Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,amesema CCM itawachukulia hatua za kimaadili viongozi,watendaji na wanachama watakaobainika kujihusisha na vitendo vya kuhujumu mchakato wa ndani ya Chama wa kura za maoni.
Hayo ameyasema wakati akizungumza na Kamati za siasa ngazi za matawi,wadi,majimbo na Wilaya ya mjini kichama katika mwendelezo wa ziara ya Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC,CCM Taifa Zanzibar ya kukagua uhai wa kisiasa na kuimarisha chama.

Amesema katika safari ya kuleta mabadiliko ndani ya CCM ni lazima kufanya maamuzi magumu ya kulinda hadhi ya Chama kwa kuchukua hatua za kimaadili baadhi ya watu wanaotumiwa na makundi ya watu wachache kuleta migogoro na vurugu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa dola wa mwaka huu.
Katika maelezo yake Dkt.Dimwa,ameweka wazi kuwa CCM Zanzibar haitowapa nafasi za uongozi baadhi ya wanachama wenye historia ya mienendo isiyofaa kimaadili ambao ni wapiga ‘dili’,rushwa,wizi,ufisadi,wafitinishaji na matapeli.
“Huu ndio wakati wa kufanya mabadiliko ya kuondosha na kudhibiti makando kando ndani ya chama ili tupate viongozi sahihi wenye uzoefu wa kisiasa,waadilifu,wachapakazi,wabunifu na wenye uwezo wa kujenga hoja na kunishauri serikali mambo yenye maslahi kwa wananchi wote.”alisema Dkt.Dimwa.

Alieleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuzungumza na Kamati hizo za ngazi mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu wa dola wa mwaka 2025.
Kupitia ziara hiyo alifafanua mabadiliko ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022 yaliyofanyika katika Mkutano mkuu maalum wa januari 18 hadi 19, mwaka 2025 ya kuongeza idadi ya wapiga kura kwenye vikao vya kura za maoni kwa wagombea wa ubunge,uwakilishi na udiwani.
“Mabadiliko haya ya kikatiba yanalenga kuongeza uwazi na ushitikishwaji wa wanachama wengi zaidi katika mchakato wa uteuzi wa wagombea ,hatua itakayopunguza malalamiko ya upendeleo katika kuwapata viongozi bora wa kuongoza wananchi”alifafanua Dkt.Dimwa.
Kupitia ziara hiyo aliwakumbusha wanachama kuwa CCM imetangaza rasmi mchakato wa ndani ya chama wa kuchukua fomu za kura za maoni za kuwania nafasi za kugombea ubunge,uwakilishi na udiwani katika uchaguzi wa dola octoba mwaka huu,ambapo fomu zitaanza kutolewa Mei 1 saa hadi Mei 15,mwaka 2025 na kwamba huo ni mchakato wa ndani bado muda wa kampeni haujatangazwa hivyo viongozi waliopo madarakani waendelee kutekeleza majukumu yao.

Alisema kuna baadhi ya viongozi wa chama kwa baadhi ya majimbo wameanza kupanga safu za viongozi wanaowataka wao kinyume na utaratibu na kwamba yeyote atakayebainika kukiuka atachukuliwa hatua na atakuwa hana sifa ya kuwa kiongozi.
Naibu Katibu Mkuu huyo,aliwambia wanachama na wananchi kwa ujumla kuwa CCM itaendelea kufanya siasa za kistaarabu,demokrasia,utu na kuheshimu sheria za nchi sambamba na kudumisha amani na utulivu ili wananchi waendelee kutekeleza majukumu yao kwa amani.
Dkt.Dimwa,aliwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 iliyoleta Mapinduzi ya kimaendeleo kwa wananchi wote bila kujali tofauti za kisiasa,kidini na kikabila.
Naye Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya organazesheni CCM Zanzibar Omar Ibrahim Kilupi,aliwasihi wajumbe hao kuendelea kuwahamasisha wanachama na wananchi waliojiandikisha katika daftari kuhakikisha wanaipigia kura CCM ili ipate ushindi wa kishindo.
Akizungumza katika ziara hiyo Katibu wa Kamati maalum ya NEC,idara ya itikadi,uenezi na mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,alisema Chama Cha Mapinduzi kinafanya siasa za kisayansi zinazojikita utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kutatua kwa wakati changamoto za jamii.
