Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ifakara

MWENYEKITI wa Umoja wa Wazazi Mkoa wa Morogoro (UWT), Dk. Kellen-Rose Rwakatare ametoa shilingi milioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa madirisha na milango kwenye Madrasat Taqwa iliyopo msikiti wa Igima uliopo kata ya Mbingu Wilaya ya Mlimba mkoani Morogoro.

Akikabidhi msaada huo mwishoni mwa wiki, Dk Rwakatare aliwataka wazazi nchini kujenga tamaduni za kuwa walinzi kwa watoto kwa kuwapeleka kwenye masomo ya dini nyakati za jioni baada ya masomo ya mchana shuleni.

Alisema wazaazi hawapaswi kuwaacha watoto wao wakizagaa mitaani na kuwa hatarini kukumbwa na majanga mbalimbali ikiwemo ya ubakaji.

Alisema madrasa au sehemu yoyote ya mafunzo ya dini ni sehemu salama kwa mtoto na yenye utulivu ambayo itasaidia mtoto kujifunza dini na maadili na kukua akiwa bora baadae mwenye kuweza kuwa hata kiongozi bora.

“Nimewiwa kuja kuchangia madirisha na milango ya madrasa hii kwasababu hii ndio sehemu sahihi tuayomtengeneza mwanadamu na mtanzania wa kesho, mafunzo mema na yenye maadili akipata mtoto inasaidia kuendeleza kuwa na nchi iliyo salama na upendo, “ alisema Dk Rwakatare ambaye pia ni Mkurugenzi wa shule za St Mary’s International Academy.

Mmoja wa watoto wanaosoma kwenye madrasa hiyo, Ridhiwani Salum alimshukuru Dk Rwakatare kwa msaada huo kwa kuwa utawasaidia kuondokana na changamoto ya bugudha kutoka kwa wapitia njia jirani na eneo hilo.

Alisema madirisha yakiwekwa yatasaidia kuzuia ndege kuingia kwenye chumba hicho na kuwaepusha na changamoto ya wezi, kuku, mbuzi kuingia kupitia madirishani na kuwasumbua wakati wakijifunza.

Katibu wa msikiti huo, Hamis Nasoro alishukuru kwa msaada huo ambapo aliomba Serikali na wadau wengine kuwakumbuka kama alivyowakumbuka Mkurugenzi huyo kwani bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mikeka mazuria, na silinigibodi.

Nasoro alisema ujenzi wa madrasa hiyo ulienda sanjari na ujenzi wa msikiti huo uliosimamiwa kwa michango ya waumini wenyewe na kugharimu kiasi cha shiligi milioni 15 na kwamba ujenzi huo ulianza 2012 na unaendelea.

Dk Rwakatare pia alikabidhi shilingi milioni 1.2 kwa Msitiki wa Masjid Yusuf Mdemu uliopo kata ya Mchome Wilayani Mlimba mkoani hapa aliyoahidi kwa ajili ya ujenzi wa choo.

Aliwataka waumini na wadau wengine kujitokeza kusaidia ujenga kwenye nyumba za ibada kwa sababu hiyo itasadia kufanya nyumba za ibada kuwa kamili na waumini wengi kuweza kuzitumia inavyostahili.

Alisema yeye ni mzaliwa wa Mchombe na ameguswa kuchangia ujenzi wa vyoo vya msikiti huo na kuahidi kuendelea kushirikiana na waumini wa msikiti huo katika kukamilisha ujenzi wake.

Imamu Msaidizi wa Msikiti huo, Abasi Abdalah alisema mtu yeyote atakayejenga msitiki kwa ajili ya Mwenyezi Mungu atahesabiwa mema na kwamba alichofanya Mkurugenzi huyo ni sadaka.

Alisema ujenzi wa choo hicho ulianza mwaka 2022 kwa kutumia sadaka za waumini na mpaka kikamilike kinahitaji si chini ya shilingi Milioni nane.

Alisema choo hicho kina matundu 10 ambapo vitano ni kwaajili ya wanawake na vitano kwa wanaume na kwamba wametenga matundu mengine kwaajili ya watu wenye mahitaji maalum.