Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, amefungua shauri katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala akiomba amri ya mahakama kulizuia Gazeti la JAMHURI kuchapisha na kusambaza habari zinazomkashifu.

Nyaraka za mahakama ambazo zimewasilishwa kwa JAMHURI zililitaka gazeti hili kufika katika mahakama hiyo jana Jumatatu kwa ajili ya kusikiliza shauri hilo.

Katika shauri hilo, Dk. Kigwangalla anaiomba mahakama itoe amri kulizuia gazeti hili lisichapishe na kusambaza habari zinazomhusu hasa zikiwa na mwelekeo wa kashfa.

Katika hoja zake, Dk. Kigwangalla anadai kuwa taarifa zilizochapishwa na kusambazwa na JAMHURI zimemkashifu na kumshushia hadhi na heshima yake kama waziri na mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ingawa katika mlolongo wa habari hizo JAMHURI lilimtafuta Dk. Kigwangalla bila mafanikio, kupitia nyaraka hizo za mahakama, Mbunge huyo wa Nzega Vijijini anakanusha tuhuma zote zilizoandikwa kumhusu.

Hatua hiyo ya Dk. Kigwangalla inakuja baada ya JAMHURI kuripoti mlolongo wa habari kumhusu waziri huyo baada ya hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli kumpa yeye na Katibu Mkuu wake, Prof. Adolf Mkenda, siku tano kumaliza tofauti zao.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, viongozi hao wakuu wa wizara walikuwa hawasalimiani.

Katika uchunguzi wake, JAMHURI lilibaini kuwa kutofautiana kati ya Dk. Kigwangalla na Mkenda kulitokana na tabia ya waziri huyo kukiuka taratibu za kiofisi, hasa kuhusiana na matumizi ya fedha.

Tayari Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeguswa na matumizi mabaya ya fedha za umma yanayodaiwa kufanywa na Dk. Kigwangalla, na kuna taarifa za uhakika kuwa imeanza kumchunguza.

Pamoja na ofisi hiyo, kuna kikosi kazi kilichoundwa na mamlaka za juu kuchunguza suala hilo na tayari kimekwisha kubisha hodi katika taasisi mbili kati ya nne zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Taasisi kuu zenye ukwasi zilizo chini ya wizara hiyo ni Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Dk. Kigwangalla amekuwa kwenye ugomvi mkubwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Prof. Mkenda, chanzo kikielezwa kuwa ni amri za waziri huyo za kuchotewa fedha kutoka kwenye taasisi zilizo chini ya wizara anayoiongoza.

Katibu Mkuu anataka matumizi ya fedha yafuate miongozo, ilhali waziri akitumia mamlaka yake ya kiongozi mkuu wa wizara kupewa anachotaka. Fedha nyingi amekuwa akizichota kwa matumizi ya kile anachosema ni kutangaza utalii kupitia kwa wasanii mbalimbali.