Wiki iliyopita tuliandika maoni tukichagiza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aanzishe mchakato wa kufukuzwa kazi katika Baraza la Mitihani Tanzania, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Joyce Ndalichako. Tulisema uamuzi wa Baraza la Mitihani (NECTA) kubadili mfumo wa kuchakata matokeo na kufanya wanafunzi wengi kushindwa hauvumiliki.
Maoni hayo tuliyaandika kutokana na taarifa tulizopata kutokana na Kauli ya Serikali iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi. Kauli ya Serikali haikugusia chochote kuhusu ushiriki wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (WEMU), Dk. Shukuru Kawambwa katika mchakato wa kubadili utaratibu huo.
Baada ya maoni hayo, wamejitokeza wasamalia wema walioona si vyema, Dk. Ndalichako akawambwa msalabani peke yake. Wakasema kama Serikali imeamua kumwaga mboga, basi heri nao wamwange ugali. Wametuwezesha kupata nyaraka za siri zilizolishinikiza Baraza la Mitihani kufikia uamuzi huu. Tumechapisha taarifa taarifa na nyaraka hizo.
Taarifa hizi zimeanzia ukurasa wa kwanza wa toleo hili, zikarukia ukurasa wa tatu na hatimaye zikaishia ukurasa wa nane na tisa kutokana na umuhimu wake. Kwa kuona unafiki uliofanywa na viongozi wa Serikali katika kutoa taarifa husika, tumeojiridhisha pasi shaka kuwa kilichofanyika ni sawa na kutetea takataka kwa nia ya kupalilia uchafu kuendelea kuwapo.
Tumesikitishwa na hatua ya Serikali kuuzunguka mbuyu, badala ya kuukumbatia au kung’oa mizizi mbuyu ukaanguka wenyewe. Malalamiko ya wananchi ni mengi. Wazazi wanalia na baadhi ya wanafunzi tayari wamejiua kutokana nakushindwa mitihani katika mazingira ya kutatanisha. Kilichotusikitisha, ni kuona kuwa uamuzi huu ni wa Serikali si wa Dk. Ndalichako.
Hatumuondoi Dk. Ndalichako katika kadhia hii, kwani kama aliona unafanyika uamuzi wenye madhara makubwa kiasi hiki alipaswa kuukataa na kulijulisha taifa hivyo. Na kimsingi asingeweza kuukataa kwani ndiye aliyeupendekeza. Kilichotusikitisha zaidi ni kuona Waziri wa WEMU na Naibu wake, Philip Mulugo walishiriki uamuzi huu, lakini hawaguswi.
Tunasema Kawambwa kwa kushiriki kikao cha uamuzi akiwa Mwenyekiti na Mulugo akiwa Katibu, nao wanapaswa kuwajibika. Profesa Rwekaza Mukandala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Mitihani na Bodi yake nao wanapaswa kuwajibishwa. Tunasema bila kufanya hivyo, watendaji wataendelea kuifanyia mazoezi nchi hii.
Tunapendekeza Dk. Kawambwa na Mulugo ama wawajibike kwa kujiuzulu au wafukuzwe kazi wasipojiwabisha. Viongozi hawa wanachezea akili za Watanzania na hawaonekani kama wanaisaidia wizara hii. Kuanguka kwa elimu, hakuwezi kutenganishwa na ufanisi wa Waziri mwenye dhamana na sekta hiyo. Tunasema wakati wa kufanya uamuzi mgumu umewadia. Chukua hatua.