Najua yameandikwa mengi kuhusu Dk. Reginald Mengi. Dk. Mengi, Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP na Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), amefariki dunia wiki iliyopita. Ni kutokana na kifo cha Dk. Mengi, leo nimeahirisha sehehemu ya 13 ya makala yangu ya ‘Jinsi ya Kuanzisha Biashara Tanzania’.
Nilifanya hivyo walipofariki dunia Ruge Mutahaba na Ephraim Kibonde, kama heshima ya pekee kwa wanahabari au wamikili hawa wa vyombo vya habari baada ya kufariki dunia.
Sitanii, kama nilivyosema wakati wa kifo cha Ruge, naamini msomaji wangu ungenishangaa mno iwapo ningeendelea na makala ile bila kuikatiza japo ‘kiduchu’ kumzungumzia mzee Mengi. Jambo moja nilisema binafsi nimebarikiwa kufanya kazi na mzee Mengi kwa nyakati tofauti.
Kwanza kwa kufanya kazi kwenye taasisi yake ya IPP miaka ya 1996/97, lakini pia kufanya naye kazi kuanzia mwaka 2000, hadi siku sita kabla ya Mungu kuchukua uhai wake nikiwa mwanahabari na kiongozi wa vyombo vya habari katika nyakati tofauti.
Dk. Mengi alianzisha kampuni nyingi na amehudumia watu wengi, ila alikuwa na mapenzi ya dhati na vyombo vya habari. Kiongozi huyu ambaye historia aliyoiandika yeye inatuonyesha kuwa ametokea katika familia iliyokuwa na umaskini uliotopea, kati ya mwaka 1986 hadi Mungu alipochukua uhai wake, ametengeneza mabilioni ya fedha. Nimemfahamu zaidi mzee Mengi kupitia kitabu chake cha “I can, I must, I will.”
Siku chache baada ya kuchapisha kitabu hiki nilikisoma na nikakutana naye. Moja ya mambo niliyomweleza ni kuwa amekuwa mfanyabiashara wa kwanza na wa pekee kuanika hadharani siri ya utajiri wake. Hakika kitabu hiki kinaeleza hatua kwa hatua jinsi alivyotengeneza utajiri. Kitabu hiki ni somo na darasa tosha kwa mtu anayetaka kuwa tajiri.
Sitanii, ndiyo maana nimesema kwa kuwa kitabu hiki kimeandikwa kwa Kiingereza, ikiipendeza familia, Jukwaa la Wahariri Tanzania linaweza kukitafsiri katika lugha ya Kiswahili na familia ikakichapisha, kisha kikasomwa na Watanzania wengi.
Kitabu hiki hakika naamini mzee Mengi ameamua kwa makusudi kuwaachia urithi Watanzania, hivyo ni vema tukahakikisha ujumbe muhimu uliomo katika kitabu hiki unawafikia Watanzania karibu wote.
Dhana ya msingi katika kitabu hiki ni kujiamini, kuondoa woga, kufanyia kazi kila wazo unalolipata bila kusubiri kuche au maandiko ya kitaaluma, kuthubutu kama alivyosema Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa ni jambo la msingi sana. Mzee Mengi amefariki dunia siku moja kabla ya maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD). Hakika kifo hiki kimetupoka mtu muhimu.
Siku ya mwisho mimi kukutana na Dk. Mengi ilikuwa Aprili 1, 2019 ofisini kwake katika jengo la Haidery Plaza, Dar es Salaam. Hapa nilikuwa na ujumbe wa watu watano kutoka Taasisi ya Vyombo vya Habari ya Kimataifa (IPI), waliokuja nchini kuangalia ni kwa jinsi gani tunaweza kushirikiana kama nchi kuboresha uhuru wa vyombo vya habari. Itakumbukwa Tanzania imeshuka kutoka nafasi ya 34 katika uhuru wa vyombo vya habari duniani mwaka 2012 na kufikia nafasi ya 118 mwaka huu.
Sitanii, kati ya wosia aliotupatia mzee Mengi mimi na ujumbe niliokuwa nao ni kuwa, katika kuishawishi serikali kulegeza kamba na kutoa uhuru wa vyombo vya habari mpana zaidi kama ilivyokuwa awali tusitumie nguvu. Tutumie diplomasia na mashauriano zaidi.
Baada ya hapo alinipigia simu akiwa nje ya nchi siku ya Muungano Aprili 26, 2019 saa 09:15 alasiri, akaniambia angependa kuona tunawezeshana kwenda Geneva, Uswisi kushiriki mkutano wa mwaka wa IPI utakaofanyika kati ya Juni 4/5, mwaka huu.
Dk. Mengi aliniahidi kuwa angerejea nchini Jumanne au Jumatano, hivyo tungeshauriana zaidi jinsi ya kushiriki vema katika mkutano huo na ule wa Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari uliofanyika Mei 3, 2019 hapa jijini Dodoma. Bahati mbaya, Mei 2, 2019 akafariki dunia. Mipango yote hiyo sasa ni historia, isipokuwa ingawa Mengi amefariki dunia kimwili, kiroho bado anaishi.
Mengi amekuwa kiunganishi kikubwa kwa vyombo vya habari nchini. Ameshirikiana na watu wenye ulemavu, maskini na yeyote awaye, wakiwamo wanasiasa. Shida kubwa ninayoipata ni iwapo kati ya wamiliki wa vyombo vya habari tuliopo yupo aliyejipanga kuvaa viatu vya mzee Mengi.
Mwili wake ulitarajiwa kuwasili jana nchini na kuzikwa kesho kutwa (Alhamisi) Machame, mkoani Kilimanjaro. Wakati tukisema Bwana alitoa, Bwana ametwaa na jina la Bwana lihimidiwe, naomba mambo mawili kama Watanzania tuyazingatie; uthubutu na kutokuwa waoga katika uwekezaji. Raha ya milele uwape Ee Bwana… Dk. Mengi kwaheri ya kuonana.