📌 Asisitiza Serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na wawekezaji wa Modern Industrial Park wanaomiliki kongani ya viwanda eneo la Kibaha, Mkoani Pwani.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo tarehe 24 Juni, 2024 katika ofisi za Naibu Waziri Mkuu Bungeni, jijini Dodoma.
Aidha, Dkt. Biteko amewaeleza wawekezaji hao kuwa Serikali iko tayari kushirikiana nao na kuwapatia umeme kwa ajili ya kuwezesha shughuli za uwekezaji katika eneo hilo.
Naye, Mwakilishi wa kampuni ya Modern Industrial Park, Bw. Yusuf Manzi alisema kuwa eneo hilo lina uwezo wa kubeba viwanda 202 vya aina mbalimbali na tayari miundombinu wezeshi kama maji, Ulinzi na usalama pamoja na barabara vimeshawekwa kwa ajili ya kurahisisha uwekezaji katika eneo hilo ambalo lina uhitaji wa 200MW za umeme kwa ajili ya kutumika na wawekezaji.