Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Imeelezwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan anatamani Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) uanze mapema ili Watanzania wapate umeme wa uhakika.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 24, 2023 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko alipokutana na kufanya kikao na ujumbe wa Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi kutoka nchini Misri, Dkt. Assem Elgazzar kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa JNHPP jijini Dar es Salaam.
Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais Samia ana mategemeo makubwa kuhusu kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo na anatamani mwanzoni mwa mwaka 2024 utekelezaji wake uanze na kuongeza kuwa mradi wa JNHPP ndio mwarobaini wa kutatua changamoto ya hali ya upatikanaji wa umeme nchini.
Aidha, Dkt. Biteko ameishukuru Serikali ya nchi hiyo kwa kuonyesha ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huo kwa wakati na kusisitiza kuwa, Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Kwa upande wake, Waziri wa Nyumba, Nishati na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Elgazzar ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuiamini nchi hiyo katika kutekeleza mradi huo. Pia amesema mradi huo utakua wa mfano katika ufuaji wa umeme.
Naye, Balozi wa Misri nchini Tanzania, Mhe. Sherif Ismail ameahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo wa Bwawa la kufua umeme la JNHPP.
Mradi wa Bwawa la kufua umeme la JNHPP unatekelezwa na kampuni ya Arab Contractor kutoka nchini Misri na hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 92.74, na mwezi Januari 2024 majaribio ya mradi huo yataanza.
Kikao hicho kilihudhuriwa na ujumbe wa TANESCO, Kampuni inayotekeleza mradi wa JNHPP (Elsewedy Electric na Arab Contractors) ya nchini Misri na Wawakilishi kutoka Wizara ya Nishati.