Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango anatarajiwa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Utatu wa Asasi mbili za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika Lusaka, Zambia tarehe 23 Machi 2024.
Makamu wa Rais ataondoka nchini Machi 22, 2024 kushiriki Mkutano huo ambao agenda kubwa ni hali ya ulinzi na usalama katika nchi za SADC, hususan katika Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji na Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mkutano huo utatanguliwa na mikutano ya maandalizi ya ngazi za Wataalam ambayo ilianza tarehe 17 Machi 2024 na itakamilishwa na Mikutano ya Makatibu Wakuu na Mawaziri itakayofanyika tarehe 22 Machi 2024.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (Mb) ataungana na Mawaziri wenzake kutoka nchi wanachama katika Mkutano huo muhimu.
Tanzania kama mwanachama wa SADC na ikiwa ni miongoni mwa nchi zinazochangia vikosi vya kulinda amani katika nchi za Msumbiji na DRC inashiriki kikamilifu katika ngazi zote za Mkutano huo.