Na Mwamvua Mwinyi, JamhiriMedia, Chalinze
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, anatamani kuona Rais Samia Suluhu Hassan akiendelea kuliongoza Taifa baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, huku akisisitiza uchaguzi uwe wa amani na salama.
Aidha amemkabidhi liongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025, Ismail Ali Ussi hati ya eneo lenye ukubwa wa hekari 400 ambalo chuo kimoja cha nchini Marekani kilipewa na kimeshindwa kuliendeleza huko Msoga, Chalinze, mkoani Pwani.

Dkt Kikwete aliyasema hayo April 10 mwaka huu wakati Mwenge wa Uhuru ulipoweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa Shule ya Amali Msoga, utakaogharimu bilioni 1.6.
Alieleza, kama mwana siasa na mwana CCM, anaamini Rais Samia anastahili kuendelea kupewa dhamana ya kuongoza kutokana na kasi ya maendeleo na uchumi inayoonekana kwenye uongozi wake.
“Mimi ni mwanasiasa, mwana CCM, natamani Rais Samia Suluhu Hassan aendelee tena, lakini pia wachaguliwe wabunge na madiwani wanaotokana na CCM,” alisema Dkt. Kikwete.
Vilevile Dkt. Kikwete alimkabidhi Ussi, hati ya ardhi yenye ukubwa wa hekari 400 iliyopo Msoga, ambayo hapo awali ilitolewa kwa chuo kimoja kutoka Marekani ambacho kilihodhi na kimeshindwa kuiendeleza kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Dkt.Kikwete, chuo hicho kilitengewa eneo hilo lakini tangu walipopewa miaka mingi iliyopita, hakuna kilichofanyika.
Alisema kwa kuwa serikali ya Halmashauri ya Chalinze inahitaji eneo kwa ajili ya maendeleo ya kijamii na kielimu ameamua kurudisha rasmi ardhi hiyo serikalini.
“Eneo hili tulilitenga kipindi cha nyuma, wakatokea chuo kutoka Marekani wakaliomba,Tukaamua kuwapa, lakini mpaka Jiiii hakuna maendeleo yoyote, Wakifufuka kuja tena niachieni mimi nitashughulika nao mwenyewe,” alieleza Kikwete kwa msisitizo.
Baada ya kupokea hati hiyo kutoka kwa Dkt. Kikwete, Ussi alimkabidhi rasmi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze, ambapo ameagiza eneo hilo litumike kwa malengo yaliyokusudiwa ili liwe na tija kwa jamii.
Pia alimuagiza mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo na kuhakikisha ubora unazingatiwa, ili mradi ukamilike kwa wakati uliopangwa.
Awali Ofisa Elimu Taaluma wa Halmashauri ya Chalinze, Zakaria Wabina, alieleza kuwa shule hiyo itakuwa mkombozi kwa vijana wa eneo hilo, kwani itatoa fursa ya elimu ya amali inayozingatia ujuzi ,stadi za maisha na maarifa ya kujitegemea.

