Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Magufuli, umeingia madarakani huku ukiachwa katika kipindi kigumu cha uchumi, wananchi wengi wakikabiliwa na umaskini wa kutisha.

Wakati unaomba ajira kwa Watanzania, kumbuka ulijinadi kwamba utawaondolea umaskini wao kwa kila kijiji kuambulia mgawo wa Sh milioni 50 na ahadi nyingi za matumaini ya kupata maisha bora ikiwa ni pamoja na maji safi, barabara, reli, kupambana na rushwa na ufisadi uliokithiri nchini. Kwa ujumla, ahadi hizi zinakadiriwa kukomba zaidi ya Sh trilioni 60.

Ulijinadi tofauti na mtangulizi wako aliyekuja kwa kaulimbiu ya “Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mpya” pia “Maisha Bora kwa kila Mtanzania”. Matokeo yake kaulimbiu hizo za Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, hazikuwa na mashiko kwa Watanzania na badala ya maisha bora imekuwa ni kinyume chake.

Imekuwa maisha bora kwa kikundi cha Watanzania wachache, waliojigeuza wakoloni wazawa ndani ya nchi yetu wakiitafuna keki ya Taifa peke yao, na kuweka pengo kubwa kati yao na mafukara ambao ni wengi ndani ya Taifa hili. Wamehubiri yale wasiyoweza kuyatenda, huku wakiwa ni maadui wa haki tofauti na alivyokuwa Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Rais Magufuli ulibahatika kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu na ya Nne na utendaji wako umeonekana wazi kwamba wewe ni mtu wa haki unayeuchukia wizi, rushwa, ufisadi, uvivu na uzembe wa kila namna.

Tangu Serikali ya Awamu ya Pili hadi ya Nne iliyomaliza muda wake chini ya Rais Kikwete, rushwa, ufisadi na uvivu katika taasisi za Serikali na umma vimeshika kasi mno. Wafanyakazi wamekuwa wazembe wa namna ya kutisha lakini ni mahodari wa kupanga dili za wizi wa fedha za umma, wanasingizia kaulimbiu za ubabaishaji kwamba kila mtu atakula kwa urefu wa kamba yake.

Ndiyo maana nasema Rais Magufuli una kazi kubwa mno ya kuwatoa Watanzania katika uongozi wa mashaka na mazoea, hivyo kama utawaiga watangulizi wako hata kwa mabaya yao ni dhahiri hutakuwa na jipya kwa Watanzania.

Ukiwaweka wanamtandao katika madaraka kwa kulipa fadhila unaweza kufanya madudu zaidi ya watangulizi wako na kuigeuza Serikali yako pango la wanyang’anyi, na yote uliyoahidi hayatatimizwa hata moja na kuwakatisha tamaa zaidi wananchi.

Jambo jingine ambalo litakupa rekodi nzuri ya kukumbukwa na Watanzania wote ni Katiba mpya iliyobeba maoni ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba na si Katiba pendekezwa iliyobeba matakwa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwa suala la Katiba mpya, Rais aliyemaliza muda wake ilikuwa ni kete kubwa kwake kukumbukwa na Watanzania, lakini alipowaruhusu makada wa CCM kuhodhi mchakato huo kwa faida yao wenyewe ameipoteza nafasi hiyo.

Januari 17, 1996 Rais Benjamin Mkapa aliteua tume ya kuchunguza kero ya rushwa nchini iliyokuwa na wajumbe tisa chini ya Mwenyekiti Jaji Joseph Warioba. Tume hiyo ilifanya kazi kubwa ya kuchunguza kero za rushwa katika taasisi mbalimbali na kuanika wazi wahusika wa vitendo vya rushwa, lakini aliyeiteua tume hiyo akaiponda.

Ripoti hiyo ikafungiwa kwenye makabati ya Ikulu, hakuna hatua zilizochukuliwa. Rais Magufuli, kama una nia ya kweli ya kupambana na rushwa, anza na ripoti hiyo, usiwaige watangulizi wako walioshindwa kutekeleza ahadi zao wenyewe.

Pia kuna ripoti nyingine ya vigogo wa dawa za kulevya ambayo rais huyo huyo wa Awamu ya Tatu aliomba apelekewe Ikulu kwa lengo kuchukua hatua dhidi ya wahusika. Tangu alipopelekewa ripoti mwaka 2001 kutoka katika taasisi moja isiyo ya kiserikali iliyofanya uchunguzi wa kina kuhusu biashara hiyo na wahusika wake, hakuweza kuchukua hatua zozote zile hadi alipomaliza muda wake na pia Rais wa Awamu ya Nne naye hakuchukua hatua zozote dhidi ya miamba ya rushwa na dawa za kulevya hadi anaondoka madarakani.

Kwa ufupi yatosha kusema wote hawa wameshindwa kutekeleza maagizo yao na kushindwa kujiwekea kumbukumbu nzuri ya kuenziwa na Watanzania. Wewe Rais Magufuli, usiwaige hawa wala kufuata mambo yao. Mungu akupe hekima na maarifa yake katika kuwaongoza Watanzania na zaidi sana uwe na hofu ya Mungu, ukimtumaini yeye wala si wanadamu. Mungu ibariki Tanzania.