đź“Ś Asema upatikanaji wa Nishati Afrika bado ni mdogo kulinganisha na Mabara mengine
đź“Ś Asisitiza uendelezaji wa vyanzo vya Nishati uzingatie mustakabali wa vizazi vijavyo
📌 Afungua Kongamano na Maonesho ya Petroli kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25)
Makamu wa Rais, Mhe.Dkt. Philip Isdor Mpango amesema kuwa matumizi ya nishati katika Bara la Afrika hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara bado ni madogo ikilinganishwa na maeneo mengine kama Bara la Amerika, Asia na Ulaya hivyo kuna umuhimu wa kubuni njia bora za kuzitumia rasilimali zilizopo ikiwemo Mafuta na Gesi Asilia ili kuwawezesha wananchi kustawi kiuchumi na kijamii huku suala la utunzaji wa mazingira likizingatiwa.
Amesema hayo tarehe 5 Machi, 2025 wakati akifungua rasmi Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) ambalo litafanyika kwa muda wa Siku Tatu jijini Dar es Salaam.

“Katika kipindi ambacho maendeleo ya nishati endelevu yana mchango mkubwa katika mustakabali wa mazingira, uchumi na jamii zetu na katika kipindi ambacho Dunia inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi bado tunahitaji kutumia rasilimali zetu zilizopo, ikiwemo mafuta na gesi asilia lakini bila kuhatarisha mustakabali wa vizazi vijavyo ili kukidhi mahitaji ya kinishati.” Amesema Dkt. Mpango
Ameeleza kuwa, Afrika Mashariki imebarikiwa na rasilimali nyingi za nishati, ikiwemo mafuta na gesi asilia ambapo Tanzania imegundua gesi asilia, Uganda, Kenya na Sudan Kusini wamegundua mafuta, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wana gesi ya methane, huku Kenya na Tanzania zikiwa na rasilimali za nishati jotoardhi hivyo rasilimali hizo lazima zitumike ili kupunguza pengo la nishati na kuharakisha maendeleo.
“Tunatambua kuwa ulimwengu unakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha madhara makubwa kama vile vipindi visivyotabirika vya mvua, mafuriko, mitetemeko ya ardhi na kuongezeka kwa joto. Tanzania, kama mataifa mengine, imejitolea kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kufanikisha azma ya kutozalisha hewa ya kaboni ifikapo mwaka 2050. Hata hivyo, tunapaswa kuweka uwiano kati ya ukuaji wa uchumi na uendelevu wa vyanzo vyetu kwa kutatua changamoto za leo huku tukijiandaa kwa changamoto za kesho.” Amesema Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango ameeleza kuwa, suala la kuhama kutoka kwenye nishati chafu kwenda kwenye nishati safi haliepukiki kwani ni mkakati muhimu wa kupunguza uchafuzi wa mazingira duniani hata hivyo uwekezaji katika nishati hiyo unahitaji mtaji mkubwa na utaalamu wa hali ya juu ambapo inakadiriwa kuwa Afrika inahitaji kati ya Dola Trilioni 1 hadi 2 kufanikisha malengo ya ya kuelekea kwenye nishati safi ifikapo mwaka 2030 hivyo kuna umuhimu wa kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na kuwa na ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma.
Katika Mkutano huo wa EAPCE’25, Dkt, Mpango amesema kuwa anaamini Viongozi na Watalaam watabadilishana mawazo na uzoefu kuhusu kufungua fursa za uwekezaji katika nishati endelevu bila kusahau nafasi ya rasilimali za mafuta katika upatikanaji wa nishati ya kutosha huku akisisitiza ushirikiano wa kikanda kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, kadri uchumi unavyokua kwa kasi mahitaji ya nishati hasa Gesi Asilia yanaongezeka hivyo Serikali inaendelea na jitihada za kuendeleza miradi ya mkondo wa juu wa petroli kwa lengo la kugundua na kuendeleza vyanzo vipya vya rasilimali za Mafuta na Gesi Asilia.

“ Nampongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuendeleza mkondo wa juu wa petroli ambapo chini ya uongozi wake uzalishaji wa gesi umeimarika katika vitalu vya Songosongo na MnaziBay ambavyo ni muhimu katika uchumi wa gesi.”Amesema Dkt.Biteko
Dkt.Biteko ametaja baadhi ya mafanikio katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia nchini kuwa ni pamoja na uendelezaji wa gesi asilia iliyogunduliwa katika eneo la Ntorya kitalu cha Ruvuma kwa kutoa leseni uendelezaji wake kwa kampuni ya ARA Petroleum na kuongezeka kwa ushiriki wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kitalu cha Mnazibay kutoka asilimia 20 hadi 40.
Naye Waziri wa Nishati wa Uganda, Mhe. Ruth Nankwabira Seitamo, ameeleza kuhusu umuhimu wa fedha zinazopatikana katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia kunufaisha Sekta nyingine huku akitolea mfano kuwa nchini Uganda wameanzisha Mfuko wa Petroli ambao unahudumia sekta nyingine ikiwemo barabara, elimu, afya lengo likiwa ni kuhakikisha kila mtu anafaidika na sekta husika.

Amesema sekta ya Mafuta na Gesi ni muhimu katika kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia hali itakayowezesha pia kupunguza uharibifu na misitu ambapo amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa Nishati Safi ya Kupikia Duniani.
Veronica Nduva, Katibu Mtendaji Jumuiya ya Afrika Mashariki amepongeza Tanzania kuendesha mkutano huo kwa mafanikio na kueleza kuwa unaendana na malengo ya Jumuiya ya EAC ya kuhakikisha kunakuwa na uendelezaji wa rasilimali za Mafuta na Gesi Asilia unaozingatia utunzaji wa mazingira.




