Na Happy Lazaro, JamhuriMedia, Arusha
MAKAMU wa Rais Dkt. Philipo Mpango ametoa wito kwa Majaji na Mahakimu wanawake nchini kutofumbia macho vitendo vya ukatili kwani wapo wanawake, watoto na wanaume wanaopitia vitendo vya ukatili wa kijinsia au kimwili lakini hawatoi taarifa kwenye vyombo vya sheria ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Amesema kuwa, baadhi ya mila na desturi katika jamii zimekuwa zikitumika kuwakandamiza waathirika, ambapo hali hii ya waathirika wa vitendo vya ukatili kutokutoa taarifa kwenye mamlaka husika inachangia kushamiri kwa vitendo hivi.
Ameyasema hayo leo mkoani Arusha katika ufunguzi wa Jubilei ya miaka 25 ya Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA) na kutoa wito kwa Watanzania wote kuibua taarifa kuhusu vitendo vya ukatili ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.
Aidha Dkt .Mpango amewataka mahakimu na majaji walioko katika utumishi na waliostaafu, kuhakikisha wanajiunga au wanahuisha uanachama wao wa TAWJA kwa kulipa ada.
“TAWJA inahitaji mshikamano na ushiriki wa wanachama wake wote ili kufikia malengo yake, ninafahamu kuhusu changamoto ya ufinyu wa muda kwa wanachama walioko kwenye utumishi, hivyo ninashauri kuendelea kutumia uzoefu wa wanachama waliostaafu katika kutekeleza baadhi ya majukumu ya TAWJA”amesema .
Ameongeza kuwa idadi ya Majaji na Mahakimu wanawake waliokuwepo miaka
25 iliyopita ni ndogo ikilinganishwa na sasa, hivyo endapo wote watakuwa
wanachama hai, TAWJA itaweza kupiga hatua kubwa katika kufikia malengo yake.
“Nawaomba mjenga tabia ya kutambua na kusheherekea mafanikio ya wanawake katika jamii ili kutoa hamasa kwa wasichana na wanawake wengine kujifunza na kuiga mifano hiyo,tunayo mifano ya wanawake hapa nchini waliofanya vizuri katika fani mbalimbali tukianza na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan “amesema Mpango.
Aidha, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanatoa fursa sawa ya elimu kwa watoto wote kwa kuzingatia
mazingira ya sasa, kumeanza kuwa na matukio mengi ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto wa kiume,hivyo ni vizuri wanapopigania haki na usawa wa mtoto wa kike, ni muhimu sana na mtoto wa kiume asiachwe nyuma.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania ,Prof.Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa , historia ya Mahakama 1921-1961 haikutoa nafasi za ajira kwa Majaji na Mahakimu Wanawake, hatua kubwa imefanywa na Serikali ya Tanzania kuongeza idadi ya wanawake katika utumishi wa mahakama.
Hata hivyo, Mahakama ya Tanzania bado inayo safari na umbali mrefu katika jitihada za kufikia asilimia ya hamsini kwa hamsini
ya idadi ya wanawake na wanaume katika nafasi za majaji na mahakimu .
Amesema kuwa,TAWJA inaposherehekea miaka 25 ya kuendeleza nafasi ya
wanawake katika mfumo wa sheria na kukuza usawa wa kijinsia, ni vyema tuipongeza pia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua za makusudi za kuongeza idadi ya Majaji na Mahakimu wanawake.
Kwa mujibu wa takwimu iliyotayarishwa na Msajili Mkuu tarehe 15 Januari 2025 kuonyesha ajira za kila mwaka kati ya Mwaka 2000 (TAWJA ilipoanzishwa) hadi Desemba 2024, Serikali iliiwezesha Tume ya Utumishi wa Mahakama (Judicial Service Commission) kuajiri jumla ya Mahakimu 1,441. Katika kipindi hicho cha miaka takriban 25, Tume ya Utumishi Mahakama iliajiri jumla ya mahakimu wanawake 688 (asilimia 48).
Ameongeza kuwa ,idadi ya Mahakimu wanaume walioajiriwa katika kipindi hicho walikuwa 753 (asilimia 52),mwelekeo wa ajira ya Mahakimu Wanawake ni kwenye usawa asilimia Hamsini, au zaidi. Ipo miaka ambayo ajira ya Mahakimu Wanawake ilizidi ile ya Mahakimu Wanaume— mwaka 2015 [wanawake 75 (adilimia 65), wanaume 40 (asilimia 35)]; mwaka 2018 (wanawake 72) (asilimia 60), wanaume 49 (asilimia 40) mwaka 2021 wanawake 74 (asilimia 54), wanaume 63 (asilimia 46) na mwaka 2024 [wanawake 56 (asilimia 50.45), wanaume 55 (asilimia 49.54)
Aidha amefafanua kuwa ,kuongezeka kwa mahakimu na majaji wanawake imesaidia kuchanganya ‘diversity’ katika wajibu
wa kikatiba wa Mahakama kutoa haki kwa wakati. Majaji na Mahakimu wanatoka katika backgrounds mbalimbali za kijamii,
kitamaduni, dini na rangi lakini wanaunganishwa na Katiba, Sheria, Kanuni za maadili ili kutoa huduma sawa kwa kila anayetafuta haki.
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) na Jaji wa Mahakama ya rufani ,Barke Sehel amesema kuwa ,TAWJA ni chama cha kitaaluma na kimeandikishwa chini ya
Sheria ya Asasi zisizo za Kiserikali kwa namba na pia ni chama Shirikishi cha Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ).
Amesema kuwa,wanachama wa TAWJA ni Majaji na Mahakimu wanawake
waliopo kazini na waliostaafu katika ngazi zote za Mahakama ya Tanzania, Tanzania Bara na Visiwani ambapo pia wakufunzi wa kiume wanatambuliwa kama wanachama wa heshima wa TAWJA.
“Tunaposheherekea Jubelei ya miaka 25 ya TAWJA, tunajivunia kuwa na wanachama wapatao 500 kwa sasa,ambapo Dira Kuu ya TAWJA ni kukuza haki za binadamu na usawa kwa wote, hususan kwa wanawake, watoto na makundi maalum.”amesema .
Ameongeza kuwa ili kufanikisha Dira hii, TAWJA ina Mpango Mkakati wake wa
miaka mitano ambao umeainisha maeneo kumi muhimu ya ufuatiliaji hadi kufikia mwaka 2029/2030 ikiwemo kuendeleza utawala wa sheria, kuhakikisha usawa mbele ya sheria, na kukuza usawa wa kijinsia katika utoaji haki.