Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko amemwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Mpango kufungua mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma nchini SHIMMUTA na kuagiza mashirika kuondokana na visingizio visivyo na msingi ili kutimiza azma ya mashindano hayo.

Dkt. Biteko ametoa maelekezo hayo Jijini Tanga ambapo amesema kumekuwa na visingizio vya kuwakosesha watumishi wa umma kushiriki mashindano ilhali ni suala linalofahamika na liko kwenye kalenda ya kila mwaka ya mashirika husika.

“Utaratibu huu wa kukubaliana jambo lakini jambo tulilokubaliana halifanyiki inatufanya tukose uhalali wa kuwasimamia wengine, nilitaka kujua kwanini hatupeleki washiriki katika mashindano haya. Kama tunaona mashindano haya sio ya muhimu ni bora tuondokane nayo tufanye jambo lingine”, amesema Dkt. Biteko.

Amewataka viongozi wa SHIMMUTA kuwatembelea waajiri na kuwahimiza waajiri kuwaruhusu watumishi kushiriki katika mashindano hayo, “hakuna jambo linalouma kwamba baadhi ya watumishi wengine wanashiriki na wengine wanapewa visingizio jambo ambalo halikubaliki kwa namna yoyote na sio sawa,”amesisitiza Dkt. Biteko

Amesema SHIMMUTA haina sababu ya kujipongeza kwa kuvunja rekodi ya kupata washiriki ilhali yapo mashirika mengi ambayo viongozi wake hawajatuma washiriki katika mashindano hayo huku akitoa mfano kuwa kujipongeza kwa hatua hiyo ni sawa na kushangilia goli la kujifunga.

Amefafanua kuwa kutekeleza maelekezo ya serikali kuhusu kushiriki katika michezo kutapunguza gharama na kuwaepusha watumishi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza sambamba na kuongeza tija na ufanisi kazini.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi, Dkt. Batilda Burian amewapongeza washiriki na waandaaji wa mashindano hayo na kuwahakishia utayari wa mkoa kuendelea kuboresha mazingira kwa ajili ya kuwezesha ushiriki mzuri zaidi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa SHIMMUTA Taifa, Roselyne Massam ameishukuru serikali kwa kutoa fursa inayowawezesha watumishi kushiriki michezo na hivyo kuwa nyenzo ya kuongeza mshikamano miongoni mwa watumishi kwa ujumla.

Ameiomba Serikali kuwezesha ukamilishaji wa sera ya taifa ya michezo ya SHIMMUTA ili kuweka msingi wa ushiriki na umuhimu wa mashindano hayo kwa watumishi.

Jumla ya watumishi 4720 kutoka mashirika ya umma 96 wanashiriki mashindano hayo yanayoendelea Jijini Tanga.