Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia,Pwani
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa utakaofanyika Aprili 2, 2025 viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 26,2025 kuhusu uzinduzi huo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete anaeleza, Makamu wa Rais atakabidhiwa vijana sita watakaokimbiza Mwenge kitaifa ambao wameandaliwa kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

“Vijana hao watakuwa na jukumu la kuukimbiza Mwenge wa Uhuru katika mikoa yenye jumla ya Halmashauri 195 za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa siku 195” alifafanua Ridhiwani.
Ridhiwani alieleza, kwa kipindi hicho chote Mwenge wa Uhuru utafanya kazi ya kuhamasisha amani, umoja, upendo na mshikamano wa Kitaifa.
Vilevile Mwenge wa Uhuru utawahimiza wananchi kushiriki shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo yao ya Halmashauri.
Kwa mujibu wa Ridhiwani, kauli mbiu ya Mwaka huu imebeba Ujumbe JITOKEZE KUSHIRIKI UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2025 KWA AMANI NA UTULIVU.

“Watanzania wenzangu tunatambua kuwa falsafa hii ya Mwenge wa Uhuru ndio chimbuko la Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 , Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964 na Azimio la Arusha la mwaka 1967.
Ridhiwani alisisitiza, Watanzania waendelee Mwenge wa Uhuru kama ulivyoasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961 wakati Taifa lilipopata Uhuru.
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakar Kunenge alieleza, wapo kwenye hatua ya mwisho ya maandalizi hadi kufikia machi 29, mwaka huu watakuwa wamekamilisha.

