Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Ifakara

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) Mkoa wa Morogoro Dk. Careen-Rose Rwakatale amewataka viongozi wa (CCM) Wilaya mbalimbali mkoani hapa kuhakikisha wanajitoa katika ujenzi wa wa chama hawadhalilishwi kwa kufukuzwa kwenye nyumba za kupanga.

Dk. Rwakatale alisema hayo jana wakati akikabidhi bati 50 zenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 1.5 kwa viongozi wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kilombero kama ahadi yake aliyoitoa wakati ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Jumuiya hiyo ulioanza hapo mwaka Jana 2023.

Alisema watumishi wamekuwa wakipata tabu sana kwa sababu kupanga nyumba sio vizuri, ambapo ikitokea wenye nyumba wamekasirika wanaweza kumfukuza au kumtolea vyombo nje na hiyo ni kumdhalilisha mtumishi na kukidhalilisha chama.

“Nyumba za kupanga kwa mtumishi siyo nzuri anaweza kudhalilishwa yeye au chama hasa pale anapokosa hela za pango lakini kwenye nyumba zetu atakuwa amekaa kwa kutulia huku akitekeleza majukumu yake bila wasiwasi wa kufukuzwa” alisema.

Aidha alisema tayari amefanya ziara kwenye maeneo mbalimbali kuhamasisha ujenzi wa nyumba za watumishi wa Chama ambapo ameshachangia ujenzi katika Wilaya za Gairo, Morogoro vijijini, Malinyi na Kilombero na ambapo ameahidi kuzunguka tena kwenye maeneo hayo kuangalia kama kumeanzishwa ujenzi ili achangie kwa maendeleo ya chama.

Aidha aliwaomba viongozi wengine wa Jumuiya zote tatu Jumuiya ya Wazazi, Umoja wa wanawake na Vijana wa CCM kuendelea kutoa michango yao ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.

Dk. Rwakatare alisema tangu jengo hilo limeanza walimshirikisha na kuanzisha ujenzi kwa mchango alioutoa ambapo wadau wengine waliendelea kutoa michango yao na kufikia asilimia 80 ya ujenzi huo mpaka sasa.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Wilaya ya Kilombero Saidi Mrisho alisema ujenzi wa jengo hilo lenye vyumba vitatu- kikiwemo chenye choo ndani, choo cha nje, jiko, sebule na stoo ulioanza mwezi Desemba mwaka 2023 na unatarajia kukamilika mwaka 2025 umeshatumia kiasi cha shilingi Milioni 14 ambapo unatarajia kutumia shilingi Milioni 20 katika kukamilisha ujenzi wa huo.

Alisema ujenzi huo ukikamilika utafanya Katibu kuwa karibu na Ofisi za Chama na kufanya kazi za Jumuiya kwa ufanisi mkubwa kwani kwa sasa anaishi mbali na ofisi za chama hicho.

Alisema changamoto kubwa hasa huwa kipindi cha masika kutokana na hali ya eneo hilo lilivyo ambalo hujaa maji wakati wa mvua nyingi na kumchukua muda zaidi kufika ofisini na wakati mwingine kushindwa kufika kabisa.

Mrisho alimshukuru Dk Rose kwa michango yake anayoendelea kutoa katika ujenzi wa nyumba hiyo ya mtumishi wa chama ambayo itatumiwa na Katibu yoyote atakayefika kuhudumia hata kama aliyepo akimaliza muda wake au kuondoka ambapo alimuomba kuendelea na moyo huo wa kuchangia Jumuiya za mkoa wa Morogoro.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kilombero, Jitihadi Jalala Jitihadi, alisema kukamilika kwa ujenzi wa nyumba hiyo kutamsaidia kutimiza majukumu yake ya kuihudumia Jumuiya kwa ufanisi sababu amekuwa akishindwa kuwasikiliza kwa wakati wajumbe walipofika ofisini kutokana na kushindwa kufika kwa wakati ofisini kwa sababu ya kukaa mbali na ofisi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wilaya ya Kilombero Luth-Better Makoloweka, alisema ujenzi wa nyumba hiyo unaoenda sanjari na ujenzi wa nyumba za watumishi wengine wa Jumuiya wilayani hapo utasaidia kuweka ulinzi thabiti kwa watumishi na kuwaepusha kukabiliana na changamoto za usalama wao hasa katika kipindi cha uchaguzi unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu.