Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tabora

MAKAMU wa Rais Dkt Philip Mpango amewataka wananchi wa Nzega mkoani Tabora kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika uboreshaji wa taarifa za Mpiga Kura na kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Pia amehimiza chaguzi hizo kudumisha amani na utulivu na Chama Cha Mapinduzi kutuma salamu za ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu mwakani.

Akizungumza jana katika ziara yake mkoani Tabora Makamu wa Rais Dkt Mpango, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuboresha taarifa zao katika daftari la Mpiga kura na kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.

“ Niwasihi wananchi wa Nzega na Tabora kwa ujumla chagueni viongozi wasio wachumia tumbo, mnaye Bashe anafanya vizuri sana twende katika uchaguzi tukiwa wamoja na tubishane kwa hoja dumisheni amani na utulivu.

“Tukampe Rais wetu Dkt. Samia zawadi katika chaguzi za serikali za mitaa kwa kazi kubwa aliyoifanya lakini pia tutumie uchaguzi huo CCM kutuma salamu kwa wale wenzetu kuelekea uchaguzi Mkuu Mwakani,”amesema.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo na Mbunge wa Nzega Mjini Hussein Bashe, amemueleza Makamu wa Rais kuwa wananchi hao ni wanufaika wakubwa wa utekeleza wa Ilani unaofanywa na serikali ya Rais Dkt Samia hususani katika sekta ya elimu, maji, Kilimo, ujenzi wa miundombinu na miradi mbalimbali.

“Katika Elimu Nzega tunajivunia ujenzi wa shule za kisasa zikiwemo za ghorofa na juzi niliwasilina na Waziri mwenzangu wa Elimu amenihakikishia kuwa sekondari yetu ya Mwanzoli inaenda kuongezwa kidato cha Tano na Sita,”amesema.

Bashe, ameongeza kuwa katika maji anamshukuru Waziri Awesu kwani Nzega kulikuwa na shida sana ya huduma hiyo lakini kwa sasa kati ya vijiji 24 mitaa 14 vitongoji 177 vibaki vitongoji 15 pekee ambavyo havina huduma na tayari maelekezo yametolewa kuhakikisha pampu zenye km 15 zinafungwa na vijiji hivyo viweze kupatiwa maji.

Pia amesema wananchi hao ni wanufaika wa miradi ya Umeme Vijijini (REA) na vitongoji vinavyosubiri huduma hadi sasa ni 38 pekee.

Ametumia fursa hiyo kumuomba Makamu wa Rais kuona haja ya Serikali kukamilisha ujenzi wa barabara za lami katika mitaa na kuanza ujenzi wa barabara ya Itono hadi Kagongwa yenye km zisizozidi 50 ili kufungua fursa za kibiashara.

“Pia nisisitize haja ya uwekaji wa taa za barabarani na kutumia mkutano huu kuwatoa hofu wafanyabaishara wa soko kuu la Nzega na maeneo ya parking kuwa eneo hilo ni kweli linaenda kukarabatiwa wengi wanahofia kunyang’anywa vibanda vyao hakuna atakayewanyang’anya, maboresho yanayofanywa ni kwa ajili yenu muwe na sehemu yenye hadhi ya biashara,”amesema.

Please follow and like us:
Pin Share