Wiki iliyopita nilikuwa bungeni hapa mjini Dodoma. Niliingia katika ukumbi wa Bunge, nilisikiliza michango ya wabunge kadhaa. Nilimsikiliza Waziri wa Habari, Vijana, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, na wengine wengi. Niseme mapema tu kuwa hapa leo najadili hoja ya Bunge kurusha matangazo yake moja kwa moja (live).
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeongoza jopo la wanahabari kwenda Dodoma kujadiliana na uongozi wa Bunge na Serikali, juu ya utaratibu unaoweza kutumika kuendelea kurusha matangazo ya Bunge moja kwa moja kwa njia ya televisheni. Tangu Aprili 19, mwaka huu, Bunge limesitisha matangazo ya moja kwa moja.
Nimemsikiliza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, ambaye kwa sababu anazozifahamu yeye, ameamua kulipa Bunge tafsiri potofu ya Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Masaju kwa sababu anazozifahamu amechagua kutumia Ibara ya 18(d) ya Katiba inayosema;
“Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala mbalimbali ya jamii.” Masaju kwa kutumia ibara hii ndogo, akahalalisha kuwa Bunge sasa linafanya kazi ya kuwapa taarifa wananchi katika matukio muhimu na taarifa si habari.
Sitanii, kuendelea na wanasheria wa aina hii wanaotafsiri Katiba kutimiza matakwa yao, nchi inaweza kupelekwa kusiko. Siamini kama Masaju alipata fursa ya kusoma Ibara ya 18(d), kwamba alishindwa kusoma Ibara ya 18(b) inayosema: “Kila mtu anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila kujali mipaka ya nchi.”
Kwa kuwa Ibara ya 18(b) inapingana na matakwa ya Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliendelea kuliaminisha Bunge na umma kuwa kwa Tanzania habari zinatolewa kama hisani ya wakubwa. Masaju amesahau pia kuwa Ibara ya 8(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema:
“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii na kwa hiyo:- (a) wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii.”
Ibara hii pekee ingetosha kumtia hofu Mwanasheria Mkuu wa Serikali asitoe kauli kama hiyo. Wananchi wanaiheshimu Katiba na wanataka ibara ya 18(b) ifanye kazi na kwa nguvu wanayopata kutokana na ibara ya 8(a), wanataka Bunge lirushwe ‘live’.
Sitanii, nguvu ninayoishuhudia ikitumiwa na Serikali, Bunge na wapambe wao kupinga matangazo ya Bunge kurushwa ‘live’, ikiwamo kuvunja ibara za Katiba ya Tanzania nilizozitaja bila kujali, inanitia hofu. Sitawazungumzia wabunge waliotamani kulia bungeni eti wanatetea Bunge lisirushwe ‘live’.
Ukiwasikiliza wenye kutetea Bunge lisirushwe ‘live’, hoja yao ni dhaifu. Walianza na hoja ya fedha, ikakosa mashiko, hawaitumii tena kwa sasa. Wamekuja na hoja ya kwamba Bunge ndilo lililopitisha mpango wa kujenga kituo chake cha kurusha matangazo. Shida ninayopata hapa, viongozi wetu karibu wote wanafuta haki ya kupata habari kwa njia ya matamko wakati waliapa mchana kweupe kuilinda, kuitetea na kuihifadhi Katiba ya Tanzania.
Wakati nikiendelea kuangalia hicho kizungumkuti, nimemshuhudia Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, akijiaibisha na kuzomewa bungeni. Kichwa cha makala hii kinasema Dk. Mwakyembe anaiaibisha PhD. Kwa muda mrefu, Dk. Mwakyembe amejenga tabia ya kuudanganya umma akijaribu kueleza kuwa yeye ni mwandishi nguli hapa nchini.
Kiuhalisia, Dk. Mwakyembe hakuwahi kufikia hata ngazi ya uandamizi kwenye uandishi wa habari. Alijiunga na Gazeti la Uhuru baada ya kuhitimu kidato cha sita mwaka 1974. Hapa alikutana na waandishi tarajali wengine kama Dk. Palamagamba Kabudi, Dk. Agrey Mulimka na Dk. Sengondo Mvungi.
Alifanya kazi ya kutumwa habari za mahakamani (court reporter) hadi mwaka 1977 alipokwenda kusoma diploma ya uandishi wa habari. Baada ya hapo aliripoti kidogo habari za vita ya Kagera, kisha akajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusoma sheria. Baada ya kusoma sheria hakupata kurudi chumba cha habari kufanya kazi ya uandishi angalau kufikia ngazi ya kuwa mwandishi mwandamizi (chief reporter).
Sitanii, kwa kutopata fursa ya kuwa mhariri akajua maana ya uhariri, kwamba ameishia kuwa ripota wa kawaida katika maisha ya uandishi wake, amekosa fursa ya kuufahamu uandishi. Ikumbukwe wakati huo anafanya uandishi, karibu kila habari aliyoiandika ilipaswa kuhaririwa na Mzee Paul Sozigwa na wenzake, aliyekuwa anafanya kazi ya ‘kuchuja habari’ kwa niaba ya Serikali.
Dk. Mwakyembe alirejea ibara ya 19 ya Tamko la Haki za Binadamu la mwaka 1948 linalotoa haki ya kutafuta, kuchakata na kusambaza habari, lakini pia tamko hilo linaweka wajibu muhimu kwa wasambazaji taarifa. Ndipo hapo ninaposema; Mwakyembe kama ndiye anayeishauri Serikali, basi anaipotosha kwa kiwango cha kutisha. Ajitokeze hadharani na kujibu iwapo alipata kufikia ngazi ya uhariri kufahamu huo wajibu.
Tatizo la watu wa aina yake ambao ni ‘half cooked’ kwenye taaluma kadhaa, huishia kuwa wanasheria makanjanja (bush lawyers), na hawa hutaka kuiaminisha jamii kuwa wao ni nguli katika kila eneo. Matokeo yake ndiyo yaliyomkuta Mwakyembe. Yapo maeneo huwa sikubaliani na Juma Nkamia, lakini wakati anachangia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Sanaa na Michezo hakuna aliyemzomea. Alijenga hoja akaeleweka, ila Mwakyembe akaambulia kuzomewa.
Sitanii, inapaswa kufahamika kuwa uandishi wa habari ni taaluma isiyoweza kufanywa na kila mtu eti tu kwa sababu anajua kusoma na kuandika. Unaweza kuwa mtaalamu wa mawasiliano au profesa mzuri wa lugha, ila kama hukuusomea na kufahamu vyema uandishi unaishia kuwa msanifu wa kurasa (proofreader).
Wajibu unaotamkwa na hilo tamko la haki za binadamu, upo kisheria mikononi mwa wahariri. Sasa najitolea shule ya bure kwa Dk. Mwakyembe anayeiaibisha shahada ya uzamivu kwa kusema mambo asiyoyafahamu. Kazi za mhariri ni nne; kuchapisha kitu kilivyo (relaying), kupunguza (limiting), kuongeza (expanding) na kutafsiri (interpreting).
Mhariri anapokuwa anafanya kazi kwa kutekeleza majukumu hayo manne, kitaaluma hawezi kuruhusu matusi, kauli za uchochezi, maneno yanayohatarisha usalama wa Taifa, hujuma kwa uchumi wa nchi, athari za kiafya na mengine mengi yanayohatarisha jamii. Mwakyembe kwa kutojua, haelewi kwa nini katika matangazo ya moja kwa moja tunaruhusu delay.
Bunge linaweza kuwa na delay ya dakika 15 ikiwa mbunge anachagia kwa dakika 15 au 10 kwa maana ya kwamba mhariri aliyepo kwenye mtambo wa kurushia matangazo anapaswa kutekeleza majukumu manne niliyoyataja hapo juu.
Sitanii, kusitisha matangazo ya moja kwa moja kwa hofu kuwa wabunge watatukana au watatoa matamshi yasiyoendana na lugha za kibunge, pia ni kukiri kuwa kiti cha Spika wa Bunge kimeyumba. Kimeshindwa kuwadhibiti wanaozungumza matusi bungeni. Wapo wanaosema TV ndiyo iliyoongeza upinzani nchini, hili linahitaji mjadala mpana.
Tumezungumza na Ofisi ya Bunge, na mimi naliona suluhisho. Bunge linasema mabunge ya Jumuiya ya Madola yanazo kanuni za utangazaji. Binafsi nasema kanuni hizo za utangazaji tunapaswa kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari, wabunge na jamii kwa ujumla ikazijua hizo kanuni. Kama mbunge anatukana, afahamu mapema kuwa akitoa lugha isiyo ya kibunge, matusi hayo hayatakwenda hewani.
Bila kutumia njia ya mafunzo itakayosaidia kuweka uelewa unaofanana kwa wananchi, wabunge na waandishi wa habari kisha tukakubaliana sawa na ilivyo katika mchezo wa mpira wa miguu kwamba sheria 17 za FIFA zinatekelezwa na wote – wachezaji, refa na mashabiki – ubabe hautatufikisha popote. Leo tunaanza kuzuia matangazo ya ‘live’, kesho tutazuia kufunga ndoa!
Haki hizi zinazotolewa kikatiba inatupasa kujizuia kuziondoa kirahisi maana tunaweza kukuta tunafifisha demokrasia nchini. Wananchi wanataka matangazo ya ‘live’, na Dk. Mwakyembe aache kudanganya umma kwa kuuaminisha kuwa yeye ni mwandishi nguli wakati hakupata hata fursa ya kuwa mwandishi mwandamizi katika maisha yake.
Wananchi wanataka matangazo ‘live’, na haki hii tutaendelea kuidai leo, kesho, alfa na omega bila kuchoka kwani ni haki ya kikatiba. Mungu ibariki Tanzania.