Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa MNEC Mhe Dkt Angeline Mabula ametoa onyo kwa watu wasiokitakia mema chama cha mapinduzi kwa kupita katika mitaa na kuanza kuwachafua wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa serikali za mitaa walioteuliwa na chama chake kwaajili ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024
MNEC Dkt Angeline Mabula amefafanua hayo wakati wa mkutano wake wa hadhara katika mtaa wa jiwe kuu ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kusikiliza kero za wananchi na kukagua miradi ya maendeleo ambapo amesema kuwa chama cha mapinduzi kimeshateua wagombea wake kinachotakiwa kufanyika ni kuunganisha nguvu kuwasaidia katika zoezi la kampeni ili waweze kushinda badala ya kuendekeza majungu na usaliti
‘.. Wagombea wa nafasi za uchaguzi wa serikali za mitaa wameshateuliwa, Tunasubiria kampeni zianze ili waje wachaguliwe kuongoza nafasi zao, Lakini sasa kuna tabia imezuka ya baadhi ya viongozi wenzetu na wanachama wasiokitakia mema chama wanapita kuwachafua, Hatutawavumilia ..’ Alisema
Aidha MNEC Dkt Mabula amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa fedha za miradi ya maendeleo zilizoletwa ndani ya Jimbo lake sanjari na kuwaomba kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea maendeleo
Elias Nhkilo ni mtendaji wa kata ya Kitangiri ambapo amemshukuru Mbunge huyo kwa juhudi zake katika kuchangia miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya kata yake ambapo tofali, saruji na fedha taslimu zimetolewa kufanikisha miradi ya ndani ya kata hiyo
Nae Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi ya CCM wilaya ya Ilemela Ndugu Bahati akasema kuwa CCM imetekeleza ilani yake kwa kiwango kikubwa na hakuna sababu za msingi za kushindwa uchaguzi wa Serikali za mitaa na kwamba kiongozi yeyote au mwanachama wake atakaeshiriki usaliti hatavumilika na hatua Kali zitachukuliwa dhidi yake kwani wananchi wanahitaji maendeleo na si malumbano
Abubakar Said na Helena John ni wananchi wa kata ya Kitangiri ambapo wamempongeza Mbunge Dkt Angeline Mabula kwa Kasi yake ya kuwaletea maendeleo huku wakiomba kutatuliwa changamoto ya barabara na upatikanaji wa huduma ya Maji safi na salama.