Safari ya kuupanda Mlima Kilimanjaro ambao ndio mlima mrefu kuliko yote barani Afrika haihitaji mbwembwe bali ni utimamu wa mwili, afya njema na kufuata maelekezo ya waongozaji wageni.

Hiyo ndiyo siri ya mafanikio kwa wale wanaofanikiwa kukifikia kilele cha Uhuru kilichopo mita 5,895 kutoka usawa wa bahari, licha ya changamoto za hapa na pale yakiwamo mabadiliko ya hali ya hewa.

Ili upande Mlima Kilimanjaro na kufika katika kilele cha Uhuru, unahitaji ushirikiano wa watu watatu ambao ni waongozaji wageni, wapishi na wabeba mizigo ya wageni ambao wanajulikana kwa jina la wapagazi ama kwa jina maarufu ‘wagumu’.

Ni ukweli usiopingika kwamba watu hawa watatu ndio tumaini kubwa la mgeni yeyote anayepanda mlima huo kwani kila mmoja ana umuhimu mkubwa kulingana na eneo lake la kazi.

Mwongozaji wageni

Mwongozaji wageni na msaidizi wake ndio wanaoweza kumfikisha mgeni katika kilele cha Uhuru kutokana na kuzifahamu kwa kina njia za kupita hadi kileleni na uwezo wa kupanga safari kulingana na hali ya hewa iliyopo. 

Ni watu ambao wanamwelekeza mgeni afanye nini na kwa wakati gani na mgeni yeyote anayefuata maelekezo hayo anakuwa amejiweka katika mazingira mazuri ya kufikia malengo aliyojiwekea kabla ya safari.

Wapo baadhi ya wageni ambao hupuuza maelekezo ya waongozaji wageni na hawa hujikuta wakiishia njiani ama kwa kupatwa na matatizo ya kiafya, ikiwamo kushindwa kupumua kadiri wanavyozidi kupanda.

Faustine Chombo ni mmoja wa waongozaji wageni nguli aliyeifanya kazi hiyo kwa miaka 20 kutoka Kampuni ya uwakala wa utalii ya Zara Tanzania Adventures. Amesema mgeni yeyote anayeshindwa kufuata maelekezo ya waongozaji wageni anajiweka katika hatari ya kushindwa kufanya vizuri.

Amesema waongozaji wageni ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro wamepewa mafunzo maalumu na maofisa wa hifadhi hiyo ya jinsi ya kuongoza wageni, hivyo wanao utaalamu wa kutosha katika masuala ya kuongozaji wageni.

“Kila ‘guide’ amefundishwa taratibu zote za uongozaji. Lakini baadhi ya wanaokuja kupanda mlima na kujiona wana nguvu na kukiuka kanuni, taratibu na sheria zilizowekwa na ambazo ‘guide’ anazitoa kwa wageni, ndio hao wanashindwa kufanya vizuri, ni muhimu wakafuata maelekezo ya ‘guide’,” amesema Chombo.

Mchango wa wapishi

Hili ni kundi jingine muhimu sana katika kufanikisha safari ya wageni wanaopanda Mlima Kilimanjaro kuanzia siku ya kwanza hadi ya mwisho, kwani suala la lishe ni moja ya nguzo muhimu kumjenga mgeni kiafya na kumwezesha kukamilisha ndoto yake.

Kwa wageni wanaotumia lango kuu la Marangu kupanda mlima huo, kazi ya mpishi huanzia kituo cha kwanza cha Mandara kilichopo umbali wa mita 2,720 kutoka usawa wa bahari kabla ya kuelekea kituo cha pili cha Horombo ambacho kipo umbali wa mita 3,720 kutoka usawa wa bahari.

Kwenye kituo hicho cha Horombo mgeni hukaa hapo kwa siku mbili na kufanya mazoezi ya kutembea umbali wa kilometa 3.4 kuelekea kwenye mwamba wa jiwe mfano wa mnyama aina ya pundamilia maarufu kwa jina la Zebra Rocks.

Hapa wageni hupata fursa ya kujumuika na kupiga picha za kumbukumbu. Mazoezi wanayoyafanya yanalenga kuwazoesha hali ya hewa na kujiweka fiti kabla ya kuanza safari kuelekea kilele cha volkano tuli cha Kibo kilichopo umbali wa mita 4,720 kutoka usawa wa bahari.

Ukiwa Kibo mpishi ana makujumu mawili makubwa. La kwanza ni kuandaa chai ya jioni kwa ajili ya wageni ambao hufika muda wa jioni na mara baada ya zoezi hilo kukamilika anawajibika kuingia tena jikoni kuandaa chakula cha usiku kabla ya wageni kuanza safari kuelekea kilele cha Uhuru.

Mgeni anaporejea kutoka kilele cha Uhuru na kufika Kibo, sharti apate chai na chakula cha mchana kabla ya kuendelea na safari ya kushuka hadi kituo cha Horombo ambako anapata mapumziko kabla ya siku inayofuata kurejea hadi lango kuu la Marangu.

Wapagazi au wagumu

Wanaitwa wagumu kutokana na ugumu wa kazi wanayoifanya kuwahudumia wageni kuanzia siku ya kwanza ya kupanda Mlima Kilimanjaro hadi wanaporejea safari yao ya siku sita ama zaidi kulingana na ratiba ya mgeni.

Kazi yao kubwa ni kubeba mabegi makubwa yaliyosheheni nguo maalumu za kuvaa wageni wakati wa kupanda mlima huo, chakula kwa ajili ya wageni, ndoo za maji safi na salama na mabegi ya nguo zao za kujistiri.

Kabla ya kuanza safari, mizigo yote hupimwa kwa ajili ya kuhakiki uzito unatostahili kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) ambazo zinaelekeza uzito unaostahili kwa kila mpagazi kuwa ni kilo 20.

Mbali na mabegi ya nguo za wageni, vyakula na nguo zao, wagumu hawa hubeba majiko kwa ajili ya kupikia chakula cha wageni na majiko yanayokubalika kwa mujibu wa taratibu za hifadhi ni mitungi ya gesi.

Hawa si watu wa mchezo mchezo. Ukikutana nao njiani na aina ya mwendo wanaotembea ni vigumu kuamini kuwa mzigo aliobeba una kilo 20. Milima na mabonde kwao ni sawa na kifungua kinywa, mwendo wao ni wa kasi ajabu na kamwe hauwezi kushindana nao.

Lakini pamoja na majukumu hayo mazito, makundi haya ambayo ni muhimili mkubwa katika kufanikisha safari za wageni ndani ya hifadhi hiyo, malipo wanayopata kutoka kwa mawakala wa utalii hayaendani na ugumu wa kazi wanayoifanya.

Kimsingi ni malipo ambayo yanadhalilisha utu wao, kwa sababu ni madogo mno ukilinganisha na uzito wa kazi wanazozifanya. Lakini wanalazimika kuyakubali kutokana na umaskini wao wa kipato, kwani upo usemi usemao ‘ukisusa wenzako twala’, maana yake ni kwamba ukisusa malipo hayo wapo wenzako wenye shida zaidi watayapokea.

Kwa mujibu wa tangazo la serikali (GN) namba 228 la mwaka 2008, Bunge liliidhinisha malipo ya dola 20 kwa siku kwa mwongozaji watalii, dola 15 kwa siku kwa mpishi na dola 10 kwa siku kwa mpagazi.

Hata hivyo, chama cha waongozaji watalii kimelalamika kuwa tangu tangazo hilo la serikali kutolewa, zaidi ya kampuni 700 za uwakala wa utalii hazijawahi kuwalipa kwa mujibu wa viwango hivyo. Chama hicho kimesema wanachama wake wameendelea kupewa malipo duni ambayo hayalingani na kazi kubwa wanazozifanya.

Waitara awatumia salamu

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanapa, Jenerali mstaafu George Waitara ameonya kuwa wakala yeyote wa utalii atakayeshindwa kuwalipa mishahara mizuri ‘wagumu’ hao, atafute biashara nyingine ya kufanya.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tanapa, Waitara alikuwa mmoja wa watu ambao wamekuwa wakipanda Mlima Kilimanjaro mara kwa mara kabla ya kutangaza kustaafu rasmi zoezi hilo mwaka jana na kubaki kuwa mhamasishaji.

Amesema kama mwenyekiti wa Bodi ya Tanapa, angependa kabla hajamaliza muda wake katika bodi hiyo ashughulikie kilio cha muda mrefu cha wapagazi, waongozaji wageni na wapishi kuhusu malipo.

Kauli ya Waziri Kigwangalla

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, mwanzoni mwa mwezi huu aliongoza timu ya wapanda mlima kupanda Mlima Kilimanjaro katika kampeni yake iliyopewa jina la ‘HK Kili Challenge’ na kuguswa na kazi ngumu zinazofanywa na wapagazi, waongozaji wageni na wapishi ambao hawakusita kuwasilisha kwake kilio chao kuhusu malipo.

Dk. Kigwangalla amekiri wazi kuwa kwa mtu ambaye hajawahi kupanda mlima huo hawezi kujua umuhimu wa makundi hayo ambayo ndiyo roho ya utalii katika mlima huo. Amesema bila ya watu hao, ni ndoto kwa kampuni za utalii kufanya biashara hiyo kwa ufanisi.

“Tukubaki bila ‘guides’, ‘porters’ na wapishi hutuwezi kuupanda huu mlima. Ni watu muhimu sana lakini kwa mtu ambaye hajapanda huu mlima hawezi akajua umuhimu wao. Mimi nimepanda na nimeona umuhimu wao,” amesema.

Dk. Kigwangalla amesema amepokea malalamiko ya watu hao na kwamba kama wizara watakutana na wadau wote wa sekta ya utalii, hasa wanaojihusisha na kupandisha wageni Mlima Kilimanjaro ili kuzungumzia changamoto hizo.

Swali linabaki je, Dk. Kigwangalla atauweza mfupa uliowashinda watangulizi wake akiwamo Profesa Jumanne Maghembe ambaye aliwahi kutoa muda kwa mawakala hao kutekeleza yaliyomo kwenye tangazo la serikali juu ya mishahara ya wagumu? Muda utatupatia jibu.