Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Chato
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Anthony Diallo amewataka wakulima wa pamba kununua mbolea pindi wanapouza mazao yao ili kuwawezesha kuzitumia wakati msimu wa kilimo unapowadia.
Amesema ni vyema wakulima kuhifadhi pembejeo badala ya fedha, kwani mahitaji ya kila siku ni mengi, na mara nyingi wakulima huishia kutumia fedha walizotenga kwa pembejeo, hivyo kulima bila kuitumia pembejeo hiyo muhimu.

Hayo yamebainika Februari 18, 2025 wakati wa ziara ya Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Anthony Diallo katika vijiji vya Necezi na Songambele wilayani Chato.
Akizungumza na wakulima wa Kijiji cha Necezi, Dkt. Diallo amesema ziara hiyo imelenga kufuatilia utekelezaji wa mpango wa ruzuku na uhamasishaji unaofanywa na Mamlaka katika kuhamasisha matumizi sahihi ya Mbolea kwa wakulima wa zao la pamba na kujionea namna wanavyonufaika na mbolea hiyo.
“Tunataka kuhakikisha ruzuku inatumiwa ipasavyo. Maafisa ugani wamewapa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, na tumeona mafanikio. Tunataka wakulima wengine waige mfano wenu,” amesema Dkt Diallo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, amesema Mamlaka imeendelea kuboresha hali ya upatikanaji wa mbolea kwa wakulima kwa kuweka bei elekezi inayozingatia umbali wa Kijiji kilipo ili kuongeza motisha kwa wafanyabiashara lakini pia kuhakikisha mkulima ananunua pembejeo hiyo karibu eneo lake na kuongeza mwamko wa matumizi ya pembejeo hiyo.

“Awali matumizi ya mbolea yalikuwa kiasi cha tani 363,599 kwa mwaka 2021/2022 kutokana na bei ya pembejeo hiyo kuwa juu na kuwafanya wakulima kushindwa kumudu, lakini sasa tunatarajia kufikia matumizi ya tani milioni moja kwa msimu huu wa kilimo kwani wakulima wengi wameona tija inayotokana na matumizi sahihi ya mbolea” ameongeza Laurent.
Mkurugenzi Laurent aliendelea kusema, ziara hiyo imebaini changamoto za usambazaji wa mbolea, ambapo baadhi ya vijiji havijafikiwa na wakala wa mbolea kutokana na miundombinu duni na mwitikio mdogo wa matumizi ya mbolea na kueleza TFRA itashirikiana na wadau wa tasnia ya mbolea hususan wafanyabiashara na wazalishaji ili kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima kwa wakati na kwa bei nafuu.
Kwa upande wao wakulima wa pamba katika vijiji vya Nekezi kata ya Ipalamasa na kijiji cha Songambele wilayani Chato wameeleza kufurahishwa na mpango wa ruzuku ya mbolea ulioanzishwa na Serikali, wakisema umeongeza uzalishaji na kuimarisha maisha yao.
Akizungumza mara baada ya kupokea ugeni huo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nekezi kata ya Ipalamasa wilaya ya Chato, Samwel Mbikili, ameeleza kuwa, wakulima wa pamba sasa wanapata kiasi cha kilo 2000 kwa ekari moja, tofauti na awali walipopata mavuno kidogo kutokana na kutokutumia mbolea kwenye kilimo.
“Tunashukuru sana juhudi za Serikali za kutuhamasisha na kutupatia mafunzo ya kilimo bora. Tunaomba pia kituo cha kuuzia mbolea kisogezwe karibu ili kupunguza changamoto za usafirishaji,” alisema.
Naye mkulima wa mfano wa zao la pamba kutoka katika Kijiji cha Songambele, Saimoni Lutabeka amesema, alibadilisha mbinu za kilimo kwa kuanza kutumia mbolea aina ya NPK kutoka Minjingu na sasa anavuna zaidi tofauti na awali.
“Tunaiomba Serikali iendelee kutuunga mkono wakulima maana sasa mavuno yanaongezeka, na hali ya maisha ya wakulima inaboreka,” alisema.
Pamoja na ziara hiyo, Mamlaka kwa kushirikiana na Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) inaendelea kutekeleza mpango wa kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea katika mashamba ya pamba ya mfano Wilayani Igunga ambapo Meneja Sehemu ya Udhibiti Ubora na Majaribio kutoka TFRA Schola Mbalila anaendelea na uhamasishaji huo.
Mbalila amefafanua kuwa, tathmini iliyofanywa na TFRA na TCB kwa wakulima waliofikiwa na mpango huo kwa Mkoa wa Tabora umekua na matokeo chanya ya uzalishaji ambapo wakulima wamekiri kuona utofauti wa shamba la pamba lililotumia mbolea na shamba la pamba lisilotumia mbolea.
Mpango huo umekuja kufuatia uwepo wa mavuno hafifu ya pamba kila msimu, ambapo wakulima wa zao hilo hulima kwa mazoea bila kuzingatia kanuni bora za kilimo ikiwemo kutumia mbolea kwa usahihi na hivyo kupelekea mavuno hafifu.
Mwenyekiti wa Bodi Dkt. Diallo ameambatana na wajumbe wa bodi, Patrick Mwalunenge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Juma Mdeke na Lilian Gabriel. Aidha, ameambatana Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa Mamlaka, Elizabeth Bolle na watumishi wengine wa Mamlaka.
