Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WAZAZI na walezi nchini wametakiwa kuhakikisha wanatenga muda wa kutosha wa kukaa na kulea watoto wao kwa kuzingatia mila na desturi nzuri.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya mtoto kwa Nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Waziri Gwajima amesema malezi na makuzi ya watoto kwa sasa yanaathiriwa na changamoto mbalimbali zikiwemo migogoro ya kifamilia ambayo inawaathiri, huku wazazi na walezi hawana muda wa kulea watoto wao kwa kuwa wapo bize na shughuli zingine.
“Tunahitaji kutafakari haya na kuchukua hatua ili watoto wetu wawe salama, tumedhamiria kuwasaidia wazazi na walezi ambao wanakuwa katika shughuli mbalimbali za usiku, ila tunatakiwa kuhakikisha wanatenga muda kwa ajili malezi ya Watoto,” amesema.
Ametoa rai kwa washiriki kujadili kisha kuja na mbinu bora zaidi za kuimaisha afua za malezi na makuzi ya Watoto kwa kuzingatia mila na desturi nzuri.
“Nasisitiza kuhusu mila na desturi nzuri kwani zingine zinamadhara kwa watoto mfano masuala ya ukeketaji yana madhara kwa watoto wetu hivyo hatupendi kuona yanafanyika,” amesema.
Hata hivyo amesema ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano ambao una manufaa mengi lakini umekuja na changamoto zake kwa Watoto ambao wanahusishwa na matumizi yasiyofaa ya mtandao yanasabbaisha Watoto kufanywa ukatili mitandaoni.
“Tunatakiwa wote tuongee lugha moja hasa ya kuwasaidia Watoto, tusikubali kuwaacha peke yao ili dunia iwafunde,” alisema
Aidha Waziri Gwajima amesema Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeendelea kuimarisha huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto katika ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika, zikiwemo jitihada mbalimbali za kuhamasisha na kufanya ushawishi kwa watoa maamuzi na watunga Sera ili masuala ya malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto yapewe kipaumbele.
“Imewezesha nchi nyingi barani Afrika kuwa na Sera na Programu maalum za masuala ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto na Serikali za nchi mbalimbali zimeweza kufanya maamuzi ya kutoa elimu bure katika shule za msingi pamoja na kuanzisha na kuyafanya madarasa ya awali kuwa sehemu ya elimu ya msingi,” amesema.
Ameongeza kuwa baadhi ya nchi za Afrika zimeandaa na zinatekeleza Sera maalum kwa ajili ya Watoto, Mwaka 2016 Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki iliandaa Sera ya Mtoto inayotekelezwa kwa pamoja na nchi za Afrika Mashariki ambayo pamoja na mambo mengine inaelekeza kuimarishwa kwa huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
“Hali hii imeongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto hasa wale wanaoishi katika maeneo ambayo hakuna huduma ya vituo vya kulelea watoto wadogo mchana haipatikani,” amesema Gwajima.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Anna Athanas Paul amesema Mlee mtoto katika njia impasayo naye hataiacha hata atakapokuwa mtu mzima. Mwana mpumbavu ni mzigo kwa mamaye lakini mwana mwenye hekima ni fahari kwa babaye. Kwa hiyo wamama ni jukumu letu kuleta wana wenye hekima
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema kila mtoto ametokana na mzazi ambaye ni Baba na Mama na mtoto huyo anaweza kuwa na mlezi ambaye ni ndugu wa wazazi, kutokana na ukweli huo hakuna jambo linalosababisha kuwepo kwa watoto wanaoitwa wa mtaani kwani hakuna mtaa unaozaa watoto.