Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Chalinze
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ,Dotto Biteko, ametoa rai kwa wana-CCM kufanya siasa za kubadilisha maisha ya Watanzania katika kuwaletea maendeleo badala ya kufanya siasa za maneno matupu zisizojibu hoja.
Aidha amewaasa watumishi wa umma kuwahudumia wananchi na kuwafuata walipo pasipo kuwasubiria walete kero zao kwenye madawati.
Akitoa rai hiyo wakati wa mkutano maalum katika Jimbo la Chalinze na kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2020-2023, Biteko ameeleza ni wakati kwa wanaCCM kujibu kwa hoja kutokana na mafanikio makubwa yanayofanywa na Serikali kupitia ilani ya 2020-2025.
Hata hivyo ,Biteko amesema ameridhishwa na namna Halmashauri ya Chalinze inavyosimamia fedha za miradi.
Wakati huo huo, akitoa nasaha Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt.Jakaya Kikwete ambae pia alikuwa mbunge wa kwanza Jimbo la Chalinze amesema, uteuuzi wa Naibu Waziri Mkuu Biteko si jambo la kushangaza kwani ni Naibu Waziri Mkuu wa tatu sasa.
Amesema ,Rais Samia Suluhu Hassan amefanya chaguo sahihi ,katumia mamlaka yake ya kikatiba.
Akielezea utekelezaji wa ilani 2020-2023 , mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete, amesema utekelezaji umefikia asilimia 96 ,na sasa hatua waliyofikia inawabeba kutembea kifua mbele.
Kuhusu sekta ya maji ,ameeleza awali kulikuwa na asilimia 62 inayofikisha huduma ya maji kwa wananchi lakini sasa imefikia asilimia 96 ya upatikanaji maji.
Ridhiwani amesema, tayari sh. Bil. sita zimepokelewa katika Halmashauri ya Chalinze kutekeleza mambo mbalimbali ya maendeleo na kuondoa vikwazo vilivyokuwepo awali.