Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azavel Lwaitama (pichani), amesema suluhisho pekee la kunusuru Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni kuwa na Serikali tatu.

Dk. Lwaitama alitoa kauli hiyo katika Mazungumzo ya Asubuhi kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania na kufanyika katika Hoteli ya Court Yard jijini Dar es Salaam jana.

“Tena ikiundwa hii ya tatu isiitwe Serikali ya Tanganyika. Tufanye kama walivyofanya Sudan Kusini. Kuepusha watu kuhangaika, tusema hii ni Tanzania Bara. Hii itawapa fursa wafanyabiashara akina Bakharesa kuendelea kuishi Tanganyika bila tatizo. “Tukisema tunaunda Serikali ya Tanganyika ubaguzi utaanza na itakuwa tabu kweli. Watu wataanza kutimuana,” alisema Dk. Lwaitama.


Mtoa mada, Profesa Abdul Sheriff kutoka Zanzibar, alisema kwa sasa yamekuwapo mabadiliko ya fikra kwa Zanzibar ambapo hata Chama cha Wananchi (CUF) kilichokuwa kinaunga mkono Serikali tatu, sasa kinataka uwepo Muungano wa Mkataba. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Issa Shivji, alisema kudai uwepo Muungano wa Mkataba ni ujanja unaolenga kuvunja Muungano.


“Kwa bahati mbaya watu wamemsingizia sana Mzee Karume, kwamba naye alikuwa akidhani ametia saini Muungano wa Shirikisho na si huu. Hatujawahi kuwa katika kichwa cha Karume, lakini  hapa tatizo ni wanasiasa wanataka kutumia wananchi kutimiza malengo yao,” alisema Profesa Shivji. Baadhi ya washiriki walipendekeza ziundwe Serikali ya Shirikisho, Serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Tanzania Zanzibar, ambapo Serikali ya Tanganyika na Zanzibar zitaongozwa na mawaziri wakuu.