Membe34Mwezi mmoja tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, apige marufuku safari za nje ya nchi kwa viongozi nchini, maombi ya viza yamepungua kwa asilimia 90.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini ya kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa iliyokuwa inaongozwa na Bernard Membe katika Serikali ya Awamu ya Nne, chini ya Rais Jakaya Kikwete, ilikuwa ikituma maombi kati ya 100 hadi 150 ya kuomba viza kwa nchi mbalimbali kwa wiki moja.

Taarifa kutoka wizarani hapo zinasema kwamba kwa sasa inaandika kati ya barua 20 hadi 25 za maombi ya viza kwa siku, lakini tangu Rais atoe katazo hilo, zimekuwa zikiandikwa barua mbili kwa siku.

Vyanzo vya habari kutoka wizarani humo zimedokeza kuwa awali kulikuwa na mlundikano wa watu wanaohitaji kupata viza hususani wale watumishi wa Serikali.

Baadaye JAMHURI lilifanikiwa kuzungumza na Mkurugenzi na Mkuu wa Itifaki, Mohamed Maharage Juma, ambako pamoja na mambo mengine, alithibitisha kupungua kwa maombi hayo ya viza.

Maharage anasema kuwa siyo siri kuwa barua hizo zilikuwa zikiandikwa kwa wingi wizarani hapo, lakini katazo la Rais limeweza kusaidia kupunguza kama si kumaliza kabisa safari za nje zisizo za lazima kwa watendaji serikalini.

Anasema kuwa hapo awali wizara hiyo ilikuwa na msongamano wa watu kutokana na wizara kuwaombea viza viongozi wa Serikali  katika balozi mbalimbali nchini.

“Hivi sasa wizara imetulia, tulikuwa tunaandika barua hapa 20 na kuendelea kwa siku, lakini hivi sasa kwa siku tunaweza kuandika barua moja au mbili kwa siku. Rais amesaidia kupunguza safari zisizo na ulazima,” anasema Maharage.

Anaeleza kuwa viongozi wengi wamekuwa hawafiki wizarani hapo kwa ajili ya kuomba viza ingawa wapo ambao walikuwa tayari wamepata viza hizo mapema kabla ya katazo la Rais ambao wamejikuta wakirudishwa wakiwa uwanja wa ndege.

“Kuna ambao katazo hili liliwakuta wakiwa tayari na viza na safari zao zilishapangwa, hao wengi nimesikia wameshindwa kusafiri kwani wamekutana na zuio uwanja wa ndege, wamerudishwa na kuzuiwa kuondoka nchini,” anasema Maharage.

Hata hivyo, anaeleza kuwa si kwamba viongozi wote hawasafiri, bali wapo wanaosafiri kutokana na umuhimu wa safari hizo ambao wizara imeweza kuwasaidia kupata viza.

Suala la kupungua safari za nje pia linathibitishwa na Mwenyekiti wa Taifa wa UDP, John Cheyo, maarufu kama ‘Bwana Mapesa’, anayevutiwa na kasi ya Rais Magufuli akisema kumekuwa na mabadiliko makubwa hasa ya matumizi makubwa ya fedha za Serikali.

Ametolea mfano Shirika la Ndege la Emirates akisema kabla ya utawala wa Dk. Magufuli, kwa siku ndege za shirika hilo zilikuwa zikifanya safari zake kutoka nchini kwa kurusha ndege tatu lakini hivi sasa anafikiri imebaki moja inayofanya safari hizo. 

“Mara nyingi mimi nimekuwa nikisafiri, Emirates sasa hivi ambalo ni shirika, safari zake zilikuwa kama tatu kila siku lakini tangu Rais Magufuli aingie madarakani zimepungua hadi kufikia ndege moja kwa siku labda ya kwenda Dubai na kurudi,” anasema Cheyo.

“Ukiingia Business Class ya Emirates utakuta karibu asilimia 90 ya wasafiri ni wafanyakazi wa Serikali. Wafanyabiashara wengi wanaenda Economy Class kulingana na level zao. 

“Lakini wafadhili wanapokuja, balozi anapokuja hukaa Ecomony Class lakini yule anayepatiwa fedha anakaa first class au Business Class, na kama Rais alivyotoa hotuba yake kuhusu matumizi ya pesa za Serikali ameainisha pesa nyingi zilizotumika kwa safari za nje, na kwa hali hiyo hapatakuwa na pesa nyingi za kuhudumia miradi mbalimbali,” anasema Cheyo.

Anatolea mfano pesa zinazodaiwa na wadau mbalimbali akisema “Hivi sasa tunapozungumza wakandarasi wengi wanadai karibu trilioni moja kwa mambo mbalimbali, sasa kama unatumia pesa zako kwa safari au sherehe nyingine kama Uhuru unategemea nini?

“Sherehe za Uhuru siyo lazima zifanyike kila mwaka kwa sababu utakuta watoto 4,000 wengine wanatoka Zanzibar n.k. hapo ni lazima zitatumika pesa nyingi, kama anataka tuwe na matumizi yanayojitegemea aangalie pesa za Serikali zitumike vizuri,”  ameeleza Cheyo.

Wiki mbili zilizopita, Gazeti JAMHURI liliripoti kwamba miongoni mwa wasafiri wakuu nje ya nchi alikuwa mtangulizi wake, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, anayetajwa kuwa ndiye kiongozi wa nchi katika Afrika aliyesafiri nje ya nchi mara nyingi kuliko marais wengine.

Wakati fulani aliweza kuishi Marekani kwa wiki tatu, akiwa kwenye matamasha na shughuli nyingine za kawaida, huku akitajwa kuwa na msafara wenye watu wengi mno.

Akifungua rasmi Bunge hivi karibuni, Rais Magufuli alizungumzia safari za watumishi wa umma nje ya nchi na kusema wapo waliosafiri kwenda nje ya nchi mara nyingi zaidi kuliko walivyoenda vijijini kuwajulia hali mama zao.

Rais Magufuli alitoa takwimu za fedha zilizotumika ndani ya Serikali, mashirika ya umma na taasisi nyingine za Serikali kwa safari za nje kati ya mwaka 2013/14 na 2014//2015 ambako jumla ya Sh bilioni 356.324 zilitumika kwa ajili ya safari za nje kama ifuatavyo:

•Tiketi za ndege (Air ticket) zilitumia shilingi bilioni 183.160;

•Mafunzo nje ya nchi (Training: Foreign) zilitumia shilingi bilioni 68.612;

•Posho za kujikimu (Per Diem: Foreign) zilitumia shilingi bilioni 104.552;

Wizara na taasisi zinazoongoza kwa matumizi ya safari za nje ni pamoja na Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali  (NAOT) na Wizara ya Mambo ya Ndani.

Dk. Magufuli ameagiza mabalozi wa Tanzania wanaowakilisha nchi katika mataifa mbalimbali na jumuiya za kimataifa, ndiyo watakaofanya shughuli zote kwenye nchi wanazofanya kazi na kuleta taarifa nyumbani Tanzania.

Mbali ya kufuta safari za nje, pia Dk. Magufuli amebadili mfumo wa kusherehekea maadhimisho ya Uhuru ambako badala ya kutumia gharama kubwa kuendesha, amewataka Watanzania kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa kufanya kazi za usafi.

Kadhalika, amefuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani iliyopangwa kuadhimishwa Desemba mosi mkoani Singida. Shughuli hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja imekuwa ikifanyika kila Desemba mosi ya kila mwaka.

Rais Dk. Magufuli ameagiza kuwa fedha zitakazotumika kwenye maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani zitumike kununua dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV) na zile za siku ya Uhuru zitumike kwa usafi wa mazingira ili kupambana na kipindupindu.

Kadhalika Serikali imepiga marufuku utengenezaji na uchapishaji wa kadi za Krismasi na Mwaka Mpya kwa gharama za Serikali na kama kuna taasisi inataka kufanya hivyo, ifanye kwa gharama zake.

Dk. Magufuli ameagiza fedha zilizopangwa kugharamia utengenezaji na uchapishaji huo, zitumike kupunguza madeni ambayo wizara, idara na taasisi za umma zinadaiwa na wananchi na wazabuni.

Sheria ya Sikukuu za Kitaifa (The Public Holidays Act, Cap 35) inampa Rais mamlaka ya kutangaza siku yoyote kuwa sikukuu au mapumziko kama alivyofanya Rais mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete, ambako aliagiza siku ya Novemba 5, mwaka huu kuwa ni mapumziko kushuhudia kuapishwa kwa Rais Dk. Magufuli.

Wakati viongozi wa nchi wakihaha, Kamishna wa Bajeti kutoka Wizara ya Fedha, John Cheyo, ameibuka wiki iliyopita akitaka wananchi kupuuza taarifa kwamba Hazina haina kitu.

“Hazina inazo pesa za kutosha  na tunajivunia kufanya uchaguzi wa mwaka huu,  kununua mashine za BVR  kwa kutumia pesa za Watanzania bila kutegemea msaada wowote kutoka nje ya nchi  na kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu mwaka huu,” anasema Cheyo.

Wakati Cheyo akisema hayo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo, amesema Dk. Magufuli anakusanya fedha kwa sababu “chungu kipo tupu” kuendesha Serikali ya Awamu ya Tano.