
📌 Azindua taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za maji mwaka 2023/24
📌 Upotevu wa maji wasababisha hasara ya shilingi bilioni 114.12
📌 Maganzo yaibuka kidedea, Rombo yavuta mkia utoaji wa huduma
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za maji kwa mwaka 2023/24 na kusema upatikanaji wa huduma za maji ni haki ya msingi hivyo ni muhimu kulinda vyanzo vya maji kuwezesha upatikanaji wake na kuzitaka mamlaka zote nchini kupunguza upotevu wa maji.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Machi 19, 2025 jijini Dar es Salaam ambapo amesema pamoja na jitihada zinazoendelea jamii ina wajibu wa kuhakikisha usafi wa mazingira, kupanda miti na kuhifadi misitu ili kuendelea kupata na kutumia rasilimali maji.

“Tusipotunza vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira tutajikuta katika mtanziko mkubwa (water stress),” amesema na kuongeza kukosekana kwa rasilimali maji kwa baadhi ya watu kinaweza kuwa chanzo cha migogoro na machafuko katika jamii husika.
Ili kukabilikana na hali hiyo na kumwezesha kila Mtanzania kupata huduma za maji na usafi wa mazingira, Dkt. Biteko amezielekeza mamlaka za maji kupunguza kiwango cha upotevu maji ili kuepusha hasara ya shilingi bilioni 114.12 iliyotokana na upotevu huo kwa mwaka huu.
Hadi sasa asilimia 84 kwa mijini na asilimia 79.6 kwa maeneo ya vijijini zimeunganishwa na huduma ya maji ambapo kuna ongezeko la asilimia 7 kutoka kipindi cha mwaka uliotangulia.
Awali, Waziri wa Maji, Mhe. Juma Aweso amesema kumekuwa na ongezeko la ubora wa viwango vya maji na udhibiti wa upotevu wa maji ambao unasababisha hasara kubwa hasa unapothamanishwa kifedha.

Hata hivyo ameipongeza EWURA kwa kazi nzuri na kutoa taarifa inayoonesha uhalisia wa mambo huku akisema mamlaka zinazofanya vizuri zinapata tuzo ikiwa ni motisha ya ushindani wa kimaendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Profesa Mark Mwandosya ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa kipaumbele na kuongeza bajeti ambayo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 206 mwaka 2010/11 hadi shilingi bilioni 558 mwaka 2024/25
Amesema uwekezaji wa katika sekta ya maji unaleta faida zaidi ya mara saba ya mtaji ambapo uwekezaji wa dola 1 unaweza kuleta faida ya dola 7 katika Uchumi wa taifa.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt. James Andelile amesema pamoja na mafanikio yaliyofikiwa bado kuna changamoto kadhaa zinazotokana na utegemezi wa Mamlaka za maji kwa Serikali.
Pia, amesema changamoto nyingine ni uchakavu wa miundombinu ya maji inayosababisha upotevu wa maji na hasara kwa serikali.
Mamlaka za maji zilizofanya vizuri katika udhibiti wa upotevu wa maji na asilimia ya maji yanayopotea ni Maganzo 4%, Nzega 6%, Kashuwasa 11%, Biharamulo 12% na Mwanuzi 13%.
Mamlaka zilizoshindwa kudhibiti upotevu huo kwa kiwango kikubwa ni Rombo 70%, Handeni 69%, Mugango/kyabakari 68%, Ifakara 56% na Kilindoni 55%.
Dkt. Biteko akiwa Mgeni rasmi ametoa tuzo na vyeti kwa mamlaka za maji zilizofanya vizuri katika utoaji wa huduma kwa wananchi.




