Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, amewaagiza Wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa kutekeleza wajibu wao kwa juhudi na nidhamu, huku wakifichua vitendo vyote vya ubadhilifu wa fedha za mali ya umma bila uoga.

Dkt. Mpango alitoa agizo hilo wakati akizindua mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwenye viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani, Aprili 2, 2025.

Aidha, Dkt. Mpango aliziagiza Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa Wakimbiza Mwenge kitaifa ili waweze kutekeleza jukumu lao la kizalendo kwa kuwafikia wananchi na kuwapa taarifa muhimu kuhusu sera, mipango, na mikakati ya Serikali.

Vilevile, alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwataka Watanzania wawaunge mkono na kuwaombea ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025.

Akielezea kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu, “JITOKEZE KUSHIRIKI UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2025 KWA AMANI NA UTULIVU,” Dkt. Mpango alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zitaendelea kusimamia misingi ya kidemokrasia ili kuhakikisha Watanzania wanatimiza haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowafaa.

Pia, alisisitiza kuwa kila mtu mwenye sifa ahakikishe anajiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

Sambamba na kauli mbiu, alisisitiza jumbe nyingine muhimu, ikiwa ni pamoja na kuzingatia kanuni za lishe bora, kupambana dhidi ya rushwa,kupambana dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI na madawa ya kulevya .

Awali akitoa salaam na kumkaribisha mgeni rasmi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kukubali na maelekezo yake ya kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu inayohamasisha wananchi kushiriki kwa amani.

“Huo ni wito ambao unatukumbusha Uchaguzi Mkuu ni haki yetu ya kikatiba kushiriki kwa amani na utulivu ambayo ni msingi wa maendeleo yetu”

Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete anaeleza, vijana sita watakaokimbiza Mwenge kitaifa ambao wameandaliwa kutoka Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar wakiongozwa na Aziz Abubakar, watakimbiza Mwenge katika mikoa 31 yenye jumla ya Halmashauri 195 za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa siku 195.

“Watanzania wenzangu tunatambua kuwa falsafa hii ya Mwenge wa Uhuru ndio chimbuko la Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 , Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964 na Azimio la Arusha la mwaka 1967.

Ridhiwani alisisitiza, Watanzania waendelee Mwenge wa Uhuru kama ulivyoasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961 wakati Taifa lilipopata Uhuru.

Kwa upande wake, Hamza Hassan Juma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera, Wawakilishi), alieleza Mwenge wa Uhuru ni tunu ya Muungano Wetu.

Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakar Kunenge alieleza, mwenge wa Uhuru utakimbizwa kwenye kilometers zaidi ya 1,300 , miradi 64 itatembelewa, kukaguliwa na kuwekwa jiwe la msingi yenye thamani ya sh. Trilioni 1.28.