RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametoa msamaha kwa wanafunzi 33 wanaotumikia adhabu za makosa yoyote katika Chuo cha Mafunzo katika Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Januari 11, mwaka huu na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Charles Hilary, katika kuadhimisha Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Mwinyi kwa kutumia kifungu cha 59 cha Katiba ya Zanzibar 1984, inampa uwezo wa kutoa msamaha kwa mtu aliyehukumiwa kwa kosa lolote.

Hivyo kupitia kifungu hicho, Rais Dk Mwinyi katika kusherehekea Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar ametoa msamaha kwa kuwaachia huru wanafunzi 33 wanaotumikia adhabu zao mbalimbali katika Chuo cha Mafunzo Zanzibar.

Alisema kati ya wanafunzi hao 33 waliopewa msamaha 25 ni kutoka Unguja na wanane ni kutoka Pemba.