayowawezesha kufikisha ajenda kwa vyombo vya maamuzi ili kuweza kutekeleza matakwa ya Umoja wa Afrika.
Hatua hiyo ya kuchaguliwa kwa Dkt: Ndumbaro inatajwa kama miongoni mwa hatua muhimu katika nyanja ya uongozi na faraja kwa taifa kwa kutoa kiongozi atakayekwenda kusimamia katiba sheria katika ngazi za juu zaidi barani Afrika.
Mkutano huo imehitimishwa leo hii mara baada ya kudumu kwa siku tisa tangu Disemba 14 na kufikia tamati leo hii Disemba 22 katika hoteli ya kimataifa ya Golden Tulip iliyoko visiwani Zanzibar.