Ashiriki Kumbukizi ya Askofu wa Kwanza AICT

πŸ“Œ Asema Vikwazo Visiwavunje Moyo Viongozi wa Dini

πŸ“Œ Uandikishaji Daftari la Wapigakura Mwanza Oktoba 11 hadi 20 Mwaka Huu

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaasa wanajamii kutenda matendo mema ya kuigwa na vizazi vijavyo ili kuweka historia na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Oktoba 6, 2024 katika Ibada ya Kumbukizi ya Askofu wa kwanza wa Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT), Jeremia Mahali Kisula iliyofanyika Kanisa Kuu (AICT)Makongoro Jijini Mwanza.

β€œ Leo Askofu Kisula ametajwa sana kwa sababu ya maisha yake miaka 40 baada ya kifo chake. Mtu huyu alifanya kazi ya kutangaza injili katika mazingira yale ambayo leo tunajiuliza mtu anawezaje kusafiri wakati huo bila uwepo wa miundombinu na vyombo vya kisasa kama ndege na SGR,” amesema Dkt. Biteko.

Amefafanua kuwa historia itamtaja marehemu Askofu Kisula kama kiongozi wa kwanza wa AICT na kuwa ni lazima kuendelea kumkumbuka kwa kazi kubwa aliyofanya katika kanisa hilo.

β€œ Maisha yetu ni lazima yawe ya kuacha alama ili watakokuja nyuma yeti wakute tuliyoacha mazuri au mabaya na kwa maisha ya kawaida mtu atachukua mema na kuepuka mabaya . Viongozi na waumini tujue viongozi wana uwezo kutuelekeza kwenye jambo au maono fulani na kutufanya tuamini, tuna wajibu mmoja wa kumuenzi Askofu huyu kwa yale yote aliyotufundisha na hasa kujitegemea.” Amesisitiza Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa waumini wa AICT wana wajibu wa kuhakikisha wanaendeleza kanisa na utamaduni wa kujitegemea kwa kutoa michango mbalimbali inayolenga kuimarisha kanisa.

Sambamba na kupongeza familia kwa kushiriki ibada ya shukrani huku akiwataka kuendeleza umoja miongoni mwao.

Akizungumzia viongozi wa dini wa AICT, Dkt. Biteko amewaasa viongozi hao kuendeleza kazi yao ya utumishi bila kujali vikwazo mbalimbali wanavyokumbana navyo. β€œ Dunia hii ina sauti mbili ya ndani na nje, isikilizeni sauti ya ndani na msisikie ya nje ambayo itawavunja moyo, waumini tutaendelea kuwa sauti ya nje iliyo njema,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amesema kuwa Mhe. Dkt. Rais Samia anaamini kuwa anaiongoza nchi isiyo na dini ila wananchi wake wana dini na kuwa amewaelekeza viongozi wa Serikali kusikiliza maoni ya viongozi wa dini na kuifanyia kazi ili mchango wao utumike kujenga nchi na Taifa lenye umoja.

Akihubiri katika ibada hiyo Makamu Askofu Mkuu Zakayo Bugota amesema kuwa utamaduni wa kushukuru Mungu kwa ajili ya maisha ya mtu aliyefariki dunia ni utaratibu mzuri unaostahili kuendelezwa ikiwa ni njia mojawapo ya kuwaenzi viongozi waliitenda mambo mema wakati uhai wao.

β€œUnapoishi nini utaachia jamii yako ili ukumbukwe na kuigwa, sio tu kuishi jamii yangu au kanisa langu watapata nini cha kuiga?,” amesema Makamu Askofu Bugota.

Ametaja sifa mojawapo ya Askofu Kisula kuwa hakutaka Kanisa la AICT kuwa tegemezi hivyo alitaka lijitegemee kwa kuhimiza waumini wake kujitoa kwa ajili ya kujenga kanisa hilo.

Makamu Askofu Bugota ameongeza β€œ Askofu Mzee Jeremia Kisula na sisi tusisitize jambo la imani ya kumfuata Yesu Kristo inapaswa kuwa imani ya kuigwa na turithishe watoto wetu, na tuonyeshe mfano mzuri wa kumfuata Yesu bila kubadilika.”

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Hassan Masala amemshukuru Askofu wa AICT kwa kuendelea kutoa huduma na kushirikiana na Serikali katika masuala mbalimbali yanayolenga kuleta maendeleo ya wananchi.

Pia, amesema kuwa wakati Watanzania wakielekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27 Mwaka huu, wakazi wajitokeze kujiandikisha kwenye daftari la wapigakura tarehe 11 hadi 20, mwaka huu ili kupata kuwachagua viongozi wanaofaa.

Ametumia fursa hiyo kuwaalika wananchi katika tukio la Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere ambapo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Naye, mtoto wa marehemu Askofu Jeremia Mahali Kisula, Adella Kisula amesema kuwa shukrani ni neno lenye upendo na neema na kuwa wameshiriki ibada hiyo ikiwa ni ishara ya alama aliyoiacha baba yao.