Kwanza kabisa nitoe pongezi kwako Dk. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa  kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na pia Makamu wako, Samia Suluhu Hassan.

Pongezi zangu hizi kwa viongozi hawa wakuu nchi ni nzito kutokana na changamoto katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu. Hakuna ubishi kwamba uchaguzi uliopita ulikuwa tofauti na chaguzi zote zilizotangulia, hivyo kuwafanya viongozi hawa kuongezeka uzito katika nafasi hiyo kubwa zaidi nchini.

Rais wangu na Amiri Jeshi Mkuu, Dk. Magufuli, tayari ameingia kazini. Kuna kazi ambayo ameifanya kwa kipindi kifupi huku akitumia mtindo wa aina yake. Pamoja na kuanza tofauti na watangulizi wake, nataraji kuona uteuzi wake ukiendelea kuwa na utofauti ili kuweza kumsaidia kuendana na kaulimbiu yake ya ‘Hapa kazi tu’.

Pamoja ya kuwa mimi si mfanyakazi wa Ikulu ya Magogoni, na wala si mshauri wake wa karibu lakini natambua ya kuwa kwa vile ni msikivu, atasoma maandiko haya na kutafakari kwa muda utakaompendeza kisha kuchukua hatua.

Rais Dk. Magufuli, wachokonozi, wafukunyuku, wapekenyuzi na vizabizabina walikuwa wakitoa ushauri wao hapo awali kwa wakubwa wenzako. Wamekuwa wakitoa ushauri bila kumung’unya maneno ili kufikisha ujumbe usio wa kinafiki. Nami binafsi kutokana na hulka yangu ya kutopenda kujisemea pembeni na unafiki kwangu mwiko, nachukua fursa hii kuanza kutoa ya moyoni.

Kupitia Safu hii Kurunzi ambayo nataraji kuwa utapokea barua nyingi za wazi  kupitia katika kipindi cha urais wako, barua ambazo umekuwa ukizisoma hata kabla ya kuchaguliwa kuwa mkubwa wa nchi.

Nakuomba Rais Dk. Magufuli endapo utakuwa na nia ya dhati ya kumletea mwananchi mabadiliko uliyoyahubiri katika kipindi cha miezi miwili ya kusaka kura na kufanya kazi ipasavyo, angalia haya.

Katika ofisi mbalimbali  zilizo chini yako, kipo kitengo cha mawasiliano  kinachotoa taarifa kwa umma. Kitengo hiki kimekuwa kikiangaliwa na watumishi wanaotakiwa kuwa wamepata mafunzo ya mawasiliano ya umma (Public Relation and Mass Communication).

Masomo haya hutolewa hasa katika vyuo vya uandishi wa habari. Waandishi wa habari ni lazima wapitie masomo haya na kufaulu ambapo huwasaidia kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa ufanisi.

Katika ofisi nyingi nchini kumekuwa na urasimu, kiburi na jeuri ya kutoa taarifa. Maofisa habari wengi (si wote) hawakupitia taaluma ya habari, hivyo kujikuta wakifanya kazi wasiyo na weledi nayo.

Waliobahatika kutoka chuoni na kupata ajira bila kufahamu majukumu yao, wamejaa kiburi na hawapo tayari kutimiza wajibu wao zaidi ya kujiona kuwa wajuzi bila kufahamu taaluma ya habari na mawasiliano. Wakuu hao wa mawasiliano wamekuwa kikwazo kikubwa kwa kuijengea taasisi husika ukuta badala ya kuwa daraja la mawasiliano ya umma.

Hawapo tayari kusaidia kuimarisha mawasiliano yanayoleta tija, bali wao wamekuwa kikwazo katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku bila kujali athari zake.

Watumishi hawa wa umma hawajui na wala hawaoni umuhimu wa waandishi wa habari nchini, hivyo kuwawekea mazingira magumu katika kutimiza majukumu yao ya kuhabarisha umma.

Natambua unafahamu vyema umuhimu wa vyombo vya habari nchini, lakini wasaidizi wako hawa wapo wasioona umuhimu wake katika kuliletea Taifa maendeleo ikiwa ni pamoja na uwajibikaji wa pamoja.

Wamejaa urasimu, hawataki kuwa sehemu ya falsafa yako ya kuhakikisha kila mmoja anatimiza majukumu yake. Wapo kukwamisha juhudi za viongozi kuwasiliana na wananchi.

Rais Magufuli, nakuomba utakapokutana na baadhi ya watendaji jaribu kuchungulia katika vitengo hivi vya habari na mawasiliano, maana vimekuwa vikikwamisha utendaji kazi.

Waandishi wa habari hawathaminiwi pamoja na kuwa mmekuwa mkiuita muhimili wa nne ambao, hata hivyo, haujaainishwa kwenye Katiba. Waandishi wanafanya kazi katika mazingira magumu hata penye wepesi. Ni kweli hakuna kazi rahisi lakini ugumu wa kazi hii umekuwa ukiongezwa na kusababishwa na baadhi ya watendaji wasiojua majukumu yao kwa Taifa hili.

Nakuomba ikikupendeza, utafakari kwa kushirikiana na wasaidizi wako kuona kama ni vyema vitengo vya mawasiliano vikawa na maafisa mawasiliano waliowahi kupitia kwenye vyombo vya habari.

Nayasema haya kwa vile inaweza kuwa njia nzuri ya kujenga utendaji wa pamoja kutokana na kufahamu kwa kina nini maana na majukumu yake kwa umma. Ni mawazo tu, msikasirike marafiki zangu.