Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango
ametoa wito kwa sekta binafsi, mashirika, Taasisi za umma pamoja na Taasisi za dini kuwekeza katika uanzishaji na uendelezaji wa Bustani za Kijani nchini kwa maendeleo endelevu.
Dk.Mpango ameeleza hayo leo Aprili 15,2024 jijini Dodoma wakati akifungua kongamano la kuhamasisha uwekezaji katika bustani za kijani kwa Maendeleo Endelevu (Green Parks) lililoandaliwa na Jukwaa la Maendeleo endelevu ambapo amesema hilo linapaswa kwenda sambamba na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi katika utekelezaji wa agenda hiyo muhimu.
Sambamba na hayo ameagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Mamlaka za Miji, Halmashauri na Majiji kuchukua hatua za makusudi kulinda maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya Bustani za Kijani na kuhakikisha hayavamiwi au kubadilishwa matumizi.
Ametaka maeneo hayo kupimwa na kuwekewa alama za kudumu kuonesha mipaka yake pamoja na kuagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutunga sheria ndogo (by-laws) na kusimamia utekelezaji wake ili kuhakikisha maeneo ya Bustani za Kijani yanalindwa na kutumika kama ilivyokusudiwa.
Pia ametoa wito kwa Mamlaka zote za Miji, Halmashauri za Wilaya na Majiji, kushindanisha vijana wa kitanzania kubuni bustani bora ya kijani katika Makao Makuu ya Wilaya, Mkoa, Mji au Jiji iweje na kuagiza Waziri wa Nchi – OR TAMISEMI na Waziri wa Nchi – OMR kushirikiana kuanzisha mashindano na Tuzo ya Kimkoa na Kitaifa ya bustani bora za kijani katika Miji na Majiji.
Halikadhalika Makamu wa Rais ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanaanzisha Bustani za Kijani tatu kabla ya mwisho wa mwaka 2025 ikiwemo moja ya Bustani ya Mimea kwaajili ya Tafiti za Kisayansi na Uhifadhi (Botanical Garden). Amelitaka Jiji la Dodoma kuchukua hatua ya kutangaza fursa ya kuwekeza katika Bustani tangulizi (pioneer green parks). Ametoa wito kwa sekta binafsi kujitokeza kuwekeza katika kuanzisha bustani hizo mkoani Dodoma ili pamoja na kutunza mazingira kufanya mkoa huo kupendeza zaidi.
Amesema uanzishwaji na uendelezaji wa Bustani za Kijani ni suala linalohitaji ushirikishwaji wa taasisi na wadau mbalimbali wenye utaalam ili kuhakikisha uendelevu wa bustani hizo na thamani ya fedha itakayowekezwa.
Makamu wa Rais ametaja baadhi ya mambo yanayopaswa kuangaliwa kabla ya kuwekeza ni utambuzi na uchambuzi wa mazingira ya bustani, usanifu wa ardhi na bustani yenyewe, aina ya miti na maua yanayofaa katika eneo hilo, kubainisha vifaa vitakavyotumika, sehemu za huduma mbalimbali kama vile kupumzika, michezo na mazoezi, ukusanyaji wa rasilimali pamoja na mpango kazi wa utekelezaji.
Kwa Upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo amesema Mipango ya Serikali ni kujielekeza katika uchumi wa kijani ambao unabebwa katika nguzo kuu tatu, ukuaji wa uchumi ustawi wa jamii na utunzaji wa mazingira. Amesema uwepo wa Kongamano hilo unaenda sambamba na lengo namba 11 na lengo 15 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia ambayo ni kuweka miji na makazi ya binadamu kuwa jumuishi , salama, imara na endelevu pamoja na kulinda uhai katika ardhi na baionuwai.