Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Isdor Mpango, amefungua matawi mawili mapya ya Benki ya NMB Chanika na Kinyerezi, yanayofanya mtandao wa matawi ya benki hiyo nchini kufikia 241, huku akiipongeza benki hiyo kwa kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa Ajenda ya Serikali ya Tanzania ya kuzipeleka Huduma Jumuishi za Kifedha karibu na wananchi.

Uzinduzi wa matawi hayo umefanyika Ijumaa Machi 28, ukienda sambamba na makabidhiano ya vifaatiba vyenye thamani ya Sh. Mil. 10 kupitia Programu ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI – zamani CSR), ambako Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna ilimkabidhi Dk. Mpango vifaa hivyo kwa ajili ya Vituo vya Afya Chanika na Kinyerezi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dk. Mpango alisema Matawi ya NMB Chanika na Kinyerezi, yatachachoea shughuli za kiuchumi na maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, na kwamba anaamini ongezeko la Mtandao wa Matawi ya NMB litaendelea kuchagiza ukuaji wa Gawio la Serikali, ambako katika kipindi cha miaka 15 imetoa gawio la Sh. Bil. 289.4.

“Tunapozindua matawi haya na kutanua mtandao wa matawi yenu kiasi cha kuwafanya kuendelea kuwa Benki Kiongozi, napenda niwapongeze kwa nidhamu yenu ya ulipaji kodi, na mchango thabiti katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupita ulipaji kodi,” alisema Dk. Mpango na kuongeza:

“Natambua kuwa nidhamu hii imeitambulisha Benki ya NMB kupitia Tuzo za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kama Taasisi Namba Moja Nchini inayozingatia Misingi na Kanuni Bora za Ulipaji Kodi na Mlipa Kodi Mkubwa Zaidi nchini. Hongereni sana NMB.”

Alibainisha ya kwamba mchango wa NMB katika uchumi wa Taifa ni mkubwa sana, ambako imechangia sehemu kubwa sana katika Mapato ya Kodi ya Serikali na hata yale ya Tawala za Mikoa, ambako takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024, kodi zote walizolipa Serikalini ni jumla ya Sh. Bil. 596 na kuwapa Tuzo za TRA.

“Nitumie nafasi hii pia kuishukuru NMB kwa Ongezeko la Tija kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambako gawio mnalolitoa kwa Serikali ni kubwa na limekuwa likiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mwaka jana mmetoa Sh. Bil. 57.39, ikilinganishwa na lile la Sh. Bil. 4.7 ililotoa kwa Serikali mwaka 2009.

“Hii inafanya jumla ya Gawio la NMB kwa Serikali katika kipindi cha miaka 15 kuwa ni Sh. Bil. 289.4, Hongereni sana na tunatarajia gawio kubwa zaidi kwa mwaka huu, maana tayari tumeona faida baada ya kodi kwa mwaka 2024 kuwa ni nzuri sana,” alisisitiza Dk Mpango katika hafla hiyo.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alimshukuru Dk. Mpango kwa kukubali kuwa mgeni rasmi wa uzinduzi huo na kwamba ushiriki wake unaakisi ushirikiano wa dhati uliopo baina ya Serikali na Taasisi za Fedha katika dhamira ya kuiendeleza Ajenda ya Taifa ya Ujumuishaji Kifedha kwa kuzisogeza huduma za kibenki karibu zaidi na wananchi.

“Ripoti ya Finscope ya mwaka 2023, ilionesha kwamba ni asilimia 22 tu ya Watanzani ndio wanaotumia huduma za kibenki, yaani bado kuna asilimia ndogo ya Watanzania wanaotumia huduma hizi, hivyo kupitia matawi haya wakazi wa Chanika, Msongola na maeneo yote ya jirani, watapata fursa ya kuingia kwenye mfumo huo kwa maslahi mapana ya maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu.

“Huduma za Kibenki  ni kichocheo kikubwa kwa maendeleo ya kiuchumi katika sehemu yeyote, kwa wingi wa shughuli za kiuchumi hapa Kinyerezi na Chanika, hasa shughuli za kibiashara na uzalishaji, NMB imeona ni vyema kusogeza huduma kwa manufaa ya wakazi wake na uimara wa uchumi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.

“Matawi haya ambayo leo hii umeyazindua, yanafikisha idadi ya matawi 34 ya NMB kwa Mkoa wa Dar es Salaam na 241 nchi nzima, kutoka Matawi 97 tu tuliyoanza nayo mwaka 1997, katika kipindi ambacho, matawi ndiyo yalikuwa njia pekee ya kuwahudumia wateja tofauti na sasa ambapo huduma zetu zinapatikana kwa ATM, Mawakala na NMB Mkononi.

“Ongezeko la matawi linaenda sambamba na ongezeko la ATM, ambapo mpaka sasa, NMB ina ATM 722, mawakala zaidi ya 50,000 na zaidi ya wateja milioni 8. Tuna imani matawi haya ya Chanika na Kinyerezi sio tu yanatanua mtandao wa matawi yetu, bali pia yanakwenda kufikia wateja wengi zaidi katika maeneo haya,” alibainisha Bi. Zaipuna.

Bi. Zaipuna alimkabidhi Dk. Mpango vifaa tiba vyenye thamani ya Sh. Mil. 10, ambavyo ni sehemu ya utaratibu wao wa kusaidia vituo vya afya, zahanati, hospitali ama mashule ya jirani na matawi mapya, vifaa hivyo ni pamoja na Vifaa Maalum 10 vya kupima mapigo ya moyo (Stethoskopu), Flowmeter 5 za Oxygen, Vitanda viwili vya kubebea watoto na Mashine 5 za kupima presha.

Wakati vifaatiba hivyo vilikuwa ni kwa ajili ya Kituo cha Afya Chanika, Kituo cha Afya Kinyerezi, na chenyewe kimepewa viti vya magurudumu vitano, stendi tano za dripu, vitanda vinne vya kufanyia vipimo, skrini tano za kutenganishia vitanda wodini, pamoja na mizani tano za kidijitali ya kupimia watoto uzito, vyote vikiwa na thamani ya Sh. Mil. 10.