Na Mathias Canal, Katoro-Geita
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mhe Dkt Doto Mashaka Biteko (Mb) ambaye pia ni Waziri wa Madini amekemea vikali kejeli, kutweza utu wa viongozi na kauli za kuudhi ikiwemo matusi.
Amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan aliruhusu mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa lakini baadhi ya wanasiasa wanatumia vibaya uhuru huo na kuanza kashfa dhidi ya viongozi.
Mhe Biteko ameyasema hayo mjini Katoro katika Jimbo la Busanda wakati wa mkutano wa hadhara wa wananchi ulioongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Ndg Nicolas Kasendamila kwa ajili ya kueleza mafanikio ya serikali na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo itafanyika katika majimbo yote ya mkoa huo.
“Ukweli tufanyeni siasa maana siasa ni pamoja na kuwa na mawazo kinzani, wacha tuyafanye lakini tusichukue muda mwingi tukaruhusu kutukanana, kudhalilishana, tukaruhusu viongozi wa nchi yetu wakatwezwa utu wao” Amekaririwa Dkt Biteko
Mhe Biteko amesema kuwa wote wanaotoa kejeli na matusi kwa viongozi wanapaswa wapuuzwe kwa sababu hawana hoja wala ajenda ya maendeleo.
Mhe Biteko amesisitiza ulazima wa wana CCM kujibu hoja bila kujibu kejeli ama matusi, waushinde ubaya kwa wema huku akisema kuwa wananchi wa vyama vyote ni ndugu na sio maadui. Na amewataka wa vyama vingine kuheshimiana miongoni mwao na kuwaheshimu wana CCM maana wote ni ndugu.
“Hakuna muujiza wa kuwatambua watu wanaosema uongo ama wanaosema ukweli zIdi sana watatambuliwa kwa matendo yao, kadhalika Rais wetu Mhe Samia atatambuliwa kwa matendo yake na sio maneno, kazi zake zinamtambulisha kama Rais aliyeamua kuwaletea maendeleo ya haraka Watanzania”. Amesisitiza Mhe Biteko
Kuhusu maendeleo Mhe Biteko amesema kuwa Maendeleo ni mchakato wa ukuaji unaoweza kuhusisha: Matumizi ya ardhi, sayansi na teknolojia, sayansi ya jamii, biashara na ueledi hivyo Mhe. Rais anaweza kufanya kila kinachotakiwa kufanywa lakini bado kukahitajika jambo jingine kufanyika kutokana na uhitaji wa wakati huo.