Wiki iliyopita, Rais John Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri. Mabadiliko aliyofanya ni kumwondoa kwenye Baraza la Mawaziri, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na kumteua Dk. Harrison Mwakyembe kuziba pengo hilo. Dk. Mwakyembe amehamishwa kutoka Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba. Nafasi yake imechukuliwa na Prof. Palamagamba Kabudi.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inampa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano kufanya mabadiliko katika Baraza bila kutoa sababu, na alifanya hivyo katika uteuzi wa zamu hii. Mwaka jana wakati anatengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, alisema katika tamko la kumwondoa kuwa alitengua uteuzi huo kwa sababu waziri alikuwa “mlevi”.

Angalau hiyo ilikata kiu ya wananchi, wapigakura wa Mhe. Rais, wakajua kuwa Kitwanga alikiuka misingi na maadili ya utumishi  wa umma. 

Kwa Nape hakutoa sababu na hawajibiki kutoa sababu. Nape ametenguliwa siku moja tu, baada ya Kamati ya Kuchunguzi tukio la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, …, kuvamia Kituo cha Matangazo cha Clouds (CMG).

Sitanii, naomba wanahabari wenzangu wanielewe hapa kuwa siandiki habari za … kinyume na tulivyokubaliana, bali nimefanya rejea ya jina lake kukamilisha ujenzi wa hoja yangu. Kwamba Kamati iliyochunguza tukio la uvamizi, mimi nilikuwa Katibu wake. Niliwasilisha na matokeo ya uchunguzi, ambayo yalitangazwa na vyombo mbalimbali nchi nzima.

Nikiri sijapata taarifa yoyote – iwe kwa njia rasmi au zisizo rasmi –  kuelezwa kuwa taarifa niliyoisoma ndiyo iliyomkera Rais Magufuli ‘akamtumbua’ Nape. Kuna ukimya mkubwa, ila mwenye macho haambiwi tazama. Nawaza kwa sauti kuwa taarifa ile itakuwa na mchango katika Nape kutumbuliwa.

Sitanii, wanahabari wameonesha mshikamano katika hili. Ingawa uteuzi uko nje ya mamlaka yao, wamethibitisha kumuunga mkono Nape. Hata askari kanzu aliyemnyooshea bastola Nape, naamini huko aliko anaifahamu nguvu ya vyombo vya habari. Radio, magazeti, televisheni, mitandao ya kijamii na kila awaye amesambaza ujumbe wa kutosha, kuonesha kuwa nchi yetu wananchi hawataki kuona bunduki hadharani.

Rais Magufuli amefanya vyema. Amevisihi vyombo vya habari kujenga uzalendo. Hapana shaka zile picha za bunduki zilivyopamba kurasa za kwanza za magazeti kwa kiwango cha kufunika hata ziara yake bandarini, ilimpa ujumbe maalumu – jinsi wanahabari walivyoumia, na jinsi Taifa letu linavyoingizwa katika enzi za vitisho vya bunduki na risasi, suala alilopoteza uwaziri Nape akilipinga.

Nape amefanya kazi ya kutetea uhuru wa habari, kwa kukataa kiongozi kuingiza askari kwenye chumba cha habari na kulazimisha aina ya habari anayotaka itangazwe. Nasema, Nape ameondoka kishujaa. Hata mrithi wake, Dk. Mwakyembe, anapaswa kulisimamia hili. Sitarajii kama Dk. Mwakyembe atahamasisha askari kuingia vyumba vya habari na bunduki kulazimisha nini kitangazwe. Nchi yetu haijafika huko.

Sitanii, nimemfahamu Dk. Mwakyembe zaidi ya miaka 20 sasa. Awali alikuwa rafiki mkubwa wa vyombo vya habari. Ingawa hajawahi kutangaza kuwa yeye ni adui wa vyombo vya habari, michango yake katika michakato ya kutunga sheria kama ya Haki ya Kupata Habari (ATI) 2015 na Huduma za Vyombo vya Habari (MSA) 2016, zinatutia hofu.

Mimi nikiwa Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) nasema ikiwa Dk. Mwakyembe hatabadilika, akaendelea na msimamo aliokuwa nao wakati wa kutunga sheria hizo mbili na mara kadhaa alipochangia bungeni, tujiandae kusikia magazeti, redio na televisheni vikifungiwa. Fungueni masikio kwa nguvu na tufungue macho kushuhudia “kifo cha vyombo vya habari nchini”.

Hata hivyo, Dk. Mwakyembe anayo nafasi. Hofu hii tuliyonayo na tunayoisema kwa uwazi bila kificho, anaweza kujitofautisha nayo kwa kuthibitisha kuwa yeye ni mlezi wa vyombo vya habari sahihi. 

Ni matarajio yangu kuwa Dk. Mwakyembe atapata faraja kubwa kuwezesha wanahabari wengi kupata taaluma ya habari na vyombo vya ndani kuwa na nguvu ya kiuchumi kuliko kuhesabu idadi ya redio, televisheni au magazeti aliyofungia. Mungu ibariki Tanzania.