Nimesikitishwa na aina ya uandishi wa habari uliojiweka wazi katika taarifa iliyonukuliwa kuandikwa na mwandishi wa gazeti moja la kila siku (Tanzania Daima la Agosti 7, 2012), Datus Boniface. Huyu mwandishi, pamoja na wahariri wake walioruhusu habari hiyo kuchapwa walithubutu kusema uongo kuwa eti “ Dk Lwaitama, Prof. Sheriff na Prof Shivji waliushambulia Muungano.” Tena, mwandishi huyu na wahariri walioruhusu habari hiyo ichapishwe wakaenda mbali zaidi na kutumia kichwa cha habari kilichosema eti ‘Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe’.
Nafahamu kuwa Prof. Shivji ameshatoa tamko juu ya upotoshwaji wa hali ya juu uliobebwa na kichwa cha habari hiki na makala nzima ya mwandishi Datus Boniface mwenye aina yake ya ujuzi wa kuandika habari. Mimi katika tamko langu sitajisemea mimi tu kama alivyosema Prof. Shivji katika tamko lake. Nitajaribu kueleza kile nilichodhani kilizungumzwa na kila aliyechangia katika ‘mazungunzo yale ya kifungua kinywa (Breakfast Talk), Jumatatu Agosti 6, 2012 yaliyofadhiliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Wa kwanza kuzungumza alikuwa Prof. Abdul Sheriff na aliainisha kile alichotaka kibainike kama historia na sababu za kuwapo Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Alieleza kile alichotaka kieleweke kama upungufu wa kisheria katika mchakacho wa kuwapo Muungano. Pia alieleza kile alichotaka kieleweke kama Muungano kukosa kuwa na uhalali wa kisiasa (political legitimacy), kutokana na ushirikishwaji hafifu wa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi wa wakati huo na wananchi kwa ujumla.
Akahitimisha maelezo yake kwa kusema Wazanzibari walio wengi sasa hivi wamefikishwa mahali wanapotamani kutumia mchakato wa kuandika katiba mpya, uliozinduliwa hivi karibuni unaoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba kujadili Muungano kwa kina na kuingia kwenye maridhiano mapya juu ya kama Muungano uendelee kuwapo na kama ndiyo kwa mfumo wa serikali ngapi.
Ilikuwa wazi kuwa Prof. Sheriff alikuwa hafikiri kuwa walikuwapo Wazanzibari wengi waliokuwa tayari kuendelea na Muungano wa Serikali mbili kama wa sasa. Sikumsikia mahali popote Prof. Sheriff alipotamka kuwa eti anataka Muungano uvunjwe – yeye kama yeye. Sasa mwandishi Datus Boniface alipata wapi ujasiri wa kumlisha mwanataaluma huyu wa historia wa Kitanzania, hata kama ni Mzanzibari pia? Uandishi wa habari wa aina hii ni wa kusikitisha.
Wa pili kuzungumza nilikuwa mimi, Dk Azaveli Lwaitama. Mimi kazi yangu ilikuwa kujibu hoja za mzungumzaji mkuu (discussant) ambaye kwa kweli alikuwa Prof. Abdul Sheriff peke yake. Kwanza nilimkosoa ndugu yangu Mtanzania mwenzangu Prof. Abdul Sheriff kwa kuomba wote tukubali kuwa viongozi wetu waliotuunganisha kuzaliwa taifa letu la Tanzania, walikuwa watu walioongozwa na dhamira safi katika kuwa waumini thabiti wa itikadi ya Umajumui wa Kiafrika (Pan Africanism), ya kutaka kuwaunganisha watu wa dola zetu hizi waliokuwa wamekusanywa pamoja na wakoloni na kupachikwa majina kama Tanganyika na Zanzibar, bila ridhaa ya wakazi walikuwa ndiyo wengi wa sehemu hii ya Bara la Afrika wenyewe.
Nikaeleze jinsi mwelekeo wa viongozi hawa kuwa haukuwa wa kufungwa sana na matakwa ya kisheria, bali na kile walichokiamini kingesaidia kufanikisha lengo la kuwaunganisha Waafrika wote bila kujali kabila (tribe) au uzawa (race). Nikatolea mfano wa jinsi Mwalimu Nyerere alivyoshiriki katika kuhimiza kuungana kwa Shirazi Association na African Association kuzaa Afro-Shirazi Party (ASP) tarehe 5 Februari, 1959, siku na mwezi ambavyo mwaka 1967 vilikuja kuwa siku na mwezi wa kuzaliwa Azimio la Arusha na mwaka 1977 vilikuja kuwa ni siku na mwezi kilipozaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na kuunganisha Tanganyika African National Union (TANU) na Afro-Shirazi Party (ASP).
Nilisisitiza kuwa leo tunaweza kuuona wazi upungufu mkubwa katika taratibu za kisheria zilizogubika mchakato wa kuunda Muungano, lakini si vizuri kukataa Muungano kutokana na upungufu huu wa kisheria tukasahau kuwa Muungano uliundwa kwa sababu za dhamira ya kuunganisha Washirazi, Waafrika, Waarabu, Wahindi na Wazungu na kuwaweka pamoja kama Waafrika waumini wa Umajumui wa Kiafrika (Pan Africanism), wawe wa dola iloyosimikwa na wakoloni la Zanzibar au dola iliyosimikwa na wakoloni la Tanganyika.
Mwalimu Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume walisukumwa na kutaka kuunda taifa ya Kiumajumui wa Kiafrika – jipya la TANZANIA, baada ya kuona Mzee Jomo Kenyatta wa Kenya na Milton Obote wa Uganda hawakuwa tayari kwa wakati huo – mwaka 1964 – kuunda dola jipya ambayo ingeongozwa na itikadi ya vuguvugu la utaifa wa Umajumui wa Kiafrika (Pan Africanist nationalist movement) la Shirikisho la Afrika Mashariki. Kwa waasisi hawa wa Muungano, taratibu za kisheria hazikupewa kipaumbele bali dhamira safi ya kutenda lililoonekana kuwa la manufaa kwa wananchi walio wengi wa sehemu hii ya Afrika.
Tukumbuke kuwa Mzee Karume na Mwalimu Nyerere walikuwa wanafanya kazi katika mazingira ya kivuli cha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 1964, mwezi mmoja baada ya Uhuru wa Zanzibar Desemba 1963 uliopatikana kwa kufuata taratibu za kisheria lakini matokeo yake yakapinduliwa kijeshi tarehe 12 Januari, 1964 kwa vile taratibu hizo za kisheria zilitumika kukwepa kupatikana kwa ridhaa ya kisiasa ya walio wengi katika kupatika Uhuru ule wa Zanzibar wa Desemba 1963.
Nilitumia muda kuelezea jinsi tabaka la mabepari uchwara Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar lilivyokuwa na ushawishi mkubwa juu ya uongozi wa serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Nikaainisha kuwa hii ndiyo iliyokuwa sababu kubwa ya watetezi wa Muungano wa Serikali mbili, waliokuwa wakifuata nyayo za Mwalimu Nyerere kama mimi vile ni wana-Umajumui wa Kiafrika, kukiri sasa kuwa ukitaka kulinda Muungano katika mazingira ya sasa lazima kukuballi kuwapo kwa Muungano wa Serikali tatu.
Nilitumia muda mrefu zaidi nikieleza kufurahishwa kwangu na mwanasiasa kijana wa chama cha Chadema, Mheshimiwa Zitto Kabwe, kuelezea kuunga mkono kwa dhana ya kutafuta kuulinda Muungano kwa kuridhia kuwapo kwa Muungano wa Serikali tatu. Kwanza, kutakuwapo Serikali na Bunge la Muungano. Serikali ya Muungano itakuwa ndogo yenye kushughulikia mambo ya Muungano machache yasiyozidi manne au matano yahusuyo mambo ya ndani (yaani uhamiaji, uraia, polisi), mambo ya nje (yaani ulinzi wa nje na mahusiano ya kimataifa), uratibu wa mambo ya fedha na mipango ya uchumi (yaani sarafu, sera ya uwekezaji, mambo ya ushuru na kodi), na miundombinu inayohitaji uwekezaji mkubwa(teknohama, uzalishaji na usambazaji umeme, usafiri wa bahari na maziwa, reli, na anga).
Hata haya mambo ya Muungano mengi yake baadaye yatashugulikiwa na Jumuia ya Afrika Mashariki kadiri itakavyokuwa inaimarika kuelekea kuwapo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki. Pili kungelikuwapo Serikali mbili za Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, zilizo sawa kila moja ikiongozwa na Waziri Mkuu na ikisimamiwa na Baraza la Wawakilishi. Mheshimiwa Zitto alipendekeza katika uchaguzi mkuu kuwepo uchanguzi wa Rais na Rais Mwenza wa Serikali ya Muungano na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, pamoja na uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Tanzania Bara na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Tanzania Zanzibar.
(Mwandishi wa Gazeti la JAMHURI, Deodatus Balile, alipendekeza Tanzania Zanzibar iitwe Tanzania Visiwani!) Lengo hapa litakuwa kuzidi kuhimiza kuukubali utambulisho wa kujiita Mtanzania – iwe mtu ni mkazi wa Tanzania Bara au Tanzania Zanzibar – na kufifisha mwelekeo wa kubaguana kwa misingi ya Utanganyika na Uzanzibari. Kwa lengo hili hili la kushamirisha utambulisho wa Utanzania na kufifisha mwelekeo wa kubaguana kwa misingi ya Utanganyika na Uzanzibari, Mawaziri Wakuu wa Seriakali za Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar watateuliwa na vyama husika kutegemea ni chama kipi au vipi vitakuwa vimepata viti vingi au kura nying katika chaguzi za Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi husika.
Kutokuwapo uchaguzi wa wakuu wa Serikali ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kutasaidia kupunguza polepole ushabiki na hamasa za kisiasa zinazojikita kwenye utambulisho wa Utanganyika au Uzanzibari. Haya yote lengo lake litakuwa kutafuta njia za sasa za kuendelea kuwaenzi waasisi wa Muungano – Mwalimu Nyerere na Mzee Karume – ambao dhamira yao ilikuwa nzuri ya kuunganisha Waafrika wote bila kuwabagua kwa misingi ya kabila, rangi, dini, uzawa au upande wa Bahari ya Hindi mtu alikokuwa anaishi kwa sasa au hapo nyuma.
Nilisisitiza umuhimu wa itikadi ya Umajumui wa Kiafrika kwa kusema hata kama itatokea ushawishi wa tabaka lenye kutaka kuvunja Muungano, wakawashawishi Wazanzibari kwa sasa kuridhia kuuvunja Muungano, basi Watanzania Bara waendelee kujiita Tanzania Bara kama Wasudani Kusini walivyoridhia kuiita Sudan Kusini, ili utambulisho wa Kiumajumui wa Kiafrika wa Sudan ubaki kwenye utambulisho wa wote – Kusini na Kazikazini – kuendelea kujiita Wasudani.
Sielewi uandishi wa Datus Bonaface ni wa aina gani uliomruhusu kusuka maneno kutoka kwenye mchango wangu hapo juu wa kusema eti ‘Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe’ au eti “ Dk Lwaitama, Prof. Sheriff na Prof. Shivji waliushambulia Muungano..” Inasikitisha sana kuwapo waandishi wa aina hii na wahariri wanaoruhusu uchapishwaji wa uongo wa kiwango hiki. Wachangiaji kadhaa walifuata mchango wangu kabla ya Prof. Shivji kutoa mchango wake ambao ameueleza vizuri sana katika tamko lake kuhusu upotoshwaji wa hali ya juu uliofanywa na Datus Bonaface, pamoja na wahariri walioruhusu habari hii ya uongo kuchapishwa. Laiti wahariri wale wangeomba ushahidi wa kanda ya kilichozungumzwa wangegundua mara moja kuwa mwandishi wao Datus Bonaface ni mwandishi wa ajabu kweli kweli.
Naliambatisha Tamko la Prof. Shivji kama alivyolitoa; ni wazi Prof. Shivji kamwe hakutamka mahali pale chochote cha kuhalalisha kusema eti ‘Shivji, Lwaitama wataka Muungano uvunjwe’ au eti “Dk Lwaitama, Prof. Sheriff na Prof. Shivji waliushambulia Muungano.” Inasikitisha sana kuwapo waandishi wa aina hii na wahariri wanaoruhusu uchapishwaji wa uongo wa kiwango hiki. Mwalimu Azaveli Feza Lwaitama ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Jukwaa la Dira Afrika Mashariki na Mhadhiri Mwandamizi mstaafu, Kitengo cha Falsafa, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anapatikana kwa barua pepe: [email protected] na simu +255784432696 au +255782807728. Amejinasibu kuwa ni msomaji mzuri wa JAMHURI.