Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
Madaktari nchini wameombwa kuwapeleka wagonjwa wenye matatizo ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya matibabu na siyo nje ya nchi kwani Serikali imewekeza vya kutosha katika vifaa tiba na rasilimali watu.
Ombi hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye kambi maalumu ya upasuaji wa moyo inayofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Open Heart International la nchini Australia.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo alisema kutokana na uwekezaji mkubwa ambao Serikali umeufanya katika Taasisi hiyo hivi sasa wagonjwa wengi ambao ni watanzania na wasio watanzania wanatibiwa JKCI.
“Ni muhimu wagonjwa wenye matatizo ya moyo wakatibiwa hapa nchini hakuna haja ya kuwapeleka nje ya nchi kwani huduma zinazotolewa huko ndizo zinazopatikana katika Taasisi yetu”, amesema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge amesema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita kuanzia Julai hadi Oktoba taasisi hiyo imepokea wagonjwa 60 kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Demokrasia ya Kongo,Malawi,Visiwa vya Comoro, Burundi na Zimbabwe.
“Tulishangazwa kupokea wagonjwa kutoka Ujerumani na Ufaransa ambao wamekuja kutalii hapa nchini lakini baada ya kupata matatizo walikuja kutibiwa katika hospitali yetu, miaka ya nyuma walikuwa wanakwenda Kenya na mataifa mengine lakini sasa wanakuja kwetu hii ni kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanyika,”amesema Dkt.Kisenge.
Dkt. Kisenge amesema katika kambi hiyo ambayo itamalizika kesho wagonjwa 11 wamefanyiwa upasuaji huku wataalamu wa Taasisi hao wakipewa mafunzo ya kubadilishana ujuzi katika upasuaji wa moyo.
Akizungumzia kuhusu magonjwa ya moyo Dkt. Kisenge amesema sababu kubwa ya ugonjwa huo ni shinikizo la juu la damu ambalo chanzo chake ni ulaji wa chumvi isiyopikwa, kutofanya mazoezi,matumizi ya sigara, pombe, unene kupitiliza na msongo wa mawazo na namna ya kukabili ugonjwa huo ni kuepuka vihatarishi vyake.
Aidha Dkt. Kisenge amewasisitiza wananchi kujiunga na bima ya afya kwani gharama ya matibabu ya moyo ni kubwa lakini kama mtu akijunga na bima hiyo itamsaidia kulipia gharama za matibabu pindi atakapoumwa.
“Gharama ya upasuaji wa moyo zinafika hadi milioni 15 au zaidi lakini kama mgonjwa atakuwa na bima ya afya itamsaidia kulipia gharama za matibabu hayo”, alisisitiza Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa Shirika la Open Heart International la nchini Australia Dkt. Darren Wolfers alisema wanajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya JKCI tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015.
Dkt. Wolfers amesema jambo kubwa linalowavutia kufika mara kwa mara JKCI kutoa mafunzo na kufanya kambi za upasuaji wa moyo ni upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa na wataalamu wenye ujuzi mkubwa vinavyowawezesha kufanyika kwa upasuaji.